The House of Favourite Newspapers

BABU SEYA AIBULIWA MAFICHONI

DAR ES SALAAM: ALIPOFUNGWA kifungo cha maisha kwa kosa la ubakaji na ulawiti, mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ mali zake nyingi ikiwemo nyumba zilisambaratika; hata alipotoka jela watu walijiuliza ataishi wapi na maisha yake yatakuwaje?  

 

Gazeti la Ijumaa linayo majibu ya maswali hayo kwa sababu limefanikiwa kumuibua mwanamuziki huyo kutoka mafichoni na kufanya naye mazungumzo hoti. Kwa msingi huo hakuna haja ya kujiuliza anaishi wapi kwa sasa, kwa nini haonekani mitaani na vipi kuhusu hatma yake kimuziki; papara isiwepo kwa kuwa Ijumaa limesheheni maelezo ya kina kuhusu mzee huyo ambaye ni raia wa nchi ya DRC Kongo.

 

TUJIKUMBUSHE

Juni 25, 2004, Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji na ulawiti watoto 10 waliokuwa wanafunzi wa shule ya msingi Mugabe jijini Dar es Salaam.

Desemba 9, 2017 mwaka jana Rais John Magufuli aliwapa msamaha wafungwa hao ambapo walirudi kuishi uraiani ambako mali walizokuwa wamezichuma wakati huo nyingi zilikuwa zimesambaratika.

IJUMAA LASAKA ALIKOFICHWA

Mara baada ya kuwepo kwa madai mengi kuwa mwanamuziki huyo alipotoka gerezani amefichwa na watu wasiojulikana ambao wamepanga kufanya naye projekti nyingi za kupiga fedha; Ijumaa lilianza kazi ya kumsaka kila kona. Awali watoa taarifa walisema, anaishi Masaki, ambako hakuwepo na hata maeneo mengine ya Mikocheni, Kijichi na Upanga yaliyotajwa nako hakupatikana kama ilivyodaiwa.

 

BABU SEYA ANAISHI WAPI?

Swali la kwanza linaloulizwa na wengi ni kuwa mwanamuziki huyo anaishi wapi kwa sasa kutokana na nyumba yake iliyokuwa Sinza eneo la Palestina kuuzwa kipindi akiwa na matatizo.

Jibu la swali hilo ni kwamba Ijumaa limebaini kuwa anaishi eneo la Mbezi, Bahari Beach jijini Dar kwenye jumba la kisasa. “Nilipotoka gerezani nikaja kuishi huku, si kwamba nimejificha ila nimeamua kutulia nafanya mambo yangu,” alisema Babu Seya wakati wa mahojiano na Ijumaa lililofika kwenye nyumba hiyo anayoishi.

 

NYUMBA NI YA NANI?

Babu Seya anajibu: “Hii ni nyumba ya marehemu rafiki yangu ambaye niliishi naye kama ndugu, anaitwa Jofrey Gondwe. “Nilipotoka Kongo mwaka 1972 nilianza kufanya kazi ya muziki, moja ya bendi niliyoipigia ni Tabora Jazz, nikiwa huko ndiyo nilikutana naye, tukawa marafiki na baadaye tukawa kama ndugu kabisa. “Nilipopata matatizo alikuja gerezani kunitembelea, tuliongea mengi lakini wakati anaondoka aliniambia kuwa hatutaonana tena.

 

“Wakati huo sikuelewa nilijua ni maneno tu, ila naweza kusema ni mtu aliyekuwa ananitia moyo sana na kuniambia ipo siku nitatoka gerezani. “Hata mimi niliamini hivyo. Siku natoka sikuwa najua nitafikia wapi, nilijua nitaishi kwa rafiki zangu. “Nilipoachiwa alikuja mwanamke mmoja akiwa na watu wengine, nilipomtazama nikamkumbuka kuwa ni mke wa rafiki yangu na ndugu zake Gondwe,” alisema Babu Seya.

SIMULIZI ILIYOMLIZA

“Tulipofahamiana na shemeji yangu, nikamuuliza kuhusu ndugu yangu Gondwe akaniambia ameshafariki kama miaka mitatu iliyopita; nililia.

“Shemeji aliniambia kuwa rafiki yangu kabla ya kufariki aliacha wosia kuwa anaamini nitatoka jela na nikitoka nisihangaike pa kuishi niende nikaishi kwenye nyumba yake niungane na familia yake. “Ndivyo ilivyokuwa, mimi niko hapa kwa marehemu rafiki yangu; namshukuru na kumuombea heri kwa Mungu,” alisema Babu Seya.

 

VIPI KUHUSU MUZIKI

Aliongeza kuwa kuhusu kutoonekana kwenye majukwaa kufanya kazi ya muziki kama anavyofanya mwanaye Papii Kocha, Babu Seya alisema: “Kuna vitu nakamilisha kwanza; nimeomba nipatiwe uraia wa Tanzania ambao mipango yake inakwenda vizuri naamini siku si nyingi nitakuwa nimepata. “Kwa sasa kuna nyimbo naandaa kwa kushirikiana na Papii, kwa hiyo mambo yakikaa sawa tutakwenda kuzirekodi na kuanza kusikika.”

GIGY MONEY; Mimi ni mzuri wanaume wanapagawa/ Cardi b ameniiga

Comments are closed.