The House of Favourite Newspapers

Bajeti Kuu ya Serikali Kupigiwa Kura Leo

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muunganom wa Tanzania, leo wanatarajiwa kupiga kura kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali ya 2019/20 ya Sh trilioni 33.11 kwa kuitwa majina na kupiga kura ya Ndiyo au Hapana. Bajeti hiyo Kuu ya Serikali itapitishwa kama kura za Ndiyo zitakuwa nyingi zaidi ya kura za Hapana.

 

Ikiwa kura za Hapana zitakuwa nyingi zaidi, Bajeti Kuu ya Serikali haitapita na moja ya athari ya tukio hilo ni Rais kuwa na mamlaka ya kulivunja Bunge endapo litakwamisha Bajeti Kuu ya Serikali kupita.

 

Kwa kawaida upigaji wa kura, huongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai. Matokeo ya kura zilizopigwa, yatatangazwa na Katibu wa Bunge, Steven Kigaigai jioni baada ya wabunge wote waliopo bungeni kupiga kura. Idadi ya wabunge waliopo bungeni, wa CCM ni 288, Chadema 62, CUF 39, NCCR Mageuzi 1 na ACT Wazalendo 1.

 

Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016, Kifungu cha 107 (1) kinaeleza kuwa Mjadala kuhusu Bajeti ya Serikali utakapomalizika, Spika atalihoji Bunge litoe uamuzi wake wa kupitisha au kutokupitisha bajeti ya serikali ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 90 (2) (b) ya Katiba.

 

Kifungu cha 107 (2) cha Kanuni hizo, kinasema Uamuzi wa Bunge wa kupitisha au kutokupitisha Bajeti ya Serikali, utafanywa kwa kupiga kura ya wazi kwa kuita jina la mbunge mmoja mmoja. Bajeti hiyo ya serikali iliwasilishwa bungeni Juni 13, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, na imejadiliwa na wabunge kwa wiki nzima tangu Jumatatu, Juni 17 hadi leo.

 

Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Mpango alisema mapendekezo ya serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2019/20 ni ya Sh trilioni 33.11, kati yake Sh trilioni 20.86 sawa na asilimia 63.0 ya bajeti, ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, zikijumuishwa Sh trilioni 9.72 kwa ajili ya ulipaji deni la serikali na Sh trilioni 7.56 kwa ajili ya mishahara.

 

Dkt. Mpango alisema Sh trilioni 3.58 zimetengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo, zikijumuisha Sh bilioni 460.5 kwa ajili ya matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya halmashauri.

UCHAMBUZI : Uwepo Wa Maabara Zisizo Rasmi, Nani Alaumiwe.? | 255FRONTPAGE

Comments are closed.