The House of Favourite Newspapers

Barclays yaitikia wito wa BoT, yafungua duka la kubadilishia fedha za kigeni

Mkurugenzi Kitengo cha Mauzo ya Fedha za Kigeni wa  Benki ya Tanzania, Esther Maruma (katikati), akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa duka la kubadilishia fedha za kigeni la benki hiyo. Wengine  kushoto ni, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano, Aron Luhanga na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Oscar Mwamfwagasi.
Mkuu wa Kitengo cha  Wateja Binafsi wa Benki ya Barclays Tanzania, Oscar Mwamfwagasi (mbele kulia), akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa duka la kubadilishia fedha za kigeni la benki hiyo. Kulia kwake ni  Mkurugenzi wa Kitengo cha Mauzo ya Fedha za Kigeni, Esther Maruma na Mkuu wa Masoko na Mawasiliano, Aron Luhanga.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mauzo ya Fedha za Kigeni wa  Benki ya Barclays Tanzania, Esther Maruma (wa pili kulia), akishikana mikono na Meneja  Mauzo wa Hoteli ya Serena, Shaban Kaluse wakati wakizindua rasmi duka la kubadilishia fedha za kigeni la benki hiyo  jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Oscar Mwamfwagasi na Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Barclays, Aron Luhanga.

 

KATIKA  kuunga mkono juhudi za Benki Kuu ya Tanzania ya kuhakikisha huduma ya kubadilishia fedha za kigeni inafanyika kwa kufuata sheria na vilevile hakuna uhaba kwa wataohitaji huduma hiyo, benki ya Barclays Tanzania imefungua kituo cha kubadilishia fedha katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

 

 

Uhaba wa sasa unatokana na uamuzi wa Benki Kuu kufunga maduka ya fedha yanayokiuka sheria za endeshaji , na kuyataka mabenki  ambayo kimsingi yamekuwa yakibadilisha fedha za kigeni katika matawi yao  kujikita rasmi sasa kutoa huduma hiyo kwa kiwango kinachokidhi utashi wa soko.

 

 

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dar es Salaam leo Mkurugenzi  wa Kitengo cha Mauzo ya Fedha za Kigeni wa Barclays, Esther Maruma, alisema, “ Mkakati huu unalenga kukidhi  haja za ubadilishaji wa pesa za kigeni taslimu, ili kuziba uhaba unaotokana na maduka ya  fedha kufutiwa  leseni zao za biashara. “

 

 

Alisema ufunguzi huo  ni mwanzo wa mkakati wa benki hiyo kupanua wigo wa huduma hiyo, na kwamba vituo zaidi vitafunguliwa katika siku za usoni, ili kuwapa nafasi wateja wanaotaka kubadilisha fedha kwa njia ya halali kupata huduma hiyo kwa urahisi na kwa gharama nafuu zaidi.

 

Akitoa ushuhuda wa ukubwa wa uhaba wa huduma hiyo, Meneja wa Mauzo wa Serena, Shaban Kaluse alisema walilazimika kutenga  fedha na kuziweka kibindoni float), ili kuwapa mkopo wateja wao ambao walikuwa wanajikuta wanahitaji fedha za kigeni nyakati ambazo mabenki nayo yamekwisha fungwa.

 

Kituo hicho cha Serena kwa mujibu wa Kaluse kipo katika eneo lenye uhitaji mkubwa sana wa huduma za kubadilisha fedha za kigeni jijini Dar es Salaam. Akiongelea huduma za kituo hicho, Mkuu Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa Barclays,  Aron Luhanga a,lisema kitafanya kazi siku saba kwa wiki.

 

Naye Mkuu wa  Kitengo cha Wateja Binafsi wa Barclays, Oscar Mwamfwagasi, alisisitiza kuwa huduma hiyo ya kubadilisha fedha itafanyika kwa kufuata taratibu na kanuni zilizopo, ikiwemo wateja kuonyesha vitambulisho na uthibitisho wa haja ya kupata fedha za kigeni kwa wanaotarajia kusafiri.

 

Uamuzi wa Benki Kuu kuhamisha imani ya kufanya biashara za ubadilishaji fedha za kigeni kwenda kwa  mabenki ya biashara unafuatia operesheni ya ukaguzi wa maduka ya fedha za kigeni uliofanywa na hivyo,  ambao uligundua kuwepo kwa ukiukaji mkubwa wa taratibu na kanuni za uendeshaji.

 

Katika kutilia mkazo uzito wa ukiukaji wa taratibu uliobainishwa kwenye operesheni hiyo, hivi karibuni Rais Dkt. John Magufuli alisema moja ya sababu za kuyafunga maduka mengi ya kubadilishia fedha za kigeni ni baada ya kugundulika yalikuwa yamegeuka vichochoro vya kutoroshea fedha nje ya nchi.

Comments are closed.