Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeainisha mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Mbarali, ambapo imesema inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Utatuzi wa Migogoro baina ya Binadamu na Wanyamapori (2020-2024), Mkakati wa Kusimamia na Kuhifadhi Tembo Nchini (2023-2033) na Mpango kazi wa Kuongoa Shoroba za Wanyamapori nchini (2022-2026).
Hayo yamesemwa leo Mei 2,2024 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii , Mhe. Angellah Kairuki alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu katika Wilaya ya Mbarali na maeneo mengine nchini.
Ametaja hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na kufanya doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo Tembo , kujenga vituo vya askari uhifadhi ambapo Wizara ina vituo 154 Nchi nzima vikijumuisha ofisi za Kanda kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uhifadhi ikiwemo doria za udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu hususan Tembo kwenye maeneo yenye changamoto.
“Kati ya idadi hiyo, vituo 16 vimejengwa Mwaka 2022/2023 katika Vijiji vya Wilaya za Meatu, Itilima, Busega, Lindi, Rufiji, Liwale, Tunduru, Nachingwea, Mwanga, Songwe, Iringa (V), Nzega, Mvomero, Chamwino, Mpwapwa na Kondoa. Aidha, kwa Mwaka 2023/2024” Mhe. Kairuki amesema.
Amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kujenga vituo vingine 16 katika Vijiji vya Wilaya za Mbarali, Kalambo, Kilwa, Namtumbo, Ruangwa, Serengeti, Bunda (V), Bariadi, Manyoni, Kilosa, Rufiji, Morogoro (V), Korogwe, Same, Babati na Monduli. Ujenzi wa vituo hivyo upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na kutoa mafunzo ya mbinu rafiki za kujikinga na tembo kwa wakufunzi 1,626 kutoka Wilaya 28 kati ya Wilaya 44 zenye changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Vilevile, amesema ili kuendelea kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa elimu kwa jamii ambapo wananchi 2,053 walipatiwa elimu katika vijiji Vitano (5) vya Wilaya ya Mbarali ambavyo ni Ilualanje, Ikanutwa, Vikae, Igunda na Igava vyenye changamoto kubwa ya tembo na pia kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi Wizara yake imetoa mafunzo ya mbinu rafiki za kukabiliana na Tembo kwa wakufunzi 41 kutoka katika vijiji hivyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi inaendelea kuwajengea uwezo jamii kushiriki katika uhifadhi pamoja na kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa kutoa mafunzo kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji (Village Game Scouts – VGS) ambapo katika kipindi cha Mwaka 2021/2022 hadi 2023/2024 jumla ya Askari Wanyamapori wa Vijiji 882 wamepatiwa mafunzo maalum juu ya uhifadhi na mbinu za kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu lengo ikiwa ni kuongeza nguvu na ufanisi katika udhibiti wa matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Aidha, amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake za TAWIRI na TANAPA (Hifadhi ya Taifa Ruaha) imewapatia mafunzo ya ukakamavu, elimu ya uhifadhi na mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu Askari Wanyamapori wa Vijiji 23 kutoka Vijiji vya Igunda, Igava, Iwalanje, Vikae na Ikanutwa katika Kata ya Igava, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali mwezi Aprili, 2022.
Waziri Kairuki amesema Serikali inaendelea kufuatilia mienendo ya wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo tembo na inatumia teknolojia mbalimbali kwa kuwafunga Mikanda Maalumu ya Mawasiliano (GPS-Satellite Collars).
”Mpaka sasa katika mifumo mitatu ya ikolojia tumeweza kufunga katika mikanda 157 katika mifumo mitano Katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2022/2023 hadi 2023/2024 jumla ya tembo 157 viongozi wa makundi wamefungwa mikanda hiyo katika mifumo ikolojia ya Tarangire – Manyara, Serengeti, Selous – Mikumi, Lake Natron – Longido na Selous – Niassa ili kuonesha mahali walipo na hivyo kuwezesha kuwadhibiti mapema kabla ya kusababisha madhara lengo ikiwa ni kuwezesha kuona mahali tembo walipo na kuwadhibiti mapema kabla hawajasababisha madhara” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amesema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa Tanzania ina jumla ya mifumo ikolojia nane (08) inayohitaji jumla ya mikanda ya mawasiliano 200 kwa wakati mmoja ili kurahisisha kupata taarifa za mienendo ya tembo, hivyo, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendeleza juhudi za kuongeza mikanda hiyo kwa kushirikisha wadau wa uhifadhi ukizingatia kuwa gharama ya kufunga mkanda mmoja ni takriban Shilingi Milioni 16 na hivyo kwa mikanda 200 ni takriban Shilingi Bilioni 3.2.
Pia, amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea na operesheni mbalimbali za kutumia helikopta kwa ajili ya kuwafukuza tembo ambao wamekuwa wakizagaa kutoka katika hifadhi kwenda katika maeneo mbalimbali ya wananchi na mpaka sasa operesheni imefanyika katika Wilaya za Nachingwea, Liwale ,Same, Bunda na Mvomero ambapo imefunga mikanda kwa tembo kiongozi na tembo zaidi ya 91 wamerudishwa hifadhini.
Kuhusu Wilaya ya Mbarali Waziri Kairuki amesema Wizara yake imeandaa zoezi la kufunga tembo watatu mikanda tarehe 8 Mei na 9 Mei,2024 ili waweze kufuatiliwa mienendo yao.
Waziri Kairuki amehitimisha kwa kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuongeza vitendea kazi na kununua helikopta tatu ili kurahisisha zoezi la kuwarudisha tembo hifadhini.