The House of Favourite Newspapers

Barua ya Einstein kuhusu Mungu yauzwa mnadani, aliamini Mungu yupo?

 

Barua iliyoandikwa kwa hati ya mkono na Albert Einstein, ambapo anajadili suala la dini na imani, imeuzwa kwenye mnada kwa bei ya karibu $2.9m (£2.3m) ambayo ni sawa na Sh. bil. 7. 

 

Barua hiyo ambayo kwa utani imekuwa ikiitwa “Barua ya Mungu” aliiandika Einstein mwaka 1954 na ilitarajiwa kuuzwa $1.5m (£1.2m) mnadani New York.

 

Mwanasayansi huyo aliyeshinda tuzo ya Nobel, aliandika barua hiyo ya ukurasa mmoja  na nusu akiwa na umri wa miaka 74.

Lilikuwa ni kama jibu kwa mwanafalsafa Mjerumani Eric Gutkind kuhusu baadhi ya kazi zake. Gutkind alikuwa pia Myahudi.

 

Huwa inatazamwa na wengi kama tangazo la msimamo wa Einstein katika mjadala kuhusu sayansi na dini.

“Barua hii yenye uwazi sana, ya kibinafsi iliyoandikwa mwaka mmoja kabla ya kifo cha Einstein inasalia kuwa nyaraka pekee yenye kudhihirisha wazi msimamo wake wa kidini na kifalsafa,” taarifa kutoka kwa waendesha mnada wa Christie inasema.

 

Barua hiyo iliuzwa karibu maradufu ya bei iliyokadiriwa ambayo ilikuwa kati ya $1m-1.5m.

Katika barua hiyo, aliyoiandika kwa Kijerumani na ambayo ilikuwa lugha yake asilia, Einstein amekosoa imani ya sasa kuhusu Mundu.

 

“Neno la Mungu kwangu tu ni jambo la kuelezea udhaifu wa binadamu na ni matokeo ya udhaifu huu wa binadamu,” anaandika.

“Biblia ni mkusanyiko wa hadithi za kale lakini za kuheshimiwa na kutukuzwa, ingawa kwangu zinaonekana zaidi kuwa za kitoto.”

 

Anaendelea: “Hakuna fasiri yoyote, hata iwe ya kina na ya kupambanua zaidi kiasi gani, ambayo kwangu inaweza kubadilisha mtazamo huu wangu.”

 

 

Mwanafizikia huyo pia anajadili asili na utambulisho wake, Uyahudi.

Anaandika kwamba dini hiyo “ni kama dini nyingine zore, ni mtazamo mpya wa hadithi za kale”.

“Wayahudi, ambao najivunia kuwa mmoja wao, na ambao nimejikita kwenye mtazamo wao wa maisha, bado kwangu hawana kitu chochote tofauti na wengine,” ameandika.

 

“Kwa yale niliyoyaona, si bora kuliko binadamu wengine, ingawa wamelindwa dhidi ya saratani mbaya zaidi kutokana na kukosa mamlaka. Kando na hayo, sioni kitu chochote ‘kiteule’ kuwahusu.” (Aliandika hayo miaka michache tu baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kumalizika, ambapo Wayahudi wengi waliuawa na utawala wa Nazi, na pia taifa la Israel lilikuwa bado halijapata nguvu).

 

Hii si mara ya kwanza kwa barua ya Einstein kuuzwa mnadani.

Mwaka jana, barua aliyomwandikia mwanafunzi wa kemia kutoka Italia ambaye alizuiwa kukutana naye iliuzwa $6,100.

 

Iliuzwa pamoja na barua nyingine za Einstein, ikiwemo barua moja ya mwaka 1928 iliyouzwa $103,000. Kwenye barua hiyo alikuwa ameeleza mawazo yake kuhusu awamu ya tatu ya kile ambacho baadaye kiligeuka kuwa nadharia kuhusu uhusiano wa vitu kwenye maumbile, kwa Kiingereza Theory of Relativity.

 

 

Mwaka 2017, barua yake ambapo alikuwa anatoa ushauri kuhusu maisha yenye furaha iliuzwa $1.56m mjini Jerusalem.

 

Barua hiyo yenye aya moja tu, inasema: “Maisha ya utulivu na ya kunyenyekea yatakuletea furaha zaidi kuliko juhudi za kutafuta ufanisi na misukosuko inayoambatana na harakati na ufanisi huo.”

 

Comments are closed.