The House of Favourite Newspapers

Benki ya NBC Yaunga Mkono Jitihada za Kuongeza Ufaulu Somo la Hesabu Jimbo la Ubungo

0
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara ambae pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw Anamringi Macha (Katikati) akimpongeza Meneja wa Benki ya NBC tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Bi Anne Mwaisaka (Kushoto) ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini kupitia ufadhili wake kwenye Mpango wa Kuchochea kiu ya kufundisha na kujifunza somo la Hisabati katika Jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam unaofahamika kama KiuHisabati. Anaeshuhudia ni muasisi na mtekelezaji wa mpango huo Mbunge Jimbo la Ubungo ambae pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Kulia). Hafla ya utoaji wa tuzo hizo kwa walimu wanufaika wa mpango hao imefanyika mwishoni mwa wiki jimboni humo.

 

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini, kwa kufadhili Mpango wa Kuchochea kiu ya kufundisha na kujifunza somo la Hisabati katika Jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam unaofahamika kama KiuHisabati.

Mpango huo ulioasisiwa na Mbunge Jimbo la Ubungo ambae pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo unalenga kuongeza ufaulu kwenye somo hilo kupitia motisha mbalimbali ikiwemo tuzo na zawadi hususani fedha taslimu kwa walimu wanaofaulisha wanafunzi zaidi kwenye somo hilo. Aidha kupitia mpango huo pia wanafunzi waliofanya vizuri somo hilo wananufaika na ufadhili wa mahitaji ya kimasomo wanapofaulu Kwenda kidato cha tano kwa shule za serikali.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara ambae pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw Anamringi Macha (wa tatu kushoto) akikabidhi zawadi ya fedha taslimu Tsh milioni 2 kwa Mwalimu Michael Msembwe (Kulia) kutoka Shule ya Sekondari Kimara ambae aliongoza kwa kufaulisha wanafunzi 20 kwa ufaulu wa Daraja A kwenye somo la Hisabati kwenye mtihani wa Taifa kidato cha nne katika jimbo la Ubungo ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Kuchochea kiu ya kufundisha na kujifunza somo la Hisabati katika Jimbo la Ubungo

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo kwa walimu hao imefanyika mwishoni mwa wiki jimboni humo ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara ambae pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw Anamringi Macha, viongozi waandamizi wa chama na serikali Mkoa wa Dar es Salaam, walimu, wananchi pamoja na maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Meneja wa Benki hiyo tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Bi Anne Mwaisaka.

Akizungumzia hatua hiyo Bw Macha alimpongeza mbunge huyo kwa kubuni mpango huo huku akiishukuru na kuiomba benki ya NBC iangalie namna inavyoweza kuutanua mpango huo uweze kufika maeneo mbalimbali nchini ili uwanufaishe walimu na wanafunzi wengi zaidi hatua ambayo alisema itasaidia kuchochea kasi ya ufaulu wa somo hilo.

‘’Hesabu ndio nguzo mama ya masomo yote kwenye mfumo wa elimu yetu. Jitihada zozote zinazofanywa na wadau mbalimbali kuongeza ufaulu kwenye somo hili zinaungwa mkono na chama pamoja na serikali kwa ujumla. Hii ndio sababu tunampongeza Mbunge wa jimbo la Ubungo kwa ubunifu huu mzuri na zaidi pia tuishukuru benki ya NBC kwa ufadhili wake kwenye mpango huu…tunaomba sana NBC muangalie namna ya kuutanua zaidi mpango huu’’ alisema Bw Macha.

Akifafanua zaidi kuhusu mpango huo Prof Kitila pamoja na kuishukuru benki ya NBC kuwa mfadhili mkuu wa mpango huo alisema unahusisha walimu na wanafunzi watakaopata daraja la A katika somo la Hisabati na wanafunzi watakaofaulu somo la Hisabati kwa kiwango cha daraja A na B.

“Kila mwalimu wa Somo la Hisabati atapata shilingi 100,000/= kwa kila mwanafunzi atakayepata daraja la A katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne katika somo hilo. Mwanafunzi atakayepata daraja A katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne katika somo la Hisabati atanunuliwa vifaa vyote muhimu vya shule, ikiwemo sare, madaftari na vitabu kama atajiunga na shule ya serikali kidato cha tano,’’ alifafanua.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara ambae pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw Anamringi Macha (wa tatu kushoto) akikabidhi zawadi ya fedha taslimu kwa baadhi ya walimu wa somo la hisabati

Kwa mujibu wa Prof Kitila, tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2020 tathmini inaonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaopata alama A na B katika jimbo hilo lakini sio katika kupunguza idadi ya wanafunzi wanaofeli somo la Hisabati.

“Hii inaonesha kuwa programu ya motisha kwa walimu imekuwa na tija katika kuwahamasisha wanafunzi kujifunza zaidi hisabati. Hata hivyo, changamoto bado ni kubwa kwa kuzingatia takwimu kwamba wastani wa ufaulu kwenye somo hili kwa jimbo hili la Ubungo ni asilimia 11 tu huku wastani wa ufaulu kitaifa kwa somo hili ukiwa ni asilimia 19 hadi 20.’’ Aliongeza.

Kwa upande wake Bi Mwaisaka alisema  hatua ya benki hiyo kufadhili mpango huo ni  muendelezo wa jitihada za taasisi hiyo kuunga mkono mipango ya serikali pamoja na wadau mbalimbali yenye nia ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Meneja wa Benki ya NBC tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Bi Anne Mwaisaka (Kushoto) akiwapongeza baadhi ya walimu wa somo la hisabati katika shule za sekondari zilizopo jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam ambao walifaulisha wanafunzi  kwa ufaulu wa Daraja A kwenye somo la Hisabati kwenye mtihani wa Taifa kidato cha nne jimbo la Ubungo ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Kuchochea kiu ya kufundisha na kujifunza somo la Hisabati katika Jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam unaofahamika kama KiuHisabati unaotekelezwa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo ambae pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo kwa ufadhili wa benki ya NBC. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo kwa walimu wanufaika wa mpango hao imefanyika mwishoni mwa wiki jimboni humo.

“Kimsingi ufadhili wetu kwenye mpango huu unalenga kuchochea utoaji wa motisha kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye somo la Hesabu katika mtihani wa kidato cha nne. Tukiwa kama taasisi ya fedha, moja kwa moja tunakuwa wadau wa elimu likiwemo somo la hisabati kwa kuwa shughuli zetu kwa kiasi kikubwa zinazongozwa na hesabu…hivyo tuna wajibu pia wa kuhakikisha ustawi wake,’’ alibainisha.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya walimu na wanafunzi walionufaika na mpango huo, Mwalimu Michael Msembwe kutoka Shule ya Sekondari Kimara ambae aliongoza kwa kufaulisha wanafunzi 20 kwa ufaulu wa Daraja A kwenye somo la Hisabati jimbo la Ubungo alisema ujio wa mpango huo umeongeza chachu na motisha kwa walimu wa somo hilo na wanafunzi kwenye jimbo hilo hatua ambayo alisema inaahidi mustakabali mzuri zaidi katika kuongeza kiwango cha ufaulu wa somo hilo kwa miaka ijayo.

Meneja wa Benki ya NBC tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Bi Anne Mwaisaka (Kulia) akielezea huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kwa wateja walipotembelea banda la benki hiyo kwenye hafla ya utoaji wa tuzo kwa walimu kupitia Mpango wa Kuchochea kiu ya kufundisha na kujifunza somo la Hisabati katika Jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam unaofahamika kama KiuHisabati unaotekelezwa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo ambae pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo kwa ufadhili wa benki ya NBC. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo kwa walimu wanufaika wa mpango hao imefanyika mwishoni mwa wiki jimboni humo.

 

Leave A Reply