The House of Favourite Newspapers

Berlin Yafuta Barabara ya Herman, Yaitwa Lucy Lameck

0

 

Barabara ya  Wissman jijini Berlin, Ujerumani, ambayo imebadilishwa jina na kupewa jina la mwanamke Mtanzania aliyeshiriki kikamilifu kupigania uhuru wa Tanganyika, hayati Lucy Lameck.

 

NA MSIMULIZI WETU

JIONI moja hivi karibuni, mwandishi wa shirika la habari la Uingereza (BBC) kanipigia simu kutaka tufanye mahojiano kuhusu hayati Bi. Lucy Lameck akanifahamisha kuwa mji wa Berlin uko katika mchakato wa kubadili jina la Barabara ya Wissman na kuiita Lucy Lameck.

 

 

Sababu ya kufanya hivyo ni kuwa huyu Hermann Von Wissman alikuwa mtu katili na alifanya mengi mabaya Afrika wakati wa utawala wa Wajerumani.

 

Nilikutana na Hermann von Wissman kwa mara ya kwanza katika mswada alioandika Kleist Sykes kabla ya kufariki mwaka wa 1949.

 

Wakati huo nilikuwa nafanya utafiti wa kitabu cha maisha ya Abdul Sykes.

Kleist Sykes katika mswada huu anaeleza kuwa Herman von Wissman ndiye aliyekwenda Kwa Likunyi kijijini kwa baba yake mkoa wa Imhambane, Mozambique, kufunga mkataba na Chief wa Imhambane, Mohosh, ili atoe jeshi kuja Tanganyika kupigana na wananchi wanaopinga utawala wa Wajerumani.

Hayati Lucy Lameck.

Wissmann na hawa mamluki wa Kizulu wakasafiri kwenda Laurenco Marques wakapanda manowari hadi Pangani.

 

Hili ndilo jeshi lililopigana na Abushiri bin Salim Al Harith Pangani na Chief Mkwawa  huko Iringa.

 

Wissman alifanya ukatili mkubwa wakati wa vita hivi akiua, kuchoma moto vijiji na kuharibu mazao mashamabani ili kusababisha njaa.

 

Katika jeshi hili la mamluki wa Kizulu pamoja na Chief Mohosh ambaye baadaye alikuja kujulikana Tanganyika kama Affande Plantan, alikuwapo Sykes Mbuwane.

 

Uzao wa askari hawa wawili, Sykes na Plantan,  ulikuja kuwa Waafrika mashuhuri katika mji wa Dar es Salaam wakati wa ukoloni wa Mwingereza na wakawa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukoloni na kupigania uhuru wa Tanganyika ingawa Schneider Abdillah Plantan na Kleist Sykes na walikuja kupigana ndani ya jeshi la Wajerumani chini ya uongozi wa Paul von Lettow Vorbeck dhidi ya Waingereza katika Vita Vya Kwanza Vya Dunia (1914 – 1918).

 

 

Katika Vita Vya Pili Vya Dunia (1939 – 1945) wajukuu wa Sykes Mbuwane wakapigana katika vita hivi lakini safari hii wakapigana upande wa Waingereza dhidi Wajerumani waliokuwa washirika wa babu na baba zao.

 

Turudi kwa Wissmann.

Hivi ndivyo Ujerumani na jina hili la Wissmann linavyogusa historia ya koo hizi mbili na baada ya Ujerumani kushinda vita dhidi ya wananchi wa Tanganyika alifanywa kuwa Gavana mwaka 1895.

 

Mji wa Dar es Salaam ulikuwa na sanamu za Wissman katikati ya mji ambazo zilikuja kuondolewa baada ya Vita Kuu vya Kwanza,  Waingereza walipokuja kuwa watawala wapya wa Tanganyika.

Mjerumani Herman von Wissman aliyekuwa Gavana wa Tanganyika 1895.

Hatua ya Ujerumani na mji wa Berlin kufuta jina la raia wao aliyewapigania kuwezesha Ujerumani kuitawala Tanganyika kama koloni lao ni hatua inayoonyesha mabadiliko makubwa ya fikra.

 

Ingetosha tu kwa Ujerumani kufuta jina la barabara na kuipa jina lingine la Mjerumani yeyote wamtakaye lakini kwa kitendo hiki cha kufuta jina la Wissman na kuweka jina la Lucy Lameck ni jambo ambalo wao wenyewe tu ndiyo wanaweza wakalieleza vizuri zaidi.

 

Wajerumani wanasema kuwa wameamua kumpa heshima hii Lucy Lameck kwa ajili ya mchango wake wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

 

Hakika Lucy Lameck anastahili heshima hii.

 

Lucy Lameck ambaye ni mzaliwa wa Kilimanjaro inaanza na kuundwa kwa chama cha Tngnyika African National Union (TANU) Moshi mjini kiongozi akiwa Yusuf Olotu, wakati huo Lucy Lameck akiwa msichana mdogo wa miaka 20.

Sanamu ya Wissman Dar es Salaam jijini Dar es Salaam 1906.

Yusuf Olotu anasema Lucy Lameck alimuunga mkono katika mapambano yake na Joseph Kimalando ambaye ingawa alikuwa mmoja wa waasisi 17 wa TANU Dar es Salaam mwaka  1954, aliporudi Moshi yeye ndiye akawa ndiyo kikwazo kikubwa cha kuisajili TANU na mwishowe akajiunga na UTP,  chama cha Wazungu kuipiga vita TANU.

 

Lucy Lameck alishiriki katika vita hivi pamoja na wanawake wengine ambao  walimzidi umri, kama vile Mama binti Maalim, Amina Kinabo, Halima Selengia,  kwa kuwataja wachache tu.

 

Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 Lucy Lameck akawa mwanamke wa kwanza kuteuliwa na Mwalimu Nyerere kuwa waziri serikalini.

 

Inatia furaha kusikia kuwa Ujerumani imemuadhimisha mzalendo mama yetu huyu aliyepigania uhuru wa Tanganyika.

 

 

Leave A Reply