BILLNASS: Sipendi mwanamke apake make up!

KAMA kawa, kama dawa! Kolamu yako pendwa ya My Style inazidi kupepea. Leo tupo na msanii wa Hip Hop Bongo, William Lyimo ‘Billnass’ ambaye amefunguka mambo mengi yanayohusu maisha yake ya nyumbani, nini anapenda kwa mpenzi wake na nini hapendi, ungana nami kwa mahojiano zaidi:
My Style: Ratiba yako kwa siku pindi unapoamka ikoje?
Billnass: Jambo la kwanza ninapoamka nasali, kisha baada ya hapo nitaingia bafuni kuoga, nikimaliza nitafanya usafi nyumba yangu mwisho ratiba zingine zinafuata, kama kunywa chai na kuangalia taarifa ya habari kwa lengo la kutaka kujua nini kinaendelea ulimwenguni.
My Style: Starehe yako kubwa ni nini?
Billnass: Mimi starehe yangu kubwa ni kulala, yaani siku nikiwa nimefurahi sana basi nitalala vizuri sana.
My Style: Ukiwa na msongo wa mawazo ni jambo gani ambalo huwa unapenda sana kulifanya ili kuirudisha akili yako sawa?
Billnass: Nikiwa na msongo wa mawazo huwa namuomba sana Mungu nipate usingizi maana huwa nikilala ndipo akili yangu inakaa vizuri hata pindi ninapoamka nakuwa mwingine kabisa.
My Style: Unapendelea rangi gani ya nguo?

Billnass: Napenda rangi nyeusi, nyekundu, njano na bluu pia.
My Style: Aina gani ya nguo ukivaa ndio unajiona umetokelezea na unakuwa comfortable zaidi?
Billnass: Nakuwa comfortable zaidi nikivaa pensi, raba na t-shirt yaani nikiwa simple ndio huwa na–enjoy zaidi, kuliko niki-complicate sana.
My Style: Ukiwa unatoka kwenda kwenye shoo au events zozote, nani ambaye huwa anakudizainia nguo au huwa unajidizainia mwenyewe?
Billnass: Inategemea, kuna kipindi huwa nadizaini mwenyewe na kipindi kingine nadizainiwa na Noel, Chidy Designs na wengineo, inategemea na sehemu ninayokwenda.
My Style: Kiasi gani cha pesa huwezi kutoa kununua nguo?
Billnass: Kiukweli hakuna kiasi ambacho siwezi kukitoa kwa ajili ya kununua nguo, kama ikitokea kitu nimekipenda na inatakiwa ninunue na uwezo wa kununua upo, basi nitanunua.
My Style: Ukiwa umetulia nyumbani na familia yako huwa unapenda kufanya nini?
Billnass: Mara nyingi nikiwa nyumbani napenda kuzungumza na familia yangu, kujua kitu gani hakipo, kuna changamoto gani na vitu kama hivyo ili niweze kuviweka sawa.
My Style: Unaweza kutoka na mpenzi wako akiwa hana make up?
Billnass: Ndio napenda, yaani mimi hakuna kitu sikipendi kama make up, kwa sababu sionagi uzuri wa mwanamke akipaka make up.
My Style: Kwa hiyo unataka kumaanisha kwamba mfano umepanga kutoka na mpenzi wako halafu akaja amepaka make up, unaweza kumwambia afute ili abaki natural kwa sababu unakuwa haupo comfortable naye?
Billnass: Kabisa, mimi bora mtu awe natural kuliko apake make up.

My Style: Unapenda kutoka na mpenzi wako akiwa katika muonekano upi wa mavazi?
Billnass: Akivaa kiheshima zaidi, lakini pia kuna muda napenda avae kulingana na mandhari tunayoenda.
My Style: Unapenda chakula na kinywaji cha aina gani?
Billnass: Napenda kula ndizi na kinywaji ninachopenda ni maji aisee yaani kwa siku nakunywa maji mengi sana.
My Style: Unatumia gari gani na gari ipi ni ya ndoto yako?
Billnass: Natumia Toyota Crown, na gari ya ndoto yangu ni Bentley Bentayga.
My Style: Viwanja vyako vikubwa vya starehe kwa hapa Bongo ni vipi?
Billnass: Huwa napenda kutembea sehemu tofauti tofauti, sehemu kubwa ambazo huwa napenda sana kwenda ni Maison, sehemu za baharini na sehemu za party ambazo zipo Masaki.
My Style: Kwa ambao hawakujui vizuri, Billnass ni mtu wa aina gani?
Billnass: Mimi ni mtu mpole sana na mcha Mungu tofauti na watu wanavyodhani, pia napenda sana utani.
My Style: Neno la mwisho kwa mashabiki.
Billnass: Naomba mashabiki wangu waendelee kusapoti kazi zangu, nina wimbo mpya unaitwa Mafioso upo You Tube na nina kazi nyingine nyingi nzuri zinakuja kwa hiyo naomba wasapoti muziki wangu.

