The House of Favourite Newspapers

Bob Haisa aibuka na Mazito

0
Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally (kushoto) akiwa na mwanamuziki Bob Haisa.

 

UNAPOZUNGUMZIA muziki wa Rhumba au Zuku, huwezi kuacha kulitaja jina la Bob Haisa. Ni miongoni mwa wanamuziki wakongwe Bongo ambaye alitikisa enzi hizo na midundo yake mikali mwanzoni mwa miaka ya 2000.

 

Mkali huyu ambaye jina lake halisi ni Haidari Said, miaka hiyo alitamba na ngoma kali kama  Nisamehe, Nipe Mgongo, Ndoa, Chagua Mwenyewe, Nithamini nikiwa hai, Bhatoja, Mbeleko na nyingine nyingi ambazo zilikuwa zikiendelea kuishi masikioni mwa mashabiki zake.

UWAZI SHOWBIZ limezungumza naye stori kadhaa na amefunguka mengi ikiwemo suala zima la kurudi kivingine kwenye gemu, ungana naye hapa chini:

 

Uwazi Showbiz: Tunafahamu wakati unahiti miaka ile ulikuwa Dar, ni kitu gani kilikukimbiza Dar na kwenda kuishi Mwanza?

Bob Haisa: Kwanza nilijipa likizo isiyokuwa na muda maalum, nilitangaza kustaafu muziki kukwepa maswali kadhaa ikiwemo kwamba nitarudi lini ikiwa ni mwaka 2013, upepo haukuwa sawa kwangu.

Vyuma vilikuwa vimekaza na haikuwa na haja ya kulazimisha maisha mazuri ya kitajiri, nikaona bora niende nyumbani.

Uwazi Showbiz: Baada ya kufika Mwanza ulianza kujishughulisha na nini?

Bob Haisa: Nilikuwa nalima, lakini kuna wakati nilikuwa nakusanya makopo na kuyauza hadi kufikia wakati watu kuniita mimi chizi, ilinipa wakati mgumu sana kwa kipindi hicho.

Uwazi Showbiz: Kwa upande wa mashabiki zako, walipokuona unaokota makopo walichukuliaje?

 

Bob Haisa: Walisema nimekuwa chizi, kuna siku nilipokuwa mtaani, mama mmoja aliponiona akaanza kulia kwamba nimerogwa, kwa kipindi hicho niliumia sana ila nikaamua kumuachia Mungu.

Uwazi Showbiz: Una kipaji kikubwa lakini kilififia, unadhani ni kwa nini?

 

Bob Haisa: Kupotea kwangu hakumaanishi kuwa nilififia katika kipaji bali muziki wangu ulizidi uwezo na ufahamu, kuna kipindi liliibuka wimbi la vijana wadogo wadogo ikiwemo waandishi na wasanii wengi ambao walishika vituo vya habari kwa kipindi hicho, tukajikuta muziki umebadilishwa ghafla. Hata uwe na mabavu vipi, usingeweza kufurukuta.

 

Uwazi Showbiz: Je, muziki wako ulikulipa?

Bob Haisa: Mimi muziki wangu ulinilipa, mwanzo sikuwa naangalia mamilioni, bali watu kunitambua kuwa ni mwanamuziki imenitosha, muziki umenirahisishia maisha hata kuingia katika maofisi, nimejenga nyumba yangu (wapi) hiyo ni kumbukumbu tosha.

 

Uwazi Showbiz: Changamoto gani umezipitia nje ya kuporomoka kimuziki?

Bob Haisa: Kwanza unadharauliwa, kutukanwa heshima inavunjika ila cha msingi niliendelea kupambana na maisha hayo.

 

Uwazi Showbiz: Kwa wanaume wengi kufilisika hutokana na kuhonga wanawake, kwako ikoje?

Bob Haisa: Hiyo ni kweli na inatokea, kwa upande wangu sijui kuhonga, mahali naweza kutoa kama nitataka kutoa ila sidhani kama inaweza ikawa sababu ya kufilisika kwangu.

Uwazi Showbiz: Ulisikika ukisema mke alikukimbia baada ya kuporomoka kimuziki, ulijisikiaje na unajisikiaje hata sasa?

 

Bob Haisa: Kwanza sijawahi kusikika nikisema hivyo, ila iliwahi kusikika kwa watu wengine wakisema hilo, kabla ya kuachana na mke wangu tulikuwa tayari hatuko katika harakati za kimuziki, naweza kusema kuwa riziki ya mapenzi ilikuwa imeisha ndiyo maana tukaachana, hatujawahi hata kugombana.

Uwazi Showbiz: Ulidumu na mkeo kwa muda gani hadi kufikia kuachana?

 

Bob Haisa: Nakumbuka tumeishi kimahusiano kabla ya kufunga ndoa tangu mwaka 1996 na tukafunga ndoa mwaka 2011, tumeishi katika ndoa kwa mwaka mmoja, tulidumu miaka 16.

Uwazi Showbiz: Je, kwa sasa umeshaoa mke mwingine ama?

Bob Haisa: Hapana kwa sasa bado sijabahatika kupata mke mwingine.

Uwazi Showbiz: Kipi ambacho unaamini kilikuporomosha kimuziki?

 

Bob Haisa: Nilipotangaza naacha muziki ndiyo kiliniporomosha, maana hata wimbo ambao nilitoa kabla ya kuacha muziki ulikuwa bado unasikika na kufanya vizuri ambao unaitwa Nithamini Nikiwa Hai.

Uwazi Showbiz: Kuna jambo unalolijutia kwenye maisha yako?

Bob Haisa: Jambo kubwa ninalojutia ni kujifunza kunywa pombe, kwa sababu inakula pesa, muda wa kazi na kwa sasa nashukuru nimeacha kutumia pombe.

 

Uwazi Showbiz: Ujio wako Dar unahusiana na nini?

Bob Haisa: Nimerudi kuwasha moto watu wajipange, kwani mwenye muziki wangu nimerudi tena na kwa ujio wangu wanamuziki wa kipindi cha nyuma watapata hamasa.

Uwazi Showbiz: Umeamua kurudi upya kimuziki, uko tayari kwa mapambano na kizazi kipya?

 

Bob Haisa: Nashukuru kitu kimoja, kuna msemo unasema kama umeunda kitu hata aje mtu gani hawezi kukuzidi hata kama vinafana, kwani hakuna msanii ambaye hajawahi kuimba muziki wangu, kwahiyo tutachuana tu.

Uwazi Showbiz: Umerudi kwa staili ipi?

Bob Haisa: Nimerudi kwa staili ya muziki wa vijana wenye midundo na ala za Kiafrika zaidi.

 

Uwazi Showbiz: Je, mashabiki zako wategemee kuona cheche zile za mwanzo au?

Bob Haisa: Zitakuwa zaidi ya zile za mwanzo, kwa sasa nimeujua sana muziki, akili imepanuka nimeongeza ufahamu hata wa kuishi na mashabiki wangu tofauti na zamani.

 

Uwazi Showbiz: Katika nyimbo ulizotoa, ni nyimbo ipi ambayo unaishi nayo hadi sasa?

Bob Haisa: Nisamehe ndiyo wimbo ambao unatibu moyo wangu hata ninapoendelea kuisikiliza nahisi kama nahitaji kuomba msamaha kila wakati. Popote pale nikisikiliza, napata faraja.

Uwazi Showbiz: Mara ya mwisho kupanda jukwaani ni lini?

 

Bob Haisa: Nakumbuka ni mwaka 2013 CCM Kirumba nikiwa na msanii kutokea Uganda Jose Chameleone, umati ulikuwa mkubwa sana, siku hiyo watu walikuwa wamepoa baada ya kupanda mimi watu walipiga shangwe sana.

Uwazi Showbiz: Maisha ya Dar na Mwanza yapi mazuri?

 

Bob Haisa: Dar kugumu sana, Mwanza nilikuwa naishi maisha ya kutulia tofauti na Dar maana hutakiwi kupoteza sekunde hata moja, lazima ujishughulishe.

Uwazi Showbiz: Vipi kuhusu kolabo, umejipangaje?

Bob Haisa: Natamani sana niende Uganda, nifanye na Jose Chameleone na zingine za hapa nyumbani zitakuwepo.

 

Uwazi Showbiz: Neno kwa mashabiki wako.

Bob Haisa: Kwanza wanisamehe kwa kuwakosesha uhondo wa nyimbo zangu kwa muda mrefu, wanipokee kwani nimerudi kivingine na watafurahi.

Makala: Happyness Masunga

Leave A Reply