The House of Favourite Newspapers

Boban Awatia Wazimu Makambo, Tambwe

 

Heritier Makambo

HARUNA Moshi ‘Boban’, leo jioni huenda a k a a n z a kuitumikia timu yake hiyo kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Tukuyu Stars utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Tangu alipojiunga nayo hivi karibuni katika dirisha dogo la usajili akitokea African Lyon, Boban alikuwa hajapata nafasi ya kuitumikia timu hiyo kutokana na kutokuwa na leseni kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lakini sasa ameshaipata.

 

Hata hivyo, washambuliaji wa timu hiyo Mrundi Amissi Tambwe na Mkongomani Heritier Makambo wameweka wazi hisia zao juu ya Boban na kusema kuwa sasa washindwe wao tu kufunga.

Wakizungumza na Championi Jumatatu kwa nyakati tofauti, wachezaji hao walisema kuwa, ujio wa Boban kikosini hapo una faida kubwa sana hasa kwao kwani wanaamini kuwa wataweka rekodi nyingi ambazo walikuwa hawazitegemei katika kuzifumania nyavu.

 

Walisema tangu waanze kufanya naye mazoezi amekuwa akiwatengenezea nafasi nyingi za kufunga, jambo ambalo linawafanya waamini kuwa lazima wataandika rekodi hizo. “Awali mpishi mkubwa wa nafasi za kufunga alikuwa ni Ibrahim Ajibu lakini sasa amepata msaidizi ambaye ni Boban, kusema kweli jamaa anajua, tushindwe sisi tu kufunga,” alisema Tambwe.

 

Kwa upande wake Makambo alisema kuwa: “Boban ni mchezaji mzuri, tangu tulipoanza naye mazoezi tumekuwa tukishirikiana vizuri, naamini atakuwa na mchango mkubwa sana katika kikosi chetu, anajua kupiga pasi za mwisho ambazo hupati tabu kufunga.

 

“Naamini kabisa kupitia kwake pamoja na Ajibu basi tutaandika rekodi nyingi za kuzifumania nyavu, niwaombe tu wapenzi na mashabiki wa Yanga pindi atakapoanza kucheza wampatie sapoti kubwa kama ambavyo wanatupatia sisi.

 

“Lakini pia nimefuatilia rekodi zake nimebaini kuwa ni mchezaji wa kiwango cha juu sana hapa nchini na mwenye mafanikio makubwa katika mchezo wa soka.”

Baadhi ya rekodi ambazo Boban ameziandika katika maisha yake ya soka ni pamoja na kuiwezesha timu ya Simba ambayo ni wapinzani wakubwa wa Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara nne wakati alipokuwa akiitumikia. Aliwezesha kutwaa ubingwa huo mwaka 2004 na 2007 lakini pia akafanya hivyo msimu wa 2009/10 na 2011/12. Pia Boban anakumbwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa msimu wa 2011/12 ambapo aliiongoza Simba kuitandika Yanga mabao 5-0 katika mchezo wa ligi kuu kwenye Uwanja wa Taifa.

STORI NA SWEETBERT LUKONGE

Comments are closed.