The House of Favourite Newspapers

BOCCO AVUNJA REKODI YA MIAKA 15

SIKU chache baada ya Simba kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu Bara, mshambuliaji na nahodha wa Simba, John Bocco amewashangaza wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuandika rekodi ya pekee katika michuano ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Bocco ambaye alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Azam FC, amefanikiwa kuandika rekodi ya kutwaa makombe mawili ya ligi kuu akiwa nahodha wa timu mbili tofauti.

Sasa anakuwa nahodha wa kwanza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na timu mbili tofauti, tangu zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Mara ya kwanza Bocco kutwaa ubingwa wa ligi kuu ilikuwa ni msimu wa 2013/14 akiwa na kikosi cha Azam FC ambapo alikuwa ni nahodha wa timu hiyo lakini pia msimu huu akiwa nahodha wa Simba.

Hali hiyo imewashangaza vilivyo mashabiki wa Simba na kumuona Bocco kuwa ni mchezaji mwenye bahati ya pekee hapa nchini lakini pia akiwa nahodha pekee ambaye ameziongoza timu mbili tofauti kutwaa ubingwa wa ligi kuu tangu rekodi za zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Akizungumza na Championi Jumatatu kuhusiana na suala hilo, Bocco alisema: “Kila kitu huwa ni mipango ya Mungu, namshukuru sana kwa hilo, lakini pia nawashukuru sana wachezaji wenzangu ambao tumekuwa tukipambana pamoja uwanjani kwa ajili ya kuhakikisha tunapata mafanikio hayo.

“Hata hiyo, nichukue nafasi hii pia kuwashukuru viongozi wangu wote pamoja na mashabiki wote waliokuwa wakituunga mkono kwani ushirikiano wao huo ndiyo leo hii umenifanya nifikie mafanikio hayo lakini pia timu yangu.”

Bocco mpaka sasa ameshaifungia Simba mabao 14.

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam.

Comments are closed.