The House of Favourite Newspapers

BODABODA HAINA TIKETI

WAJANJA wanakwambia hiviii, hata gari lina sofa lakini siyo za kutengenezwa kwa mbao, upo nyonyo? Heee eheeeeiyaaaa tangu lini mfuniko wa plastiki ukafunikia nyama kwenye jiko! Wape habari zao Anti Naa ndiyo nimeshaingia tena mjini .Shoga kwani lazima matatizo yako uyapeleke kwa jirani, ebooo! Tangu lini ukatumia mkono wa mwenzio kujikunia? Wakati mwingine tuwe tunaacha kujiweka mbelembele, utakuta janamke zima na watoto watano kama siyo sita kutwa kiherehere kama mita ya luku, halooooo eeeeehhh! Nicheke miye nikinuna utaumbuka!

Baada ya kukupa udambwidambwi shoga leo usishangae kuona unaambiwa bodaboda haina tiketi! Niko na wewe mwanamke mwenzangu maana nimewachamba wababa hadi napigiwa simu naambiwa nipunguze kuwachamba!

Hivi shoga hadi unaolewa na mwanaume tena mwenye kazi zake wewe umekalia tu kuwa mama wa nyumbani inahu? Unashindwa hata kuwa na mtaji wa shilingi elfu 30 ukaanzisha kagenge ka mboga za majani?

Wakati mwingine sisi wanawake tunakera ati! Kutwa mwanamke anaona raha mwenyewe, mumewe amemuandaa anaenda kazini, anarudi na kumkuta yupo palepale, ukimuuliza kutwa amefanya nini utaambiwa amepika, amepiga deki na kuwafulia watoto nguo, shoga umekuwa hausigeli wewe?

Zama hizi si za zamani ati! Maisha ya sasa yamebadilika shoga badilika! Kama mumeo anaingiza chochote ni wakati sasa wa kusaidiana kama elimu unayo kidogo angalia jinsi ya kutafuta kazi au kujiajiri tena ujasiriamali wa siku hizi ni pesa yako tu na ujanja wa kuongea, uongo nyonyo? Sasa weee zubaazubaa kama unayesubiri kuokota dodo kwenye mbuyu!

Kila siku nimekuwa nikipigania na siye tuonekane tuna thamani mbele ya mwanaume, kama hujaolewa unampa hata wakati mgumu atakayekuoa maana atakukuta una kila kitu ndani, una biashara zako, atakupelekeshaje kwa mfano?

Wanawake sisi wengi wao tumekuwa tukipitia manyanyaso mengi kutoka kwa waume zetu kisa hatuna kazi wala mtaji wowote sema tumekuwa wavumilivu sana tu! Wengi wamekuwa wakinya-nyasika si kwenye mapenzi tu hadi kwenye maisha yenyewe, mwanamke una wazazi wako kijijini unataka mwanaume ndiyo awe kila kitu kuwahudumia, kwao ahudumie na kwenu ahudumie jamani? Haya pesa ya kila kitu mpaka mwanaume ndiyo atoe, hadi pesa ya naniiii? Heeee heeeiyaaaa!

Shoga bodaboda haina tiketi, huwezi kukata ukasubiri uje upakizwe upelekwe unapotaka! Badilika mwanamke mwenzangu, maisha kusaidiana, wanaume wengine siyo wa kushauri, ili mradi ana kisehemu chake cha kuingiza pesa mbili tatu hana muda wa kukushauri utafute japo na wewe pa kupata pesa ya kusaidiana maisha.

Zama hizi si za zamani ati! Maisha ya sasa yamebadilika shoga badilika! Kama mumeo anaingiza chochote ni wakati sasa wa kusaidiana kama elimu…

Comments are closed.