The House of Favourite Newspapers

BOSI ADAIWA KUMZALISHA HAUSIGELI, AMTELEKEZA GESTI

0
Binti huyo akiwa na mwanaye.

DUNIA uwanja wa fujo! Bosi mmoja aliyejulikana kwa jina la Jackson mkazi wa Mbagala-Mwanamtoti, Dar, anadaiwa kumzalisha mfanyakazi wake wa ndani aliyetambulika kwa jina la Amina Donisiani kisha kumtelekeza gesti.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Amina alisema kuwa, baada ya bosi wake kumpa ujauzito, mkewe aligundua japo hakujua kama ni wa mumewe ndipo akamrudisha kwao, Kijiji cha Kwa Mtoro, Kondoa mkoani Dodoma ambako alikaa hadi alipojifungua. “Niliogopa kumwambia nani aliyenipa ujauzito ndipo nikarudishwa kwetu, nikajifungua, lakini maisha yalikuwa ni magumu sana, nikawa ninawasiliana na huyo bosi wangu wa kiume na kumweleza hali halisi, akawa ananitumia fedha kidogo za matumizi.

 

“Alifikia uamuzi kwamba nirudi Dar ili anitafutie kazi au anipangishie chumba, akanitumia nauli, nikaja Dar, akanipeleka kwa baba mmoja, akaniambia nikae na kufanya kazi hapo. “Nilikaa kwa siku kadhaa, alipoona ninazungumza na kuzoeana na watu, akaja kunitoa pale baada ya kusikia nimewaeleza watu kuwa mtoto ni wake maana alidanganya kwamba mdogo wake wa kiume ndiye aliyenipa mimba.

“Baada ya kuona pia mkewe amepata taarifa kwamba nimerudi na nina mtoto wa mumewe, ikabidi yule baba anichukue saa 5:00 usiku na kunipeleka gesti iliyopo Kwa Aziz Ali (Dar) ambapo tulikaa siku nne ndipo akaondoka na sikumuona,”  alisema Amina.

MSAMARIA MWEMA AMUHIFADHI

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mama aliyemhifadhi Amina, Christina Mwanjala mkazi wa kwa Aziz Ali alisema kuwa, alikuwa akienda kwenye shughuli zake za kawaida ndipo akakuta watu wamekusanyika wakimshangaa mama huyo, akamsikiliza na kumuonea huruma ndipo akamchukua.

“Niliamua kumchukua na kumsaidia lakini kwa sasa sina cha kumsaidia tena hivyo ninaomba Watanzania na jeshi la polisi linisaidie ili apate haki yake maana ameshafika mpaka ustawi wa jamii, lakini bado suala lake halijapatiwa ufumbuzi na mimi uwezo wangu ni mdogo,” alisema Christina.

MTENDAJI ATHIBITISHA

Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Mwanamtoti, Mbagala, Kabula Igambwa alithibitisha kutokea kwa tatizo hilo na kwamba Amina alipeleka malalamiko ofisini kwake kisha walimuomba namba ya simu ya Jackson na kumpigia ambapo aliwaporomoshea matusi. Baada ya hapo walimpa barua ya wito mkewe ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi ambaye alipofika alijaribu kumpigia simu naye akapokea matusi huku akimtaka kuacha kufuatilia mambo yasiyomuhusu hivyo kuomba msaada kwa jeshi la polisi.

STORI: GLADNESS MALLYA| IJUMAA WIKIENDA

===

VARANGATI: Mgomo wa Daladala DAR Yasimama, Madereva Watoa Yamoyoni

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

Leave A Reply