The House of Favourite Newspapers

Bosi Tff Atua Tunisia Kuongeza Nguvu Stars Ikisubiri Kuivaa Libya

Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao (PICHA NA MAKTABA)

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao ametua mjini Sousse hapa Tunisia na kuungana na Kikosi cha Taifa Stars.

 

Stars ipo mjini hapa kujiandaa kabla ya kuwavaa Libya katika mechi ya kuwania kucheza Afcon, kesho.

Kidao amesafiri kutokea Dubai, UAE alipokuwa na mkutano kuungana na Stars kwa ajili ya mechi hiyo ya pili ya Afcon baada ya ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza dhidi ya Equatorial Guinea jijini Dar es Salaam.

Wilfred Kidao

“Nimekuja kuungana na vijana, najua umuhimu wa pointi tatu za ugenini. Limekuwa ni jambo zuri sana kwa kuwa tulishinda mechi ya kwanza.

“Vizuri kama tukifanikiwa kushinda ya pili, tutakuwa tumejiweka katika nafasi nzuri sana. Hivyo nimeona niungane na makocha na wachezaji kwa ajili ya mechi hiyo,” alisema.

 

Kidao amesema ana imani na maandalizi waliyoyafanya, yaliyobaki yanabaki mikononi mwa makocha na wachezaji na TFF inaendelea kuwaunga mkono bega kwa bega kwa asilimia mia.

 

Kidao alisafiri na ndege kutoka Dubai hadi Tunis, Tunisia kwa umbali wa saa saba moja kwa moja kabla ya kusafiri kwa saa mbili kwa gari kuja hapa Sousse akiungana na wadau wengine.

 

Stars imefanya mazoezi kwenye uwanja utakaochezewa mechi dhidi ya Libya kiwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon, kesho.

 

Kocha Mkuu Ndayiragije, amesema kikosi chake kina hali nzuri na kimejiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo.

“Tuko vizuri kabisa tayari kwa mchezo, Libya si timu tunayoifahamu sana lakini tumefanya maandalizi mazuri na tuko tayari kwa mchezo,” alisema Kocha huyo raia wa Burundi.

 

Ndayiragije ambaye anasaidiwa na Selemani Matola amesema maandalizi ya kikosi hicho ni ya uhakika na wanachosubiri ni mapambano.

 

Mji wa Sousse ni kati ya miji maarufu ya utalii barani Afrika na unaongoza kwa kuzungukwa na mahoteli ya kiss nchini hapa kwa ajili ya watalii.

 

Libya tayari wako hapa na wamekuwa wakiufanya mji huu kama nyumbani kwao.

Tayari Stars imecheza mchezo mmoja wa michuano hiyo na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Equatorial Guinea.

Na Saleh Ally, Sousse, Tunisia

Comments are closed.