The House of Favourite Newspapers

BREAKING: Shule za Hazina, Alliance, Nyingine 6 Zafutiwa Matokeo – Video

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) limezifutia matokeo ya mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya msingi, shule nane za msingi ambazo ni Hazina na New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy za Dar es Salaam, Alliance, New Alliance na Kisiwani za Mwanza  na Kondoa Integrity ya Kondoa  kwa tuhuma za kuvujisha mtihani huo.

 

Hayo yamesemwa leo Oktoba 2, 2018 na Katibu Mtendaji Baraza hilo, Dkt. Charles Msonde alipokuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam na kutoa ripoti ya jinsi mtihani huo ulivyofanyika Septemba 2018.

 

“Ofisa wa Baraza aliyekuwa akifuatilia ufanyikaji wa mtihani katika Shule ya Hazina alikamata kipande cha karatasi chenye maswali ya somo la sayansi kikiwa mahali ambapo hapakustahili, maswali yale yalikuwa kwenye mtihani huo, iligundulika walimu na mmiliki wa shule hiyo waliutafuta mtihani na kuufanya usiku kisha kuwaonyesha wanafunzi wote majibu ili wafaulu, na walifanya hivyo kila siku za mtihani huo.

 

“Walimu hao walihusika kuwachukua wanafunzi wa Shule ya New Hazina usiku na kuwapeleka Shule ya Hazina ili nao wakaonyeshwe majibu hayo. Waliohusika ni Mwalimu Henche (Mkuu wa Shule hiyo), Nasri Bahanzika, Mambo Bakari Idd, Jacob Ochieng na Mussa Juma waliokuwa wakikokotoa majibu na kuwapa wanafunzi.

 

“Baada ya kubanwa walimu hao walibainisha kuwa walitumiwa mtihani huo na walimu wa shule ya Alliance ya Mwanza, na walimu hao wa Alliance walipokamatwa na kupekuliwa kwenye simu zao walikutwa na maswali ya mitihani hiyo kwenye simu zao na walipohojiwa walikiri kutuma mitihani hiyo lakini wakasema walitumiwa na mwalimu Kennedy Malongi wa Shule ya Aniny Nndumi ya Ubungo, Dar. Mwalimu Kennedy alipobanwa alisema alipokea mitihani hiyo kutoka Fountain of Joy,” alisema Msonde.

 

Aidha, wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisiwani iliyopo Mwanza Jiji walikamatwa wakiwa wameandika majibu ya mtihani wa Hisabati kwenye sehemu za miili yao na walipohojiwa walisema walipewa na Mwalimu Mkuu wao alitwaye Mugeta Obeid na inaonekana mwalimu huyo alikuwa na mitihani hiyo hivyo anashikiliwa.

 

Pia, katika Shule ya Kondoa Integrity alikamatwa mwanafunzi aliyekuwa na majibu ambapo baada ya kukamatwa,  wasimamizi walimshtukia yule msimamizi ili kumnyang’anya ile karatasi kupoteza ushahidi lakini wanafunzi waliwataja walimu waliohusika kuwapa majibu.

 

Kwa matukio hayo ya udanganyifu, NECTA imefuta matokeo ya shule hizo, imefuta pia usajili wa vituo hivyo vya mitihani hadi baraza hilo litakapojiridhisha kwamba vituo hivyo vinaweza kuzingatia kanuni za mitihani na kuamuru mtihani huo urudiwe tena wiki ijayo Oktoba 8 na 9, 2018 kutaka walimu hao wachukuliwe hatua. mara moja.

 

VIDEO: MSIKIE MSONDE AKIFUNGUKA HAPA

Comments are closed.