The House of Favourite Newspapers

CAG AANIKA RIPOTI YAKE, “TUTAENDELEA KUTUMIA NENO ‘DHAIFU'”

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad,  ametangaza kuwasilisha ripoti ya ukaguzi bungeni na kusema kuwa mwaka 2017 ofisi yake ilitoa mapendekezo 350, lakini yaliyotekelezwa kwa ukamilifu ni mapendekezo 80 (23%) wakati hati walizotoa mwaka huu ni 548, hati zinazoridhisha ni 531 (97%), na kwamba ubora wa hati unaongezeka mwaka hadi mwaka.

 

Prof. Assad amesema hayo leo Aprili 10, 2019 na kuongeza kwamba, mashirika ya umma yanaongoza kwa kuwa na hati zinazoridhisha huku akitaja mapungufu mbalimbali yaliyobainika kwenye ukaguzi huo.

 

Assad amesema ripoti yake imejikita kwenye kaguzi zifuatazo:

Ukaguzi serikali kuu
Ukaguzi serikali za mitaa
Ukaguzi mashirika ya umma
Ukaguzi miradi ya maendeleo
Ukaguzi TEHAMA
Ukaguzi ufanisi katika sekta 11

 

Aidha,   amesema kulingana na taratibu za ukaguzi wataendelea kutumia neno ‘dhaifu’ katika ripoti za ukaguzi na hata hii aliyoiwasilisha leo, ya mwaka unaoishia Juni 2018, ina neno dhaifu katika maeneo mbalimbali ya ukaguzi.

 

“Eneo la kwanza katika ukaguzi maalum linahusisha Shirika la Bima la Taifa kwa sababu lilinunua mfumo usiofanya kazi ambao ulinunuliwa kwa gharama za Dola za Marekani 3.59 milioni. Tumezoea kufanya mkutano huu mara baada ya ripoti hii kuwasilishwa. Nimetazama TV, ripoti imewasilishwa bungeni na ‘order paper’ ninayo hapa inaonyesha ripoti imekabidhiwa bungeni leo asubuhi na nimetazama ikiwasilishwa.

 

“Mwaka huu tumetoa ripoti yetu kwa CD, ili kuepuka gharama nyingi za uchapishaji. Halmashauri za Kigoma Ujiji na Nyang’hwale zimepata hati zisizoridhisha na hati mbaya katika mwaka wa fedha 2017/18.

 

‘Tumebaini Wilaya ya Hanang’ haikuwasilisha vitabu vya fedha na kuna upotevu wa mapato ya Sh. bilioni 1.4 na walilipa fedha kwa wakandarasi kwa kazi ya dharura pasipo kuwapo kwa kazi ya dharura. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilinunua mashine za BVR 8000 kwa ajili ya usajili wa wapiga kura, mashine 5000 hazikukidhi vigezo na hivyo kutorandana kimatumizi na zile zilizonunuliwa awali na NIDA na RITA na kusababisha hasara ya Sh862.08m,” amesema Assad.

 

Aidha, Halmashauri za Kigoma Ujiji na Nyang’hwale zimepata hati zisizoridhisha na hati mbaya katika mwaka wa fedha 2017/18.

 

Assad amesema wamebaini Chadema ilinunua gari Nissan Patrol kwa Dola 63,720 (TSh147.76m), lilisajiliwa kwa jina la mwanachama badala ya Bodi ya Wadhamini, CCM haijawasilisha NSSF makato ya Tsh3.74b ya wanachama wake. Majengo ya ofisi za CUF yamesajiliwa kwa majina ya watu badala ya Bodi ya Wadhamini.

 

“Serikali ilikuwa ichagie Tsh.118b katika miradi 10 ambayo ina ubia na washirika wa maendeleo lakini imetoa Tsh7.3bilioni sawa na asilimia 6 na kusababisha Tsh111b kutopelekwa kinyume na makubaliano. Tumewaalika wenyeviti wa kamati za Bunge (PAC na LAAC) lakini hawajaja hapa. Tutawapatia nakala hizi. Deni la Taifa limeongezeka lakini bado ni himilivu. Tunaishukuru Ofisi ya Rais na Ofisi ya Bunge kwa kutusaidia kukamilisha ripoti hii.

 

“Mashirika ya umma 14 ikiwemo Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Benki ya TWB yana matatizo ya kifedha na kusababisha kuwa na madeni makubwa kuliko mtaji wake, kati ya mashirika hayo, 11 yana ukwasi hasi na mengine kujiendesha kihasara kwa miaka miwili. Tuliona kuwa kuna miradi 27 yenye thamani inayofikia Sh5.24 bilioni ilikamilika katika mamlaka za serikali za mitaa 16 lakini miradi hii hautumiki, sasa kwa nini ulijengwa kama hutumii.

 

“Eneo la saba na la mwisho katika ukaguzi maalumu ni ununuzi wa sare za askari polisi uliofanywa na Jeshi la Polisi nchini, tulibaini kwamba jeshi lililipa Sh16.66 bn bila kuwepo kwa ushahidi wa uagizaji wala upokeaji wa sare hizo.” – CAG Prof Assad,” amesma Assad.

Comments are closed.