The House of Favourite Newspapers

CECIL MWAMBE: Safari yangu kisiasa haikuwa rahisi

0

Mgombea Ubunge jimbo la Ndanda mkoani Mtwara, Cecil Mwambe amesema safari yake kisiasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita haikuwa rahisi.

Mwambe ambaye kuanzia mwaka 2015 alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema kabla ya Februari mwaka huu kurejea CCM, amefichua namna alivyokuwa anaitumia Ilani ya CCM kabla ya kutoa michango yake bungeni kwa kuwa aliamini ndio Ilani inayosimamia Serikali.

Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo katika Uwanja wa Lukuledi mkoani humo, Mwambe amesema ilimlazimu kufanya hivyo kwa sababu tatizo alikuwa kwenye upande ambao hauamini Ilani ya CCM wakati ndio iliyoivusha Tanzania kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Aidha, alisema safari yake ya kisiasa haikuwahi kuwa nyepesi katika kipindi hicho kwa kuwa ilihitaji nguvu kubwa kusukumana ili kufikia malengo.

” Ndugu zangu mlinichagua ili kuleta mabadiliko, ila bahati mbaya mabadiliko tuliyokusudia hayakuweza kufikiwa huko nilipokuwa ndio maana niliona niungane na ninyi ili kufikia malengo yetu.

“Kuna mambo mengi niliyafanya tukiwa pamoja lakini asilimia kubwa hayakufanikiwa kutokana na mivutano iliyokuwepo ya kisiasa. Sasa niwahakikishie nitashirikiana nanyi baada ya kunipa kura kwa kuniamini katika kipindi kijacho cha miaka mitano,” alisema.

Alisema akiwa bungeni aliuliza maswali 57 na kutoa michango mara 37 lakini kati ya yote ni machache yaliyofanyiwa kazi.

“Ndio maana nikawaambia safari yangu haikuwa rahisi sana lakini sasa niwahakikishie haya yote yanakwenda kutekelezwa.

“Ninachowaomba mniamini na kunipatia miaka mitano tena ambayo tutamalizia kutekeleza mambo hayo ikiwamo ujenzi wa chuo cha kipya cha watoto wenye mahitaji maalumu,” alisema.

Na Mwandishi wetu

Leave A Reply