The House of Favourite Newspapers

CHELSEA na Manchester City Kuonyeshana Kazi leo

CHELSEA na Manchester City leo zinaonyeshana kazi wakati zitakapovaana kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Carabao itakayopigwa kwenye Uwanja wa Wembley jijini London.

 

Fainali ya mwaka huu inahusisha timu zenye mafanikio makubwa zaidi katika mashindano haya, ambapo Chelsea na Manchester City zote zimetwaa taji hilo mara mara tano zikizidiwa na Liverpool iliyonyakua kombe hilo mara nane.

 

Hata hivyo, Manchester City inayotetea ubingwa ndio imetwaa mara nyingi taji la mashindamo haya katika miaka ya karibuni ikiwa imetwaa mara tatu katika fainali tano. Chelsea ilitwaa taji hilo mwaka 2015, nayo Manchester United kwa upande wake walinyakua mwaka 2017. Pia timu hizi mbili zimekuwa na mafanikio katika soka la England kwani tangu msimu wa 2010//11, hakuna timu zilizotwaa mataji mengi zaidi ya hizo mbili.

Timu hizo kwa ujumla wao zimetwaa mataji matano ya Ligi Kuu England, Kombe la FA mara tatu na Kombe la Carabao mara nne.

 

Bila kusahau kuwa Chelsea imetisha barani Ulaya, pia kwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na lile la Ligi ya Europa. Timu hizi zinakutana kwa mara ya nne msimu huu, baada ya kufungua msimu huu wa 2018/19 kwenye Ngao ya Hisani, ambapo Manchester City ilishinda 2-0 na pia zimekutana kwenye mechi mbili za Ligi Kuu England. Mara ya mwisho kwa timu hizi kukutana ilikuwa wiki mbili zilizopita, ambapo Manchester City iliibuka na ushindi wa mabao 6-0.

 

Matokeo hayo yalimletea matatizo kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri, ambapo yupo hatarini kupoteza kibarua chake akifungwa leo. Sarri akitwaa taji hilo leo basi itakuwa mara ya kwanza kutwaa taji hilo tangu aanze kazi ya ukocha tofauti na mwenzake kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, ambaye ametwaa mataji 20.

Guardiola tangu aanze ukocha ameshinda ligi mara saba na kutwaa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ana rekodi ya kupoteza fainali moja tu pale Barcelona ilipofungwa na Real Madrid mwaka 2011 kwenye fainali ya Copa del Rey.

 

Chelsea inaweza kujipa moyo kuwa inaweza kurudia ilichofanya Desemba, mwaka jana wakati ilipoifunga Manchester City 2-0 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge. Ilikuwa mechi ya kwanza kwa Manchester City kufungwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu wa 2018/19.

 

Manchester City itakuwa inamtegemea Kevin De Bruyne, ambaye ana rekodi ya kufunga mabao tisa kwenye michuano hiyo tangu mwaka 2015. Matumaini mengine ya Manchester City yatakuwa kwa mfungaji wao hatari, Sergio Aguero, ambaye amefunga mabao 15 katika mechi 18 alizoivaa Chelsea. Chelsea kwa upande wao watakuwa wanamtegemea Eden Hazard, ambaye amepachika mabao 12 na kutoa asisti 10 kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Comments are closed.