The House of Favourite Newspapers

Chid Benz; Mtazame Ray C, Halafu Jifunze Sasa!

Rashid Makwiro ‘Chid Benz’.

KWAKO mkali wa Hip Hop, Rashid Makwiro ‘Chid Benz’. Habari za siku, mishemishe zinakwendaje? Binafsi mimi sijambo, naendelea na mapambano ya kila siku.

Nimekukumbuka leo ndugu yangu ambaye ninatambua umuhimu wako katika muziki wa Hip Hop Bongo. Najua unaweza kuwa bado hujatoka mahabusu lakini naamini utatoka na utarudi uraiani.

Ndugu yangu, wewe unajua kuutendea haki muziki wa Hip Hop ndiyo maana nina kila sababu ya kukuandikia barua pale ninapoona mambo hayaendi sawa.

Chid naumia kutokana na mfululizo wa matukio yako ya hovyo. Tatizo la madawa ya kulevya kwako linaonekana ni gumu kuliacha. Matokeo yake kila siku unajikuta matatizoni kutokana na matumizi hayo ya madawa ya kulevya.

Nakumbuka uliwahi kupelekwa soba kule Iringa, mambo yakaenda vizuri na afya yako ikaimarika. Chid naikumbuka hali uliyokuwa nayo kabla na baada ya kwenda kule soba. Ulikuwa unatia huruma, wadau mbalimbali wakajitokeza kukusaidia.

Kinachonisikitisha ni kuona bado uliporejea, umerudi kulekule. Watoto wa mjini wanasema gari limewaka. Nimekuona wiki iliyopita ukitangazwa hadharani na Kamanda wa Dodoma, Gilles Muroto kuwa wamekunasa kwenye kundi la wavuta bangi.

Moyo wangu uliumia sana. Akili yangu ilirudi nyuma na kuanza kuwakumbuka wasanii mbalimbali ambao wameondoka duniani huku chanzo kikubwa kikiwa ni madawa ya kulevya.

Chid unamkumbuka marehemu Langa, Ngwair, Dogo Mfaume (Mungu awapumzishe kwa amani) na wengine wengi tu, wameyafupisha maisha yao hapa duniani kwa sababu tu ya madawa ya kulevya.

Chid hujajifunza tu kupitia hao watu? Unataka kuniambia hadi sasa hujatambua madhara ya madawa hayo? Huoni umuhimu wa kuyakataa?

Nafsi yako inashindwa kujiwekea nadhiri ya kuyaacha? Wewe mwenyewe umewahi kukiri mara kadhaa kwamba madawa yamekurudisha nyuma. Madawa yamekufanya udharaulike, uumwe karibia na kufa.

Sasa kweli kwa kuumwa hadi kufikia hali ile, kwa kutazama mifano ya wasanii waliotangulia mbele ya haki bado tu unashindwa kuamua kuacha?

Niliwahi kumsikiliza Q Chillah ambaye naye alitopea kwenye madawa ya kulevya, alisema silaha kubwa iliyomsaidia ili aweze kuachana na madawa hayo ni kuamua yeye mwenyewe kuyaacha.

Chid nafsi yako mwenyewe ndiyo inayoweza kukuponya. Sisi hata tupige kelele ya namna gani lakini kama wewe mwenyewe hujaamua kuacha ni kazi bure.

Amua sasa kuacha madawa ya kulevya, inawezekana. Kama Q-Chillah aliamua na ikawezekana kwa nini wewe ushindwe?

Ray C ameweza wewe una kasoro gani? Hebu basi mtazame mrembo huyo na uone jinsi alivyofanikiwa na wewe hata ufuate nyayo zake.

Ndugu yangu Chid, utafika wakati Watanzania na mimi tutakuchoka, tutakukatia tamaa kitu ambacho sioni kama ni sawasawa.

Viongozi wa Serikali waliwahi kukusaidia, wanapoona umerejea tena kwenye tatizo hilo ni wazi wanaweza kusita kukusaidia kwa mara nyingine.

Nikusihi sana endapo Mungu atakujalia kusoma barua yangu hii, amua wewe mwenyewe kuacha. Jiwekee nadhiri kwamba sasa unaamua kuacha na nina hakika kweli utaacha.

Mungu akusaidie katika safari yako, natamani nikuone tena jukwaani ‘ukizipasua’ spika kwa sauti nzito yenye mamlaka.

Kila la kheri Chid Benz mzee wa Ilalaaaa!

Mimi ni nduguyo;

Erick Evarist

 

 

 

Comments are closed.