The House of Favourite Newspapers

Chirwa, Kwasi Uso Kwa Uso Zenji

KWA sasa wote wawili hawapo katika vikosi vya timu zao, lakini Januari mwakani straika Obrey Chirwa wa Yanga na beki Asante Kwasi wa Simba watakutana Zanzibar katika Kombe la Mapinduzi.

Kaimu Kocha wa Simba, Masoud Djuma amepanga kumjumuisha Kwasi kwenye kikosi atakachokitumia katika Kombe la Mapinduzi mara baada ya mechi yao ya leo Jumamosi dhidi ya Ndanda FC.

Mechi za Kombe la Mapinduzi zinaanza leo kwa Mlandege kucheza na JKU huku Jamhuri ikicheza na Mwenge na Zimamoto dhidi ya Taifa Jang’ombe. Mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kwasi ambaye ndiye aliyekuwa gumzo kwenye dirisha dogo, alisaini Msimbazi akitokea Lipuli FC iliyomuachia kwa dau la Sh25 milioni.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Djuma alisema; “Kwasi atajiunga na mazoezi ya pamoja na wenzake Jumatatu tukirejea kutoka Mtwara.”

Djuma alisema Kwasi ataanza mazoezi ya pamoja na wenzake akiwa tayari amemaliza programu ya mazoezi ya fitinesi ya gym na kukimbia ufukweni ambayo alimpatia.

 

Wakati huohuo, Yanga kupitia kwa Ofisa Habari wake, Dismas Ten imesema straika wake Obrey Chirwa anawasili leo Jumamosi na keshokutwa Jumatatu ataungana na wenzake kwenda Zanzibar katika Kombe la Mapinduzi.

“Chirwa atawasili kesho (leo) kutoka kwao Zambia, huyu hayupo katika kikosi kitakachocheza na Mbao (FC) Jumapili (kesho), lakini Jumatatu ataungana na wenzake kwenda Zanzibar katika Kombe la Mapinduzi,” alisema Ten.

Wilbert Molandi na Ibrahim Mussa.

 

Comments are closed.