The House of Favourite Newspapers

Tuache Kulalamika Kupita Kiasi, Mwaka 2018 Uwe Wa Vitendo

LEO ni Jumamosi ya mwisho kwa mwaka 2017 na hii ni makala yangu ya mwisho kwa mwaka huu. Cha kujiuliza hivi tumepiga hatua yoyote kwenye soka letu? Au bado mambo ni vilevile tu?

Tumekuwa watu wa kulalamika sana siye tunaojiita watu wa mpira na sijui ni nani atatuokoa katika hili. Sijui tumekosea wapi hadi tumekuwa watu wa namna hiyo na tumeshazoea kufanya hivyo.

 

Kuanzia Januari Mosi hadi Desemba 31, watu wa mpira wa nchi hii wanalalamika tu kila mtu analia na lake. Kila mtu analia na mfumo mbovu wa kuendesha soka kwenye nchi hii iliyopata uhuru miaka 56 iliyopita na hapo ndiyo utakapochoka.

 

Nasema utachoka kwa sababu ndani ya miaka hiyo 56 ya Uhuru Tanzania imeshiriki michuano ya Afrika mara moja tu nayo ilikuwa miaka 37 iliyopita na nina hakika hata wasomaji wengi wa makala haya walikuwa bado hawajazaliwa.

Sasa jiulize kwa nini wasilalamike? Lazima watafanya hivyo hawapati kile wanachotaka yaani wao wamekuwa ni watu wa shida tu utadhani wamechaguliwa kupata shida kumbe siyo.

 

Tatizo letu jingine hatujifunzi kutoka kwa wenzetu yaani wamefanyaje hadi wakapiga hatua bali sisi tumekuwa ni watu wazuri wa kuwasifia kuliko kujifunza.

Ukienda kwenye klabu nako ni vilevile tu watu wanalalamika kuanzia Januari hadi Desemba siyo katika Ligi Kuu Bara tu yaani kuanzia timu za chini kabisa hadi juu.

 

Shida tupu kuanzia kwa viongozi hadi kwa wachezaji na hapo kila mmoja anamlaumu mwenzie na kila mtu anamnyooshea kidole mwenzie kuwa anakosea na hapo ndiyo utachoka.

Siyo klabu tu na wachezaji wao bali hata kwenye vyama vya soka vya mikoa na wilaya nako mambo ni yaleyale, malalamiko yamekuwa sehemu ya maisha.

Yaani sisi tumekuwa watu wa kuhangaika na kutatua matatizo kwenye soka letu kila kukicha hata sijui tutayamaliza lini na tuanze kufanya kazi ya kuendeleza soka.

 

Muda unakwenda tena kwa kasi mno na wenzetu wanapiga hatua ila sisi bado tunazuga tu kama hatuoni vile kumbe tunaona na tunajua ila tumeziba masikio yetu na pamba na kujifanya hatusikii.

Hivi lini nchi hii itakuwa na mipango ya uhakika ya kucheza Kombe la Dunia? Najua nimeuliza swali gumu kweli ambalo wengi wanashindwa kulijibu.

Basi tuache kulalamika sana ili na sisi tuwe na mipango ya uhakika na yenye malengo ya kweli ili tuweze kucheza Kombe la Dunia maana mwaka 2022 au 2026 siyo mbali na tukijipanga tutaweza tu.

 

Sasa hapa tujiulize nani atamfunga paka kengele? Nalo hilo ni swali gumu pia na kama hatumfungi paka kengele basi tutaishia huko huko kwenye kulaumiana tu kuanzia mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka.

Basi mwaka ujao unaoanza keshokutwa Jumatatu tuache kulalamika na tufanye kazi ya maendeleo na kila kitu kiende kama kinavyotakiwa kusipo na ubabaishaji na kama tukifanya hivyo nina hakika tutafanikiwa tu bila wasiwasi ingawa sina hakika sana kama tutaweza maana kuna madudu mengi yapo yamejificha tu.

Mwisho kabisa nawashukuru nyie wasomaji wangu wa Besela kwa kuwa pamoja kwa kipindi chote cha mwaka 2017 nawatakia mwaka mpya mwema na tuache kulalamika na mbarikiwe sana.

Kumbukeni kuwa makini kwenye kipindi hiki cha sikukuu na kila kitu tufanye kwa kiasi pia upendo na amani utawale kwenye kila jambo mnalotenda, Ameni.

Comments are closed.