The House of Favourite Newspapers

Chombo cha Anga cha China Tiangong-1 Chaanguka Pacific

CHOMBO cha anga za juu cha China, Tiangong-1 kimemeguka na kuvunjika vipande vipange wakati kikikatiza anga la dunia maeneo ya bahari Kusini mwa Pacific leo Jumatatu, ikiwa ni miaka saba tangu kiliporushwa angani mwaka 2011 kufanyia majaribio ya teknolojia ya kuunganisha vyombo mbalimbali anga za juu na vyombo vya kuzunguka kwenye mzingo wa dunia.

 

Tiangong-1 ni sehemu ya juhudi za China za kuunda kituo cha anga za juu kitakachokuwa kinadhibitiwa na binadamu katika anga za juu kufikia mwaka 2022.

 

Wataalamu wa anga za juu wa Marekani wakisema wametumia teknolojia ya kufuatilia mzingo wa dunia kuthibitisha kuingia ardhini kwa Tiangong-1. Mtaalamu wa anga za juu Jonathan McDowell kutoka Chuo Kikuu cha Harvard ameandika kwenye Twitter kwamba huenda chombo hicho kimeanguka Kaskazini Magharibi mwa Tahiti.

Wataalamu walitatizika kubaini hasa ni wapi chombo hicho kingeanguka. Idara ya anga za juu ya China ilikuwa awali imekadiria kimakosa kwamba chombo hicho kingeanguka karibu na Sao Paulo, Brazil muda mfupi kabla ya chombo hicho kuingia anga ya dunia.

 

Shirika la Anga za Juu la Ulaya (ESA) lilisema mapema kwamba uwezekano mkubwa ni kwamba chombo hicho cha Tiangong-1 kingeanguka baharini.

 

Imeelezwa kuwa, chombo hicho kiliacha kufanya kazi tangu Machi 2016 japo kwa kawaida Tiangong kilifaa kusitisha shughuli yake ya kuizunguka dunia kwa utaratibu na mpangilio fulani. Tiangong ni chombo kilichokuwa na urefu wa mita 10 (futi 32) na uzani wa zaidi ya tani 8 na ni kikubwa zaidi ya vyombo vyote vilivyoundwa na binadamu ambavyo vimewahi kuanguka kutoka anga za juu.

 

 

Lengo lilikuwa kutumia vifaa vinavyokipa chombo hicho msukumo kukielekeza hadi maeneo ya mbali yasiyo na watu (Bahari ya Kusini). Lakini kabla ya hilo kufanyika, ghafla hitilafu ya mfumo wa kukidhibiti ulikikumbwa na wataalamu wa China wakashindwa kukidhibiti.

 

Mashirika 13 ya anga za juu ya mataifa mbalimbali, yakiongozwa na Shirika la Anga za Juu la Ulaya (ESA), yalifuatilia njia ya Tiangong na kujaribu kuiga tabia yake kadiri kilivyokaribia kuingia ndani ya anga ya dunia huku kikiendelea kuizunguka. Tiangong maana yake ni ‘Kasri la Mbinguni’

 

Comments are closed.