Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema kwa sasa hakuna chama chochote cha Siasa au Mtu yeyote aliye na uhitaji mkubwa wa Katiba iliyo bora na yenye manufaa kwa Watanzania kuliko CCM.
Katibu Mkuu huyo ametoa kauli hiyo leo Mei 26, 2023 wakati alipowasili wilayani Mufindi mkoani Iringa wakati akizungumza na Wanachama,wafuasi wa chama hicho pamoja na wananchi ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku saba inayolenga kuimarisha uhai wa chama kuanzia ngazi za Shina, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, pamoja na kusikiliza kero za wananchi ili zipatiwe ufumbuzi.
“Nimesikia sikia huko watu wanasema sema kuhusu katiba mpya, labda niwaambie tu kwamba CCM tunahitaji katiba iliyobora kuliko mtu yoyote yule, ndio Maana Chama cha Mapinduzi kimempa ridhaa na dhamana Mwenyekiti wake Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuanzisha mchakato wa mapitio kuhusiana na suala la katiba mpya” amesema Chongolo.
Mhe. Chongolo amewasili Mafinga, wilaya ya Mufindi mkoani Iringa tayari kuanza ziara ya siku saba akiwa ameongozana na Wajumbe wawili wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Ussi Gavu na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema.