The House of Favourite Newspapers

COMPLEX, VIVIAN WAWAPONGEZA WAKONGWE KUOA

 

MUZIKI mnene unapiga, sijui hata ni muziki gani. Macho yangu yanagongana na jumba moja kubwa ambalo lina watu wamevaa makoti marefu meusi.

Nawasalimia lakini wao hawanijibu. Najaribu kufungua mlango niingie kunaposikika muziki, wananizuia.

 

Nawaomba niingie, wananiuliza shida yangu na kunitaka niseme ninapotoka. Nawaambia sijui nitokako na hata hapo nilipo sijui ni wapi.

Wanaangaliana na kupeana ishara kwamba waniruhusu tu niingie ndani. Nazama ndani, nakutana na sura za watu wengi ambao akili yangu inanieleza kwamba walifariki miaka mingi iliyopita. Wapo maarufu na wasio maarufu lakini kila mtu yupo bize na mambo yake.

Kuna ambao wanacheza muziki, wengine wanapiga tu stori zao.

 

Wakati natafuta sehemu ya kukaa, macho yangu yanakutana uso kwa uso na mrembo ambaye alikuwa tishio kwa kurap Bongo, Vivian.

Niliposogea karibu zaidi, nagundua aliyekaa naye pembeni ni aliyekuwa mtangazaji wa Clouds FM na prodyuza maarufu Bongo, Saimon Sayi ‘Complex’.

Akili sasa inakubaliana na mazingira kwamba nimekutana na wapendanao waliofariki kwenye ajali ya gari, Vivian na Complex. Wananikaribisha kwenye meza yao na kuanza kupiga nao stori:

 

MIMI: Vivian nilipokuona hapa nimekufahamu lakini sijui kama wewe unaweza kuwa unanifahamu.

VIVIAN: Aisee hapana! Labda ujitambulishe.

MIMI: Kwa kweli huwezi kunifahamu lakini kifupi mimi ni mwanahabari na nilikufahamu wewe kupitia muziki wako miaka ya 2000 kabla hujafariki na mchumba wako.

VIVIAN: Ooh! Afadhali leo nimekutana na mwanahabari labda atanipa picha ya watu niliowaacha duniani. Hivi Hip Hop inaendeleaje sasa hivi? Kuna kina nani wanachana?

MIMI: Siku hizi wapo vijana kina Godzillah, Nikki Mbishi, Nikki wa Pili na wengine wengi.

 

VIVIAN: Ina maana wale wakongwe niliowaacha mimi kama kina Professor Jay, Sugu wameacha gemu?

MIMI: Professor Jay sasa hivi ni Mbunge wa Mikumi, Sugu naye ni Mbunge wa Mbeya Mjini lakini bahati mbaya tu amehukumiwa jela miezi mitano kutokana na kesi ya kuzungumza lugha kumfedhehesha Rais Dkt John Pombe Magufuli.

COMPLEX: (Anadakia kwa mshutuko mkubwa) Wewee! Usiniambie. Sugu yupo ndani? Tatizo nini jamani?

 

MIMI: Ni lugha tu ambazo alizitoa katika Viwanja wa Luanda Nzovwe, Mbeya ambapo kesi iliunguruma na Sugu akakutwa na hatia, akafungwa.

COMPLEX: So sad! Sugu najua harakati zake. Kama ulisema alishakuwa mbunge, angeweza kufanya makubwa kwa kipindi hicho alichofungwa.

MIMI: Ndio hivyo ila ninazo taarifa kwamba watakata rufaa, hivyo nafikiri tusikilizie.

VIVIAN: AY na FA wapo? Wameoa maana nawajua walikuwa si wa kuoa leo au kesho, vipi bado wanaruka na dunia.

 

MIMI: (Nikacheka kidogo) AY na FA wote sasa hivi wameshauaga ukapera. Wako bize tu na ndoa zao!

VIVIAN: Vizuri sana. Hayo ndio mambo tuliyokuwa tunaelekea kuyafanya mimi na mwenzangu hapa (anamshika bega Complex) lakini ndio hivyo tena hatukuweza kufikia malengo yetu huko duniani.

Complex akadakia…

 

COMPLEX: Daah umenikumbusha mbali sana, AY nakumbuka tuliwahi kufanya naye ngoma ya Raha Tu, ilikuwa bonge moja la ngoma.

MIMI: Ni kweli kabisa kaka. Ila daah, kifo chenu kiliwagusa watu wengi sana. Kapo yenu ilipendwa sana naifananisha na kapo ya sasa ya Diamond na Wema ambayo mara kadhaa imeingia kwenye kuachana na kurudiana lakini inapendwa sana.

VIVIAN: Wema na Diamond? Nahisi hao siwajui kihivyo. Watakuwa walikuja kuwa maarufu baada ya sisi kufariki.

 

MIMI: Ni kweli, yawezekana mlikuwa mnakutana nao katika mishe zao za kawaida lakini kifupi, Wema ni muigizaji mkubwa ambaye umaarufu wake ulichipukia kwenye Shindano la Miss Tanzania 2006 baada ya kuibuka kidedea.

Diamond alikuja kuwa maarufu kwenye Bongo Fleva baadaye sana baada ya Wema kushinda Miss Tanzania.

VIVIAN: Wakati sisi tunaondoka, muziki ulikuwa ndio kwanza unaanza kulipa kwa mbali, hali ikoje kwa sasa.

 

MIMI: Daah watu sasa hivi wamepiga hatua sana. Wanamiliki majumba ya kifahari, magari, miradi mbalimbali kutokana na muziki. Kifupi sasa hivi kuna mafanikio makubwa sana.

VIVIAN: Enhee! Wakilisha bado wapo? Wanaendeleaje? Langa najua tuko naye huku.

MIMI: Kundi lilishasambaratika, kila mtu anaendelea kivyake. Shaa na Witness wapo mchezoni lakini hawasikiki kiviile.

 

COMPLEX: Maprodyuza gani wanafanya vizuri kwa sasa?

Wakati nataka kumjibu, simu yangu ikaiita. Ghafla nikashtuka na kugundua kumbe mazungumzo yangu na Vivian pamoja na Complex yalikuwa ni ndoto. Naamka na kuanza kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini.

 

NA ERICK EVARIST: SAA TISA USIKU KITANDANI KWAGU

Comments are closed.