The House of Favourite Newspapers

Coutinho Mbadala wa Tatu wa Neymar

MOJA ya jambo ambalo Liverpool hawawezi kulijutia ni kumuuza kiungo wao mshambuliaji, Phillipe Coutinho, kwenda kwenye kikosi cha Barcelona cha Hispania.

Coutinho alikuwa mchezaji mahiri kwenye kikosi cha Liverpool na alikuwa akionyesha uwezo wa juu kwa kipindi chake chote alichokaa kwenye timu hiyo.

 

Lakini kwa kuwa soka ni biashara ni kichaa tu alikuwa anaweza kukataa kitita cha pauni milioni 145, zaidi ya shilingi bilioni 300, ambazo Barcelona walizitoa kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo mwenye uwezo wa juu uwanjani.

Liverpool walikataa ofa ya kwanza ya mchezaji huyo kwa kuwa haikuwa hata imefikia kitita cha pauni milioni 100, lakini baada ya fedha hizo kuongezeka hakika walikubali kuzipokea uamuzi ambao kila mmoja anauona kuwa sahihi.

 

Mchezaji huyo pamoja na kwamba anaonekana kuwa wa kawaida lakini kwa sasa ndiye mchezaji ghali zaidi duniani na haionekani wazi rekodi yake inaweza kuvunjwa kwa hivi karibuni.

Ukweli ni kwamba pamoja na Barcelona mara kwa mara kusema kuwa wanataka saini ya kiungo huyo lakini walikoleza moto zaidi baada ya staa wao Neymar kuondoka kwenye timu hiyo na kujiunga na PSG ya Ufaransa.

 

Kuondoka kwa Neymar kulivuga mambo mengi sana kwenye timu hiyo kutokana na jinsi walivyokuwa wametengeneza pacha ya wachezaji watatu, Neymar, Suarez na Lionel Messi ambao walikuwa wanaofanya mambo makubwa.

Hayakuwa matarajio ya Barcelona kuwa wangeweza kumuachia mchezaji huyo kwa kipindi kile, bali waliamini kuwa angeweza kubaki kwao kwa muda mrefu kama walivyofanya mastaa wengi wanaokwenda kwenye timu hiyo akiwemo Lionel Messi ndiyo maana ondoka yake iliwashtua na kujikuta wakifanya mambo mengi kwa mpigo bila kuangalia madhara yake.

 

Hadi sasa ambapo anakwenda Coutinho kwenye kikosi hicho cha Catolania, Barcelona wameshafanya usajili wa wachezaji watatu wa kiwango cha juu kwa ajili ya kuziba pengo la Mbrazil huyo, lakini wawili kati ya hao walishaanza kazi na kuonekana kuwa hawakidhi mahitaji ya timu hiyo inayowania ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania msimu huu.

 

Mara baada ya kuondoka kwa Neymar Barcelona walitangaza kumsajili Ousmane Dembele, kutoka kwenye kikosi cha Borrusia Dortmund ambapo walitumia kitita cha pauni milioni 97, kwa ajili ya mchezaji huyo.

Huyu alikuwa wa kwanza kabisa kwenye timu hiyo kusajiliwa baada ya kuondoka Neymar na pamoja na umri wake wa miaka 20, alitajwa kuwa anaweza kuziba pengo hilo, lakini pamoja na kwamba alikuwa anachipukia bado kwenye michezo michache aliyocheza kabla ya kuumia hakuweza kufanya jambo lolote na sasa anatarajiwa kurudi klabuni hapo mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao baada ya kukaa nje muda mrefu akiuguza majeraha.

 

Mpaka anaumia staa huyo alifanikiwa kucheza michezo mitano tu akiwa alicheza mitatu ya Ligi Kuu Hispania na hakufunga bao hata moja.

Kuumia kwake kuliendelea kufifisha matumaini yake kuwa anaweza kuziba pengo la Neymar.

Lakini wakati huohuo, Barcelona waliamua kutumia tena fedha kwa ajili ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa zamani wa Tottenham, Paulinho kutoka kwenye kikosi cha Guangzhou Evergrande.

 

Paulinho ambaye naye alitajwa kama mbadala wa Neymar alionekana kuwa kwenye presha kubwa sana mwanzoni kutokana na timu aliyotokea kujiunga na Barcelona.

Staa huyo ambaye anacheza kwenye alisajiliwa Barcelona kwa kitita cha pauni milioni 40, na mwanzoni alionekana kama mchezaji wa kawaida sana lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele kasi yake uwanjani imeonekana kukua kwa kiwango cha hali ya juu.

 

Hadi sasa ameshacheza michezo 24 na kufunga mabao saba kwenye timu hiyo ambayo inawania kwa nguvu kubwa ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania msimu huu.

Mchezaji huyo pamoja na kwamba alionekana kuwa mbadala wa Neymar alisema kuwa hataki kuona watu wanamfananisha na Mbrazil mwenzake huyo kwa kuwa wote wa malengo tofauti na kiwango tofauti uwanjani.

 

Paulinho ndiye amekuwa akicheza mbele na Messi, Suarez kuhakikisha kuwa Barcelona inapata matokeo mazuri, wakati yeye akifunga mabao saba, staa wa timu hiyo Messi ameshapachika mabao 16, kwenye michezo 18 aliyocheza kwenye Ligi Kuu ya Hispania lakini jumla akiwa amepachika mabao 20 kwenye michezo 26, aliyotumika kwenye timu hiyo.

Bado inaonekana pia Coutinho ambaye hadi anaonekana Liverpool msimu huu alikuwa amecheza michezo 20 na kufunga mabao 12, hawezi kuwa na kazi rahisi ya kuziba pengo la Neymar na atakuwa Mbrazil wa pili kucheza kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo akiwa pamoja na Paulinho lakini akiwa mchezaji wa Amerika ya Kusini wa nne kucheza kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

 

Hii ina maana kuwa asilimia kubwa ya mabao ambao yatafungwa na timu hiyo yatakuwa yakifungwa na wachezaji kutoka Amerika ya Kusini msimu huu.

Coutinho hatakutana na ugumu wa kombinesheni au kuwazoea wenzake kwa kuwa atakuwa na Paulinho ambaye wamekuwa wakicheza wote kwenye timu ya taifa ya Brazil, lakini pia atakutana na Suarez ambaye waliwahi kucheza pamoja kwenye kikosi cha Liverpool kwa mafanikio makubwa sana.

 

Jambo lingine ambalo linaweza kumfanya staa huyo akafanikiwa haraka ni kwa kuwa aina ya soka wanalocheza Liverpool kwa sasa la pasi nyingi za kasi ndiyo hilo ambalo linachezwa na Barcelona ambayo inaongoza Ligi Kuu ya Hispania.

Alichokisema kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp kuwa Mbrazil huyo alilazimisha kwenda kwenye kikosi cha Barcelona, kinazidi kuongeza kasi kuwa atafanikiwa mapema kwa kuwa atakuwa na mapenzi na timu hiyo tofauti na wale ambao wamekuwa wakienda kutafuta fedha.

 

Hii ina maana kuwa kama Coutinho naye atashindwa kuwika kwa kiwango ambacho wengi wanakitarajia basi Barcelona watakuwa wamekosa mbadala wa staa huyo ambaye kwa sasa ameshapachika mabao 19 kwenye michezo 21 aliyoichezea timu hiyo ya Ufaransa.

Comments are closed.