The House of Favourite Newspapers

DAAH! STARS NDIYO HIVYO BANA AFCON 2019, TANZANIA 2-3 KENYA

MCHEZOvwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Kenya uliochezwa jana usiku, umemalizika kwa Kenya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Katika mchezo huo wa Kundi C uliochezwa kwenye Uwanja wa June 30 uliopo jijini hapa, ni wa pili kwa timu hizo katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) inayoendelea kwa sasa hapa Misri.

 

Simon Msuva alianza kufungua milango kwa bao la dakika ya sita baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Kenya, Patrick Matasi kutokana na shuti lililopigwa na Mbwana Samatta. Bao hilo liliamsha shangwe za Watanzania na kuendelea kuishangilia kwa nguvu timu yao.

Makosa ya Aishi Manula dakika ya 39 ya kushindwa kuukoa mpira wa krosi, ulitua miguuni mwa Michael Olunga na kuisawazishia Kenya. Dakika moja baada ya kuingia kwa bao hilo, Samatta aliongeza bao la pili kwa Taifa Stars baada ya kumpiga chenga Matasi na kuuweka mpira kimiani.

 

Kipindi cha kwanza kilimalizika Taifa Stars ikiwa mbele kwa mabao 2-1. Mabadiliko kadhaa yaliyofanyika kipindi cha pili, yaliisaidia Kenya kwani dakika ya 64, Johanna Omolo aliisawazishia Kenya kwa kichwa, kabla ya Olunga kufunga bao la tatu dakika ya 81.

 

Mwamuzi wa mchezo huo, Ahmad Heeralall raia wa Mauritius, alionekana kuumudu mchezo huo licha ya kuwa na presha kubwa. Kwa matokeo hayo, Taifa Stars inaendelea kuburuza mkia wa kundi hilo ikiwa haina pointi baada ya kucheza mechi mbili na kufungwa zote.

 

Algeria inaongoza ikiwa na pointi sita, Senegal na Kenya zote zina pointi tatu. Kikosi cha Taifa Stars; Aishi Manula, Ramadhani Kessy,

Gadiel Michael, Kelvin Yondani, David Mwantika, Mudathiri Yahya/ Himid Mao, Erasto Nyoni/ Frank Domayo, Thomas Ulimwengu/ John Bocco, Simon Msuva, Mbwana Samata na Farid Mussa.

SALEH ALLY, Cairo

Comments are closed.