The House of Favourite Newspapers

DAKIKA 450 YANGA KITAELEWEKA

BAADA ya Yanga kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St Louis ya Shelisheli na kufanikiwa kufuzu hatua inayofuata, uongozi wa timu hiyo umeibuka na kusema kwa siku za hivi karibuni, ratiba ya mechi zao imebana, lakini watapambana kuhakikisha wanavuka kipindi hicho salama.

Yanga imefuzu hatua ya awali ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya juzi kutoka sare ya bao 1-1 na timu hiyo katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Linite, Shelisheli. Mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa, Yanga ilishinda bao 1-0.

 

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, walitarajiwa kurudi nchini jana Alhamisi usiku tayari kwa mchezo wao wa Kombe la FA dhidi ya Majimaji utakaopigwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika amesema kwa sasa ratiba imewabana sana kwani baada ya kumalizana na Majimaji, Jumatano ijayo watacheza mechi ya ligi kuu dhidi ya Ndanda, lakini watajipanga kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi hizo mfululizo.

 

Ikumbukwe kuwa, ndani ya takribani siku 14, Yanga itatakiwa kucheza mechi tano ambazo ni sawa na dakika 450 zikiwemo za Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kati ya hizo, nne ni za ugenini na moja wataichezea nyumbani.

 

Ratiba hiyo ya Yanga ipo hivi baada ya juzi kucheza ugenini dhidi ya St Louis; Februari 25 dhidi ya Majimaji katika Kombe la FA, Februari 28, dhidi ya Ndanda (ligi kuu), Machi 3, dhidi ya Mtibwa Sugar (ligi Kuu), hizo zote ni za ugenini, kisha itacheza nyumbani dhidi ya Township Rollers ya Botswana katika Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Machi 6 na 7.

 

“Kiukweli tunashukuru Mungu tumeweza kusonga mbele katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ukiangalia ratiba yetu kwa sasa imebana sana.

“Baada ya kumalizana na St Louis, sasa tunaelekeza nguvu zetu zote kwa Majimaji baada hapo tunaelekea kwa Ndanda, tunataka kufanya vizuri katika mechi hizi licha ya kwamba zipo karibukaribu sana,” alisema Nyika.

 

Omary Mdose | Dar es Salaam

Comments are closed.