The House of Favourite Newspapers

MONI: R.O.M.A KITU GANI BANA, NASIMAMA MWENYEWE!

UKIACHANA na ngoma kali iitwayo Mwaaah, aliyoiachia msanii kutoka Dodoma Awadhi Mtezo ‘Moni Central Zone’, aliyoshirikiana na Country Boy, gumzo kwenye mitandao ya kijamii na media mbalimbali juu yake ni kuhusu tofauti kati yake na msanii wa Hip Hop, Ibrahimu Mussa ‘R.O.M.A Mkatoliki.’

Gumzo hilo linatokana na kwamba, Moni na R.O.M.A ni watu ambao mashabiki wa muziki waliwafahamu kuwa karibu.

Waliambatana pamoja kwenye shoo, studio, kwenye mahojiano ya media na kwenye maisha ya kawaida. Zaidi hata walipopata balaa la kutekwa mwaka jana walikuwa pamoja na prodyuza wao Bin Laden.

Hata hivyo, hivi karibuni mambo yameonekana kwenda kombo. Wawili hao kila mmoja kwa nafasi yake amekuwa akizungumza maneno yanayoashiria kutokuwepo maelewano mazuri kati yao kwenye mahojiano ambapo hakuna ambaye amekuwa akiainisha ukweli wa nini hasa mzizi wa kutoelewana kwao.

Kutokana na utata huo, gazeti hili liliamua kuwatafuta wawili hao ili waweze kuukata mzizi wa fitina.

Ijumaa lilianza kumtafuta mkali wa ngoma za Sembe Dona na Usimsahau Mchizi, Moni ambaye pia ni msomi mwenye digrii ya Environmental Disaster Management kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma. Mahojiano yalikuwa hivi:

Ijumaa: Moni kwanza hongera kwa ujio wako mpya na Country Boy, tumeona mmetengeneza kundi, ni baada ya ugonvi wako na R.o.m.a nini?

Moni: Asante kwa pongezi. Lakini si kweli kwamba nimeunda kundi kwa sababu ya tofauti zangu na R.O.M.A, kuhusu watu kuungana na kushirikiana ni vitu vimeanza zamani sana. R.o.m.a na Stamina si wa kwanza, tulianza kuona huko nyuma Chegge na Temba walifanya kazi pamoja lakini hata A.Y na FA. Kwa hiyo mtu ukiona mpo sawa mnaweza kufanya lolote lile.

Ijumaa: Kwa nini huu muungano uwe sasa na si huko nyuma wakati upo karibu na R.O.M.A?

Moni: Kila kitu kina wakati wake. Halafu mimi na Country tumeanza muda tu kufanya kazi pamoja maana tulianzia kwenye shoo. Nikiandaa shoo ananipiga sapoti, akiandaa shoo pia nampa sapoti, kwa hiyo baadaye tuliona hiki kitu ni kikubwa na kinaweza kufanya kazi.

Ijumaa: Tukirudi kwenye ugomvi wenu, katika moja ya nyimbo zako umesema hata R.O.M.A akikuacha nyuma huwezi kufeli, nini ulikuwa unamaanisha?

Moni: Nilikuwa ninamaanisha kwa yeye kuamua kuniweka kando alifikiri pengine kwamba nitafeli kimuziki jambo ambalo haliwezi kutokea. Naweza kusimama mwenyewe na kufika kule ninakohitaji kufika.

 

Ijumaa: Kwani nini hasa mzizi wa tofauti zenu?

Moni: Mzizi ni kwamba mimi na R.O.M.A kuna vitu vingi tumefanya kwenye muziki. Sikatai ni kweli yeye ndiye alinipokea pale Tongwe Records mwaka 2014 nilipokwenda na kupitia yeye nimeweza kukutana na watu wengi.

Lakini hata kujifunza kwenye shoo na mambo mengine ya kimaisha. Sasa umefika wakati naona nilionekana kama kikwazo, kwa hiyo vitu vyake vingi akaanza kuvifanya peke yake na kuniacha nyuma.

Sasa mnapokuwa safarini na mtu ambaye unamuamini, ukafika sehemu labda stendi ukalala halafu ukagundua mtu wako wa karibu anataka kukuacha lazima ushituke na kumuona si mwenziyo.

 

Ijumaa: Kwa hiyo suala ni hilo tu?

Moni: Yapo mengi, kama unavyokumbuka baada ya kutekwa mimi ndipo nikawa na jina kubwa kuliko hata muziki wangu. Sasa ulikuwa ni muda ambao nilihitaji pia, naweza kusema hata na wengine tuliokuwa nao kuweka uwiano wa kazi zetu na jina tulilolipata.

Sasa ambaye angeweza kutusaidia katika hilo ni R.O.M.A ambaye tayari alikuwa na jina kubwa. Lakini ukiangalia wimbo ambao aliutoa ilikuwa ni kwa ajili ya kujizungumzia yeye, kwa manufaa yake mwenyewe na si ya wote ambao tulipata tatizo. Kwa hiyo ni kama mtu alitumia matatizo yetu kujinufaisha yeye.

 

Ijumaa: Labda kutokana na yote yaliyotokea umewahi kuzungumza kuhusu mabadiliko hayo na R.O.M.A?

Moni: Hapana. Siwezi kuzungumza naye lolote ilihali kila kitu nilishakiona. Ninaweza kusonga mbele mwenyewe kwenye muziki wangu.

Ijumaa: Kuna baadhi ya watu mpaka leo hawaamini kama ni kweli mlitekwa, hebu funguka juu ya hili.

 

Moni: Ni kweli. Hilo jambo lilitokea na wala watu wasifikirie mambo mengine. Kungekuwa na jambo lolote lile lilitokea ambalo siyo sahihi ningeweza kuliweka wazi. Siwezi kutumika kwa kitu ambacho hakina manufaa na mimi.

Ijumaa: Na kwenye muziki wako kwa sasa tutegemee nini?

Moni: Kikubwa ndiyo kama hivyo, mimi na Country Boy tumetengeneza muungano uitwao Moco. Ni ngoma baada ya ngoma, tuna mipango mingi ya kikazi na watu wategemee vitu vingi sana kutoka kwetu.

 

Hayo ndiyo mahojiano kati ya Moni na gazeti hili. Je, huo ndio ukweli kuhusu ugomvi wao? Hilo ndilo swali ambalo wengi wanaweza kuwa wanajiuliza. Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta R.O.M.A pia ili aweze kuzungumzia kwa upande wake nini hasa sababu za ugonvi wao lakini hakuweza kupatikana.

Juhudi za kumtafuta zinaendelea na akipatikana kila kitu kitaanikwa.

BONIPHACE NGUMIJE | IJUMAA

Comments are closed.