DAR ES SALAAM: Hatari! Hili ndilo neno sahihi unaloweza kusema kufuatia wiki iliyopita, mtu mmoja aliyetambulika kuwa ni daktari, kunaswa akiwa anafanya shughuli za kuendesha zahanati binafsi kimagumashi, katika eneo la Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar es Salaam, kwani hakuwa na cheti wala nyaraka zozote kutoka mamlaka zinazohusika na shughuli za kitabibu
Chanzo kilicho makini kililitonya Risasi Mchanganyiko juu ya kufanyika kwa shughuli za kitabibu kwa namna ya ujanjaujanja kwani zahanati hiyo ilikuwa ikitoa huduma kwa matatizo mbalimbali kimachalemachale.
“Sisi ni majirani hapa, lakini tumeshtushwa na utaratibu wa zahanati hii kufanya kazi ya kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa nyakati za usiku tu. Jambo hilo limetupa shaka tukaona hapa kutakuwa na kitu, ndipo tukaamua kuwapigia simu polisi ili waweze kuchunguza kuna nini,” kilisema chanzo hicho juu ya zahanati hiyo ambayo pia haina jina.
Risasi Mchanganyiko lilifika eneo hilo sambamba na polisi na kushuhudia daktari huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma, akikiri kuwa yeye ni daktari wa hospitali moja wilayani Kisarawe na kukiri kuwa anatoa huduma za matibabu pasipokuwa na kibali.
“Ni kweli jamani, najua kabisa kuwa kutoa huduma ya matibabu bila ya kuwa na leseni wala kibali chochote ni kosa, lakini nipo katika process ya kukamilisha vitu hivyo.
“Mimi ni daktari kabisa, nalijua kosa langu lakini naomba tusameheane, nitajitahidi kukamilisha taratibu za kupata leseni haraka sana,” alisema huku akiomba.
Kuhusu tuhuma za kufanya kazi usiku tu, daktari huyo alisema anafanya hivyo kwa kuwa muda mwingi wa mchana huwa anafanya kazi kwa muajiri wake, hivyo nafasi kwa kazi zake huwa ni muda huo pekee.
Hadi Risasi Mchanganyiko linaondoka eneo la tukio, daktari huyo alikuwa bado akihojiwa na askari hao kutoka kituo kimoja cha polisi wilayani Ilala.
WAANDISHI WETU, RISASI MCHANGANYIKO