The House of Favourite Newspapers

DAR DERBY… MANULA, KABWILI HAWAKULALA

Ramadhani Kabwili wa Yanga

TANZANIA nzima inawezekana usiku wa kuamkia leo Jumamosi ulikuwa mgumu kwa watu wawili tu. Tena ingekuwa inaruhusiwa kisheria pengine wangeenda kukesha sehemu kuondoa msongo wa mawazo.

Mmoja anaitwa Ramadhani Kabwili wa Yanga na mwingine ni Aishi Manula ni Simba. Achana na Deo Munishi na Klaus Kindoki hawa walikuwa wanakoroma kabisa kwani wana uhakika kwamba kikombe cha leo pale Uwanja wa Taifa kitawaepuka.

 

Wala hawakuwa na presha sana ingawa wakisikia hata kocha kaita jina, wanashtuka kwamba kuna nini tena?

Shughuli ilikuwa kwa Manula na Kabwili, hawajalala. Usiku mzima walikuwa wakiucheza mchezo huo kichwani.

Manula anafikiria kelele na mizuka ya mashabiki wa Simba na kwa mbali anamuona Mohammed Dewji na miwani yake ya bei mbaya akihamasisha mashabiki kushangilia.

 

Huku kwenye jukwaa la mzunguko anamuona Haji Manara akikata mauno na mashabiki wakipiga kelele za kutosha. Zaidi ya nusu ya uwanja ni nyekundu tupu. Akiangalia uwanjani anaona Ibrahim Ajibu, Heritier Makambo, Deus Kaseke na Feitoto wanajitahidi kumshambulia kutafuta sifa.

Kabwili yeye anawaza hii ndiyo mechi yangu ya kwanza ya watani nikiteleza hapa nimepotea kabisa.

Akiangalia mashabiki jukwaani wana mizuka ya kufa mtu na wote wana hamu mnyama apigwe kwani mitaani hawakai kutokana na kelele. Sasa kilichomnyima usingizi na kumfanya kila dakika ashtuke usingizini ni kwamba anawazuiaje?

Akiangalia mbele yake anaona Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco wote wanakuja kama nyuki wanataka kufanya yao. Ghafla anashtuka inabidi aendelee kukaa macho.

Makala haya yanakupa baadhi ya vitu vya makipa hawa ambao ndiyo watakaoanza kwenye mechi hii.

 

MANULA

Ndiye nguzo ya Simba. Kisaikolojia yuko imara sana kutokana na kipigo cha mabao 10-0 alichopata kwenye mechi mbili za AS Vita na Al Ahly pamoja na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ahly ndani ya Uwanja wa Taifa.

Hana hofu tena ya mechi kubwa, amekuwa sugu. Tatizo litaanza kama wenzie wakimuangusha Yanga wakapata

mabao ya haraka. Lakini Manula ni imara kwenye mechi kama ya leo. Kuonyesha benchi la ufundi la timu hiyo lina imani naye hadi sasa ameshacheza dakika 1359 za mechi zote 15 za Simba msimu huu.

 

Kipa huyo wa zamani wa Azam FC anafanya kazi kubwa ya kuokoa hatari zote zinazoelekezwa langoni mwake huku akishika nafasi ya kwanza kwa makipa walioruhusu mabao machache katika ligi, akifungwa matano tu.

 

Kipa huyo anayeshikilia Tuzo ya Kipa Bora msimu uliopita amekuwa akilalamikiwa na mashabiki wengi kwa kuruhusu mabao ya mbali, amewahi kufungwa kwa staili hiyo kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi za ligi dhidi ya Mwadui na African Lyon.

 

Ni mjanja wa kumsoma mpinzani wake kisha kuwapanga mabeki wake namna bora ya kumlinda ndiyo maana hadi sasa ana idadi ndogo ya mabao aliyofungwa.

KABWILI

Anajiamini sana kuliko mashabiki wanavyomdhania. Hajakumbana na mitihani mizito kama mwenzie Manula, bado anakuwa.

 

Hii ndio mechi yake ya kwanza ya watani, atadaka baada ya kipa namba moja, Beno Kakolanya kuwekwa pembeni. Mashabiki wa Yanga wanaomba asiumie kwavile hawana imani na Kindoki. Haswa kwa mechi kama hii.

Mlinda mlango huyu atakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji wa Simba wenye uchu wakiongozwa na Okwi, John Bocco na Meddie Kagere wasipate bao.

 

Kabwili licha uchanga wake ana uzoefu wa mechi ngumu kama hizi kwani aliwahi kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) akiwa timu ya vijana ya Serengeti Boys.

 

Kipa huyu ni mjanja wa kupanga vyema safu yake ya ulinzi, pia ni mwepesi wa kuokoa mashambulizi ya haraka kutokana na umbo lake dogo lakini amekuwa hodari wa kuondoa hatari langoni mwake.

Tatizo la Kabwili ni kushindwa kumaliza mechi bila ya kutofungwa ambapo rekodi zinamhukumu na hilo, ingawa wanaojua soka wanainyooshea kidole beki yake.

 

Kwenye mechi 11 alizocheza ameruhusu mabao nane, hali ambayo inazua hofu kwa mashabiki wake kama kweli ataweza kuwazuia Kagere, Bocco na Okwi wasimfunge.

Kabwili endapo akimaliza pambano hili bila ya kufungwa ataweka rekodi iliyowahi kuwekwa na kinda mwenzake Peter Manyika kwa kipindi cha nyuma kwa kucheza mechi hii bila ya kufungwa.

Comments are closed.