The House of Favourite Newspapers

Gondwe Aanika Maajabu ya ‘One Stop Jawabu’ Temeke – Video

0
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe,  amesema kuwa kampeni ya ‘One Stop Jawabu’ ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais  John Magufuli kwa wateule wake ambapo amekuwa akiwahimiza kutokaa ofisini badala yake kuwafuata watu huko waliko na kuwahudumia pamoja na kutatua changamoto zao.
Akizungumza kupitia kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio, Gondwe amesema kuwa wameziunganisha taasisi zote za umma, mashirika na taasisi binafsi ili ziwahudumie wananchi wa Temeke na Dar es Salaam katika sehemu moja kwa uharaka, ufanisi na bila kupoteza wakati.
“Hapa tunahudumia watu wanaotaka vitambulisho vya NIDA, migogoro ya ardhi na familia, NSSF, RITA, DAWASA, TRA na mengine mengi sana. Tunawahudumia vijana, wazee, akina mama na matabaka yote, tunataka tuondoe pengo kati ya watumishi wa umma na wananchi.
“Tulianza siku saba Mbagala tukaona haitoshi, tukaongeza nyingine zikawa siku 14, tukahamia Mwembeyanga, majibu yanapatikana hapahapa, mtu anaandikishwa anaondoka na cheti cha kuzaliwa hapahapa, awali tulikuwa tukipata shida, sasa tumejifunza na kuboresha,” amesema Gondwe.
Naye, Ofisa Utumishi Mkuu na Utawala wa Manispaa ya Temeke, Mrisho Mlela, amesema; “One-Stop Jawabu tumeunganisha taasisi zote za serikali, mashirika ya umma na taasisi binafsi, maelfu wananchi tumehudumia, tuna huduma za NIDA, TRA na taasisi zote mpaka watendaji wa kata, huduma zote unapata hapahapa.

“One-Stop Jawabu sehemu ya mkakati wa Mkuu wa Mkoa wa Dar kushirikiana na Manispaa ya Temeke kuwahudumia wananchi na kutatua changamoto zao, kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akisema, sisi tumewafuata wananchi na kuwawekea huduma zote hapa.

“Kwa Mkoa wa Dar, sisi ndiyo wa kwanza kufanya kampeni kama hii  ya ‘One Stop Jawabu’ huduma zote zipo, tunalo mpaka banda la wanasheria kwa ajili ya viapo, kusaidia waliodhulumiwa viwanja na malalamiko mbalimbali wanasaidiwa hapa, ” amesema Mlela.
Aidha, Mkurugenzi Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi, amesema: “Kazi yetu ni kutoa huduma kwa wananchi, juzi tulihudumia wananchi 82,000 pale Mbagala, jambo hili linawagusa sana wananchi. Kwenye bajeti ijayo tumepanga kujenga jengo moja la ghorofa saba, ambalo litakuwa na ofisi za taasisi zote pamoja.”

Leave A Reply