The House of Favourite Newspapers

DENTI APEWA KIPIGO CHA KIFO

ENZI za tabia ya utemi wa wanafunzi kwa baadhi ya Shule za Sekondari uliokuwa ukifanywa miaka ya tisini huenda unarudi, tukio la hivi karibuni katika Shule ya Sekondari ya Kwiro iliyopo Mahenge wiliyani Ulanga, Morogoro, linaonesha hivyo.

Taarifa kutoka chanzo cha habari zilisema denti huyo, Salum Mushumbuzi anayesoma kidato cha tano alipewa kipigo cha mbwa mwizi kama siyo cha kifo na watu wanaotajwa kuwa ni wanafunzi wenzake.

Kisa cha kipigo kwa mujibu wa chanzo ni hiki: “Salum alituambia kuwa wanafunzi wenzake kutoka kikundi cha skauti (Ijumaa Wikienda halijathibitisha) ndiyo waliompiga baada ya kutokea ubishani kati yao.

“Alisema kuna wanafunzi wapatao 10 walimfuata wakati anachemsha maji (haikujulikana ya nini) bwenini kwake na kumwambia hatakiwi kujifanya mjanja sana kwa sababu wao wana nguvu kuliko mwalimu mkuu,” bibi wa Salum aitwaye Fatuma Mushumbuzi aliliambia Ijumaa Wikienda akinukuu maelezo ya mjukuu wake.

HABARI KAMILI

Ilielezwa kutoka eneo la tukio kwamba, kabla ya Salum kuhamishiwa shuleni hapo alikuwa akisoma katika Shule ya Sekondari ya Kongwa mkoani Dodoma na kwamba alipofika Kwiro yapata mwezi mmoja uliopita alidaiwa na baadhi ya wenzake kuwa anajifanya mjanja (haijulikani ni aina gani ya ujanja) na hivyo kuwekewa chuki iliyozaa chokochoko na hatimaye kipigo. Agosti 5, mwaka huu, majira ya saa nane mchana ilidawa kuwa wanafunzi hao kutoka kikundi tajwa kinachosoma shuleni hapo walimfuata Salum na kuanza kumpa mikwara.

“Waliposema kwamba wao wana nguvu kuliko mwalimu mkuu, Salum akapinga, akawaambia haiwezekani wanafunzi wajilinganishe na nguvu za mwalimu. “Baada ya kusema hivyo wale wanafunzi wakamchukua na kumpeleka kwenye chumba maalum wanachotumia katika kazi zao ambako walianza kumpiga,” bibi wa Salum alinukuu tena maelezo ya mjukuu wake.

MASWALI YALIYOKOSA MAJIBU

Ijumaa Wikienda lilipojaribu kudadisi kwa nini mwanafunzi huyo wakati anapigwa kwa takriban saa 3 mfululizo kama inavyodaiwa hakupiga kelele kuomba msaada; majibu yalikuwa ni kwamba alidhibitiwa asifanye hivyo.

Ingawa kwa mujibu wa kalenda Agosti 5, ilikuwa ni Jumapili, bado tafakuri inaonesha kwamba wanafunzi kuachwa katika mazingira ya kufanya watakavyo kwa saa 3 bila kujulikana ni hatari kwa usalama wao.

TUREJEE ENEO LA TUKIO

Kwa mujibu wa Salum katika maelezo yake kwa ndugu zake aliwatuhumu wanafunzi wanzake kumtembezea kipigo kikali sehemu mbalimbali za mwili kwa saa 3, hadi alipopoteza fahamu.

Alieleza kwamba baada ya wanafunzi hao kutambua kuwa unyama walioufanya ulikuwa umemsogeza mwenzao katika mlango wa kuingia kifoni walitaharuki na kuanza kushughulika kumrejeshea fahamu. “Walipoona kapoteza fahamu ndipo walipokwenda kuteka maji na kuanza kumwagia mwilini hadi aliporejewa na fahamu,” bibi wa Salum alisema.

BAADAYE IKAWAJE

Ilidaiwa kuwa, baada ya mwanafunzi huyo kurudiwa na fahamu aliwekwa kiti moto tena na wenzake hao huku akionywa kwamba anapaswa kuwa mpole na kamwe asithubutu kutoa siri ya kipigo alichopewa. “Walimwambia mwalimu akimuuliza amwambie kuwa alidondoka, asiseme kuwa kapigwa, akifanya hivyo atakiona cha mtema kuni,” bibi aliliambia Ijumaa Wikienda.

TAARIFA YAJULIKANA SHULENI

Aidha, baada ya tukio kukamilika na mtendewa kuonywa, wanafunzi wake wanaodaiwa kufanya unyama huo walimjulisha mwalimu aliyekuwa shuleni hapo (jina halikupatikana) kuhusu hali ya Salum. “Mwalimu alimuuliza Salum kafanya nini? Salum akasema, ameanguka kama alivyoonywa na waliompa kipigo kwa sababu walikuwepo,” bibi alieleza haya kwa sababu Ijumaa Wikienda lilishindwa kuzungumza na Salum kutokana na hali yake kuwa mbaya.

MWALIMU ADADISI ZAIDI

Baada ya mwalimu huyo kutoridhishwa na mazingira yaliyokuwepo na maelezo yaliyotolewa, aliamua kuwatoa wanafunzi wake wanaotuhumiwa kumtesa na kubaki na Salum ambapo alimuuliza kwa kina. Baada ya kuona yuko katika mikono salama ya mwalimu wake ndipo mwanafuzni huyo alipomwambia ukweli kwamba kapigwa na wenzake na kwamba alikuwa anajisikia vibaya.

HATUA ZA KUMTIBU ZAANZA

Kufuatia taarifa za kipigo kuwa wazi mwalimu huyo aliwasiliana na bibi wa Salum na kumweleza kilichotokea na hatua za kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, Mahenge, zilichukuliwa.

Hata hivyo, alipofikishwa hospitalini hapo wauguzi walishauri kwamba mwanafunzi huyo apelekwe kwenye Hospitali ya St. Francis ambayo iko Mahenge kwa uchunguzi zaidi. St. Francis nako hawakumudu kumtibu Salum, wakashauri kwamba apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako Ijumaa Wikienda lilitaarifiwa juu ya uwepo wa tukio hilo na kuanza kulifuatilia.

Ripoti za kitabibu baada ya kuchukuliwa kipimo cha kuchunguza mwenendo wa mwili maarufu kwa jina la MRI ilikuwa bado haijatoka ingawa hali ya mgonjwa kwa mujibu wa ndugu wanaomuugunza ni mbaya.

“Tupo tunasubiri vipimo, lakini mgonjwa ndiyo kama unavyomuona hali yake mbaya, sasa hivi anatapika damu,” bibi wa Salum mbaye ndiye anamlea na kumuuguza mwanafunzi huyo aliliambia Ijumaa Wikienda.

MWALIMU MKUU ATAFUTWA

Gazeti hili badaa ya kusikia madai hayo kutoka kwa bibi wa mwanafunzi huyo lilimtafuta mwalimu mkuu wa shule hiyo (jina halikupatikana) kwa njia ya simu ambapo alipoulizwa kuhusiana na kipigo cha mwanafunzi huyo aliomba:

“Mimi najua kuna jambo natakiwa kuzungumza kwa mwanafunzi huyo, lakini kwa sababu dini yangu ya Sabato hainiruhusu kufanya kazi siku hii (Jumamosi) mpaka jioni saa 12, ndiyo naweza kuzungumza chochote,” alisema mwalimu huyo.

Mwalimu huyo alipotafutwa saa aliyotaja hakupatikana hewani na kwamba juhudi za kumpata zinaendelea kufanywa. Naye Kamanda wa Mkoa wa Morogoro, ACP Wilbrod Mutafungwa alipotafutwa simu yake iliita, haikupokelewa.

Hata hivyo, habari kutoka vyanzo vya Polisi zilisema kwamba wanafunzi watatu wanaotuhumiwa kumjeruhi Salum kwa kipigo walikamatwa na kuachiwa kwa dhamana licha ya kwamba hali ya mgonjwa ni mbaya.

STORI: Imelda Mtema, DAR 

Comments are closed.