The House of Favourite Newspapers

Deus Kaseke Awatuliza Yanga

 

Kiungo mpya Yanga, Deus Kaseke.

BAADA ya kuifungia Yanga bao kwenye mechi yake ya kwanza tangu arejeshwe Jangwani, kiungo mpya, Deus Kaseke amewaambia mashabiki watulie hali itakuwa sawa kwenye Ligi Kuu Bara kwani mastaa wengi watacheza.

 

Kaseke alifunga kwenye mechi ya Shirikisho dhidi ya Gormahia ambayo Yanga walilala mabao 3-2 na kujiondoa rasmi kwenye mbio za robofainali ya michuano hiyo huku wakiwapa Wakenya hao tiketi ya bwerere.

 

Mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alicheza Singida United, alisema usajili ambao Yanga imeufanya anaamini timu hiyo itafanya vizuri na kuwasaulisha mashabiki hao machungu ya kufungwa kimataifa.

 

Lakini pia akawahakikishia kuwa kwa upande wake atakuwa akipambana vilivyo uwanjani ili kuhakikisha anarudisha furaha hiyo iliyopotea kwa mashabiki hao wa Yanga lakini pia kulinda heshima ya timu hiyo.

 

“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuanza vizuri katika timu yangu mpya ambayo nimejiunga nayo kwa mara nyingine tena na safari hii nikitokea Singida United,”alisema mchezaji huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu wa Shule za Msingi.

 

“Kitendo cha kushindwa kuwaibuka na ushindi dhidi ya Gor Mahia, kimeniumiza sana kwani hayakuwa matarajio yangu, lakini nichukue nafasi hii kuwaambia wapenzi na mashabiki watu kuwa wasikate tamaa, mambo mazuri yanakuja,”aliongeza mchezaji huyo wa zamani wa Mbeya City.

 

Kaseke ambaye anavaa jezi namba 27 ndani ya Yanga ameongeza kuwa; “Usajili ambao umefanyika ni mzuri, tuna kikosi kizuri kwa hiyo wasivunjike moyo naamini tutafanya vizuri.”

Comments are closed.