The House of Favourite Newspapers

DHANA YA UCHAWI KATIKA MAPENZI-2

0

NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa kabisa, nakukaribisha kwa moyo mkunjufu katika ukurasa huu. Wiki iliyopita tulianza kuzungumzia mada hii kama inavyojieleza hapo juu, leo ningependa tuendelee kuanzia pale tulipoishia.

Nilikuuliza msomaji wangu, je, unaamini kuna kitu kinachoitwa limbwata katika mapenzi? Bila shaka kila mmoja atakuwa na majibu yake kwa sababu ujumbe mfupi ambao umekuwa ukiingia kwenye simu yangu, unaonesha kwamba kila mmoja ana uelewa na mawazo tofauti kuhusu suala hili.

Si malengo yangu kuipinga imani yako au uelewa wako juu ya suala hili, bali ninachotaka ujifunze, ni kwamba matendo yako ni uchawi tosha katika mapenzi. Unaweza ukawa unalalamika kwamba mumeo au mpenzi wako amekuacha kwa sababu kuna mtu amemroga na kumbadilisha akili, au unaweza kuwa unadhani jirani yako au shoga yako fulani anapendwa sana na mumewe, mpaka kufikia hatua ya kumuoshea vyombo au kumfulia nguo, kwa sababu tu amemuendea kwa mganga.

Narudia tena, uchawi, iwe ni kumfanya mke au mume wako akusahau na kulowea kwa mtu mwingine, au kumfanya akugande kama mmezaliwa tumbo moja unao wewe mwenyewe, kwa lugha nyepesi, wewe ndiyo mganga na mchawi wa uhusianao wako wa kimapenzi. Yapo matendo ambayo ukiyafanya, hata kama mpenzi wako alikuwa akikupenda vipi, atakuchoka, atakukinai na hatapenda kuendelea kuishi na wewe, hata kama ni mzuri kiasi gani au una fedha nyingi kiasi gani.

Vitu kama maudhi ya kujirudia, leo mwenzi wako anakwambia sipendi ufanye jambo fulani halafu siku mbili au tatu mbele unafanya vilevile, ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kuharibu kabisa uhusiano wako wa kimapenzi. Kukosa uaminifu, yaani simu yako wewe imejaa namba za michepuko, kutwa nzima uko bize mara sijui na WhatsApp, mara Instagram, mara Facebook kote huko unawasiliana na michepuko yako,

ukitoka nyumbani unaweza hata kudanganya kwamba ndugu yako anaumwa hoi mahututi kumbe unaenda nyumba za wageni kuchepuka, ni uchawi mwingine mbaya sana. Hata kama alikuwa anakupenda kwa kiasi gani, hawezi kuendelea kukupenda tena. Dharau ni sababu nyingine.

Kila mwenzi wako anachokwambia, hata kama ni kizuri lazima mbishane, umuoneshe dharau na kupandishana hasira, nani anapenda aina hiyo ya maisha? Zipo dosari nyingine ndogondogo, kama kutozingatia usafi, kutojua namna ya kumfurahisha mwenzi wako muwapo faragha, kutowajali ndugu au watu wake wa karibu pia zinachangia sana kumfanya mtu aliyekuwa anakupenda sana, akupe kisogo na kugeukia kwa wengine. Haya yote niliyoyataja hapa, ni uchawi mbaya ambao hata kama mtu alikuwa anakupenda kiasi gani, hawezi kuendelea kuwa na wewe, atakuchoka tu.

Ukiwa na sifa hizo zote mbaya nilizozitaja, hata uende kwa mganga gani kuroga ili mumeo au mkeo akupende, ni kazi bure kwa sababu adui wa mapenzi yako ni wewe mwenyewe. Lakini sasa, hayo yote niliyoyataja, ukiyafanya kwa upande wake wa pili, ni limbwata tosha kwa mwenzi wako.

Hebu jaribu kuanzia leo, mpende mwenzi wako, muoneshe uaminifu wa dhati kabisa, mheshimu, msikilize, mfanyie mambo yanayom-furahisha, kuwa karibu naye, onesha kuzijali hisia zake na mambo mengine yote mazuri unayoyajua! Utashangaa jinsi atakavyoanza kukupenda na kukuganda mpaka kila mtu aamini kwamba umemuendea kwa mganga. Mapenzi ni sanaa, ukiiwezea utayafaidi maisha lakini ukienda ndivyo sivyo, wewe ndiyo adui wa mapenzi yako. Ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

MASKINI MAIMARTHA JESSE! Ameamua Kupima UKIMWI! Kasemwa Sana, Majibu Je?

Leave A Reply