The House of Favourite Newspapers

Mambo ya Kufuata ili Kumsahau Mpenzi wa Zamani

0

Dollarphotoclub_85545845-copy-820x450

Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu upo freshi kabisa! Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu jamvini, wiki iliyopita tulianza kujadiliana kuhusu mada hii kama inavyojieleza.

Tulipata nafasi ya kusikia ushuhuda wa dada yetu ambaye licha ya kuachana na mpenzi wake mwaka 2007 na kukutana na wanaume wengine kadhaa, ameshindwa kumsahau na matokeo yake, kila mwanaume anayekuwa naye, hadumu katika uhusiano kwa sababu ya kumfikiria mpenzi wake wa mwanzo.
Tulianza pia kuangalia njia nzuri za kukabiliana na hali hiyo ambapo kwa kuanzia, nilianza kwa kueleza kwamba jambo muhimu unalotakiwa kulifanya mwanzo ni kukubaliana na ukweli kwamba ulimpoteza mtu uliyekuwa unampenda ndiyo maana unateseka.

Japokuwa kukubaliana na ukweli huo kunamaanisha kwamba utakuwa unajuta, haimaanishi kwamba wewe ni dhaifu au ni mkosefu sana bali inadhihirisha jinsi ulivyo mkweli kwa moyo wako.

Unaweza kuwadanganya watu wote kwamba fulani sikumpenda, alikuwa na tabia mbaya, ukamkandia unavyoweza lakini kama moyo wako unazungumza lugha tofauti, inakuwa sawa na kujipiga mtama wewe mwenyewe.

Umeshakutana na watu wa aina tofauti na kuanzisha nao uhusiano lakini bado unaendelea kumkumbuka, unafikiri ni nini kama siyo kwamba ulikuwa unampenda? Ukubali ukweli kwanza.
Baada ya kukubaliana na ukweli, usikilize pia moyo wako. Unajua wakati mwingine, unapomkumbuka mtu haina maana kwamba ni lazima mrudiane japokuwa kama kila mmoja bado yupo huru, mnaweza kukaa chini na kujaribu kuangalia mliteleza wapi na kama bado mnayo nafasi ya kurekebisha makosa yenu.

Nimewahi kueleza siku za nyuma kwamba wengi huwa wanaona kama ni dhambi kubwa kurudiana na wenzi walioachana nao, hasa kwa kuhofia kwamba jamii itawaelewaje? Usiwe mtumwa wa watu wengine, usikilize moyo wako! Kama mnaweza kukaa chini na kumaliza tofauti zenu, si jambo la ajabu kurudiana.

Lakini kama tayari mmoja au wote mlishaingia kwenye uhusiano ‘serious’, kwa maana kwamba tayari wewe au mwenzi wako ameshaingia kwenye ndoa, au yupo kwenye hatua za uchumba, si busara kuendelea kung’ang’aniza kurudiana! Kubali hali halisi na songa mbele, hakuwa riziki yako ndiyo maana ametulia kwa mtu mwingine. Huu ndiyo ukweli mchungu ambao huwa unawaumiza wengi.
Kwamba alimpenda fulani, wakashindwa kuelewana na kuachana, matokeo yake mwenzake akampata mtu ambaye wamekubaliana kusonga mbele pamoja na kweli wakaanzisha uhusiano ‘serious’, kwa sababu ameshindwa kumsahau anataka kulazimisha kwamba warudiane! Hii si sawa.

Kama tayari mwenzako alishapiga hatua kwenda mbele, tuliza nafsi yako huenda na wewe utapata mtu sahihi wa kuanzisha naye familia.

Japokuwa ni vigumu kukubaliana na ukweli, huna namna. Anza kufuta kumbukumbu zake maishani mwako, kama kuna zawadi au vitu mlivyowahi kupeana kipindi cha mapenzi yenu, vigawe au vitupe kwa sababu ukiendelea kuviona utazidi kujiumiza moyo wako.

Pia hilo liwe funzo kwako kwamba itakapotokea ukampata tena mtu unayempenda, naye akakupenda kwa dhati, mkigombana ni kutafuta suluhu siyo kuachana. usiachane na mtu kama bado moyo wako unampenda, hakuna kosa ambalo halisameheki hata lingekuwa kubwa kiasi gani.

“WIZARA YA UJENZI, TAMISEMI MALIZENI MGOGORO WENU, WANANCHI WANAHITAJI MWENDOKASI”- CPA MAKALLA


 

Leave A Reply