The House of Favourite Newspapers

Diamond, Kiba Walivyotibuana!

Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ Akisalimiana na Ali Saleh Kiba

KUFUATIA tukio la dharura la kifo cha aliyekuwa video queen mkali Bongo, Agness Gerald Waya ‘Masogange’ aliyeagwa jana kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni na kusababisha Jiji la Dar kuzizima kwa vilio, waandishi wetu, Richard Bukos, Neema Adrian, Gladness Malya na Imelda Mtema walikuwa na shughuli maalum ya kumpasha Mkuu wao kilichokuwa kikiendelea katika tukio hilo.

 

Pamoja na mambo mengine, lakini tukio kubwa ni la wasanii mahasimu, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Saleh Kiba kusalimiana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi na kutibua shughuli nzima ya kuaga kutokana na kuibua gumzo.

 

SAA 5:12 ASUBUHI

Mkuu akiwa ofisini anaanza kuwatwangia vijana wake ili kuhakikisha kama wamejipanga vizuri kwa ajili ya kuchukua matukio mbalimbali ya msiba huo ambapo anaanza na Neema Adrian.

Neema: Mkuu ninakupata, niambie…

Makao Makuu: Uko wapi na nini kinaendelea hapo?

Neema: Mkuu mimi niko hapa nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tunausubiri mwili wa Masogange.

Makao Makuu: Vipi, kuna mastaa gani hapo?

Neema: Mkuu ukweli mastaa ni wengi, ninamuona Dude, Mike wa Thea, Idriss, Uwoya na wengine kibao ila Dogo Janja sijamuona.

Makao Makuu: Mimi sijakuuliza habari za Dogo Janja, ngoja nikuache nimtafute Bukos.

SAA 5:40 ASUBUHI

MAMA LORAA ANASWA NA MAJI YA KUPUNGUZA UCHUNGU

Bukos: Mkuu wangu ninakupata.

Makao Makuu: Haya niambie uko wapi?

Bukos: Mkuu niko hapa Leaders Club, tunasubiri mwili wa Masogange, lakini pembeni yangu niko na Mama Loraa, namuona macho yamekuwa mekundu ile mbaya, nimeongea naye ananiambia amelia kwa siku tatu mfululizo ndiyo maana macho yake yako hivyo. Pia ninamuona mkononi ameshika chupa ya ‘tumaji twa’ baridi’ anafyonza taratibu, nilipomuuliza sababu ya kupiga maji muda huu anasema anapunguza machungu.

Makao Makuu: Sawa Bukos, ngoja nimsikilize Gladnes Mallya naye aniambie tukio lililopo mbele yake.

SAA 6:21 MCHANA

MWILI WA MASOGANGE WAINGIA LEADERS

Gladness: Naam Mkuu, shikamooo.

Makao Makuu: Marhaba binti, haya nieleze uko upande gani?

Gladness: Mkuu niko hapa viwanja vya Leaders na hivi tunavyoongea mwili wa Masogange ndiyo unaingia. Ninawaona wasanii wakiongozwa na Steve Nyerere wanaushusha kwenye gari na kuupeleka sehemu iliyoandaliwa.

Makao Makuu: Vipi umenasa tukio lolote hapo?

 

Gladness: Matukio ni mengi sana Mkuu kuna sharobaro mmoja anajifanya kulia sana akiona kamera iko mbele yake, nilipomhoji anajifanya eti marehemu alikuwa mtu wake.

Makao Makuu: Kwa hiyo umechukua vizuri maelezo yake?

Gladness: Mkuu nilivyomsikiliza vizuri nikamuona kama anahitaji kiki tu hana lolote, tena nimesikia wala hawajuani maana baada ya kumuhoji anajifanya eti ametoa singo yake nayo anataka tuiandike.

Makao Makuu: Hiyo singo alimshirikisha marehemu?

Gladness: Hapana Mkuu hajamshirikisha, tena mtu wa karibu wa marehemu nilipomuuliza akaniambia wala walikuwa hawajuani huyo na sharobaro anatafuta kiki tu.

Makao Makuu: Dah! Watu wa mjini nao kwa kiki, haya piga kazi ngoja mimi nimcheki tena Bukos.

Saa 7:21. Mchana

 

DIAMOND, KIBA WATIBUA

Bukos: Naam Mkuu wangu ninakupata.

Makao Makuu: Haya niambie nini kinaendelea hapo?

Bukos: Mkuu kwa muda mrefu tulikuwa na bwana harusi, Ali Kiba, naye amechomoka kwenye fungate amekuja hapa kujumuika na wasanii wengine. Pia ninamuona Diamond naye anakuja. Naona ameandaliwa mahali pa kukaa ni jirani kabisa na Ali Kiba.

Makao Makuu: Hebu angalia kama watasalimiana?

Bukos: Mkuu hivi tunavyoongea namuona Diamond ndiyo anasalimia waliokaa meza kuu ambapo aliowakuta wote wamesimama kiheshima wakati wakisalimiana, sasa amefika kwa Ali Kiba naye anampa mkono, ninamuona Ali Kiba naye anainua mkono kumsalimia, lakini akiwa amekaa tofauti na wenzake.

Makao Makuu: Mbona nimesikia kama shangwe fulani hivi vipi tena?

Bukos: Baada ya tukio la wawili hawa kusalimiana ndiyo mashabiki wameibua shangwe za kuwashangilia na kutibua taratibu za kuaga hapa.

Makao Makuu: Wabongo nao, wameshaona hapo ndiyo pakuwaonea laivu bila kiingilio!

Makao Makuu: Sawa Bukos, ngoja nimcheki tena Neema Adrian.

 

 

 

Saa 7:56. Mchana

 

MWILI WAAGWA

Neema: Naam Mkuu.

Makao Makuu: Haya niambie kuna tukio gani mbele yako?

Neema: Ninaona sasa waombolezaji ndiyo wanaanza kuaga mwili, nawaona Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia, Diamond, Dokta Cheni, Chegge wanapita mbele ya jeneza lenye mwili wa marehemu.

Makao Makuu: Enhee mbona nasikia vilio vimezidi nini tena?

Neema: Hayaaa duh!

Makao Makuu: Nini tena?

Neema: Rammy Gallis ameanguka na na kuungana na mastaa wengine kibao wanaozimia, naye amezimia, naona anakimbizwa kwenye gari la wagonjwa, namuona na mzazi mwenzake marehemu Sabri Shaban naye anaaga, ameishiwa nguvu kabisa waombolezaji wengine wanamsaidia kutembea.

Makao Makuu: Sawa Neema endeleeni na kazi.

KUZIKWA LEO

Mwili wa Masogange ulisafirishwa jana jioni kwenda kuzikwa kijijini kwao, Utengula wilayani Mbalizi jijini Mbeya huku Rais John Magufuli akituma salamu za rambirambi kupitia Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James. Rest In Peace Masogange!

Stori: Waandishi Wetu, Dar

Comments are closed.