The House of Favourite Newspapers

Msiba: Dickson Kagembe Afariki Hospitalini Muhimbili Leo

0
Mfanyakazi wa Global Publishers, Huruma Bujiku (kushoto) akiwa na Dickson Kagembe enzi za uhai wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric James Shigongo, kwa kushirikiana na familia ya marehemu Boniphace Shija Kagembe, wanaungana na ndugu, marafiki na Watanzania wote waliomfahamu Dickson Kagembe ambaye amefariki asubuhi ya leo kunako saa tatu wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Muhimbili.

Shigongo alikutana na marehemu Dickson kwa mara ya kwanza katika Hospitali ya Ocean Road alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya kansa ya damu.  Walikutana siku Shigongo alikuwa amekwenda kumwangalia marehemu shemeji yake aliyekuwa pia amelazwa katika hospitali hiyo kwa matibabu ya kansa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric James Shigongo (aliyesimama) akiwa na Dickson Kagembe (kulia) enzi za uhai wake na Wakonta Kapunda.

Pamoja na kwamba walikuwa hawajuani, lakini siku hiyo ndiyo iliyoumba undugu na ukaribu kati ya watu hao wawili ambapo Shigongo na familia yake walijumuika na familia ya marehemu na wauguzi katika kufuatilia matibabu ya Dickson.

Kama ilivyo ada yake, Shigongo alivitumia vyombo vyake vya habari kuwajulisha Watanzania wengine kuhusu tatizo la kiafya la  Dickson na wagonjwa wengine ili kila wapatapo fursa yoyote waweze kuwakumbuka kwa kuwasaidia kwa aina yoyote.

Miongoni mwa fursa ambazo Global Publishers ilitoa kwa marehemu Dickson ni pamoja na kumsaidia kuandika na kuchapisha kitabu cha maisha yake tangu utotoni hadi alipokuwa amefikia.  Kitabu hicho kilikuwa katika hatua za mwisho kumalizika kabla ya Mwenyezi Mungu kumuita katika enzi yake.

Maisha ya Dickson aliyezaliwa Agosti 23, 1982,  yamefikia mwisho leo wakati akiendelea kupata matibabu  huku akitegemea kurejea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kumalizia masomo yake ya Sheria.

Mkurugenzi Mtendaji na wafanyakazi wote wa Global Publishers wanaungana na familia ya marehemu Dickson katika msiba huu na kumwomba Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema pepeni na awape nguvu za matumaini ndugu na familia yake aliyoiacha.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa.  Jina lake lihimidiwe.  Amina!

Na Walusanga Ndaki/ GPL

HII NI VIDEO IKIONESHA SIKU DICKSON ALIPOFANYA ZIARA YA KUMTEMBELEA WAKONTA NYUMBANI KWAO MBEZI, WAKIWA NA SHIGONGO. WAKONTA NAYE NI MLEMAVU WA MIGUU NA MIKONO, ANAANDIKA KWA KUTUMIA ULIMI!

Leave A Reply