The House of Favourite Newspapers

Diwani Mstaafu Mtarawanje Ashinda Kesi ya Rushwa

0

ALIYEWAHI kuwa Diwani wa Kata ya Kijichi Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Elias Mtarawanje ameshinda kesi iliyochukua takriban miaka miwili iliyokuwa inamkabili ya tuhuma za kupokea rushwa kwa nyakati tofauti na hivyo kuachiwa huru.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es salaam Wakili Dkt Aloys Rugazia ambaye amesimamia shauri la Mtarawanje ambalo limekuwa linasikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke amesema kesi hiyo No. 266 ya mwaka 2020 ilikuwa ni tuhuma na hivyo Mahakama imewabaini kuwa hawana hatia.

 

Dkt. Rugazia amesema hiyo imemaanisha kuwa kiwango cha fedha kinachosadikiwa mteja wake kuchukua hakikua na uthibitisho wowote wa kuwa pesa hizo ambazo zimepelekwa mahakamani kama ushahidi hivyo mahakama ikaamua kutupilia mbali shauri la upande wa Mwendesha Mashtaka na kumuachia huru Diwani mstaafu Mtarawanje.

 

‘Tunashukuru sana Taasisi ya Kupambana na Rushwa PCCB kwani tumeweza kupata dhamana bila usumbufu wowote na baada ya kufikishwa mahakamani ushahidi wa pande zote ulichukuliwa na wateja wetu wawili Bwana Elias Mtarawanje na Constantin Moris walibainika kwamba hawana kosa’amesema Wakili Dkt Rugazia.

 

Aidha, Wakili Dkt Rugazia amesema umuhimu wa Kesi hiyo imetokana na Mtarawanje kuwa diwani kijana kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hivyo tuhuma dhidi yake zimeleta msisimko kwa jamii kutaka kufahamu hitimisho lake.

 

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Temeke Mohammed Abdalah amepongeza hatua hiyo na kusema kuwa haki imetendeka kwani Mtarawanje alikuwa kiongozi shupavu ambaye amefanya kazi yake kwa uaminifu bila ya uoga.

 

‘Kama chama kina taratibu zake na miongozo yake lakini ni jambo zuri kwa Mwanachama mwenzetu aliyekuwa Diwani kushinda hivyo ninayofuraha ya kuona kijana mwenzangu amepata haki yake na ukweli umedhihiri’ amesema Mohammed.

 

Amesema kuwa kwenye siasa kuna changamoto nyingi pindi vijana wanavyofanya mambo mazuri wengine wanaingiwa na wivu kwani Mtarawanje alipambana sana katika ujenzi wa Mradi wa barabara zilizokuwa chini ya DMPD.

 

Ikumbukwe kuwa Diwani huyo mstaafu wa Kata ya Kijichi alifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yake na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU,Mwanakombo Rajabu mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Catherine Madili.

Leave A Reply