The House of Favourite Newspapers

Dkt. Abbasi: Vyombo vya Habari Viwape Nafasi Wahitimu wa Habari

0
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa, Dkt. Hassan Abbasi.

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi ameviagiza vyombo vyote vya habari nchini kutoa nafasi kwa wahitimu wa taaluma ya habari kufanya  mazozezi  kwa vitendo katika vyombo hivyo  ili waweze kujendeleza  katika taaluma hiyo.

 

Ametoa agizo hilo Desemba 18, 2020 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa Astashada na Stashada ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) ambapo amesema kuwa lengo la kutoa nafasi kwa wahitimu hao ni kuwajengea uwezo wa kufanya vizuri katika taaluma hiyo.

“Tutahakikisha kwenye kuhuisha leseni ya chombo cha habari pamoja na mambo mengine, sifa nyingine lazima uonyeshe uthibitisho wa kuchukua wanafunzi wangapi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo katika chombo chako,” alisema.

 

Huku akisistiza kuwa hapa nchini kuna  idadi ya magazeti na majarida zaidi ya 230, redio 185 zinazotangaza katika ngazi ya mikoa, kitaifa na kimataifa, pamoja na runinga  takriban 40 ambazo zimesajiliwa nchini na kupewa leseni,  hivyo ni lazima kila chombo kutoa nafasi kwa wanachuo wa taaluma  hiyo kufanya mazoezi kwa vitendo  ili taaluma hiyo izalishe wataalamu wengi zaidi.

Vilevile amewaeleza wahitimu hao baadhi ya siri za mafanikio ikiwemo kuweka malengo, malengo makubwa  na kuwa na malengo yanayotekelezeka.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Johson Swoa, amewapongeza wanafunzi hao kwa kuhitimu na kutunukiwa vyeti ambapo ameeleza kuwa chuo hicho kimefanikiwa kuzalisha wataalamu wengi ambao wanafanya vizuri katika tasnia ya habari ikiwemo kutangaza, kuandika na kuhariri.

Leave A Reply