The House of Favourite Newspapers

Dokta Aanika Chanzo cha Vifo vya Mapema!

KUNA watu hawana taarifa sahihi kuhusiana na ulaji unaofaa na mtindo sahihi wa maisha unaozingatia afya bora ambao husababisha kuwa na uwezekano wa kuwa na umri mrefu wa kuishi.

 

Watu wanaishi ilimradi siku zinakwenda bila kuzingatia kanuni za afya. Lakini siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la wagonjwa wengi wa magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni hatari na husababisha vifo vya mapema.

Bahati mbaya, watu wanaoishi mijini wametajwa kuwa katika hatari zaidi ya kukumbwa na magonjwa hayo. Ripoti hii maalum ya Gazeti la Ijumaa Wikienda, iliyoanza wiki iliyopita imekusanya yote hayo; kuhusu mtindo bora wa maisha na ulaji unaofaa, ambao ni rafiki kwa afya ya binadamu.

 

Tuliona magonjwa yaliyotajwa zaidi kusababisha majanga kwa nchi mbalimbali ulimwenguni, zikiwemo zenye uchumi wa kati na nchi maskini (Tanzania ikiwemo), kuwa ni kisukari, moyo, saratani, shinikizo la damu na magonjwa yanayohusiana na upumuaji.

Wiki iliyopita tulianza kwa kuona maelezo ya mtaalam wa tiba lishe kutoka Mumbai, Maharashtra nchini India, Santosh Sawant ambaye alitolea ufafanuzi kuhusiana na vyakula vinavyopendekezwa, ratiba sahihi ya mlo, mazoezi na mwisho alianza kuelezea kuhusiana na tendo la ndoa.

 

TENDO LA NDOA

“Lakini hata tendo la ndoa ni sehemu ya mazoezi. Pia ni sehemu ya mahitaji muhimu ya mwili na akili. Ukiweza, fanya mapenzi hata kila siku, hakuna shida. Inategemea na uhitaji wako na utayari wa mwenzako,” anaeleza Sawant na kuongeza:

“Tendo la ndoa lina faida nyingi. Licha ya mazoezi, linahusisha starehe ya akili. Mtu anayeshiriki tendo la ndoa, anakuwa mwenye furaha, akili yake inafanya kazi haraka na anakuwa mwepesi wa kufikiri na kutoa maamuzi.

 

“Lakini lazima tendo lenyewe liwe salama. Umjue unayelala naye, pia uwe tayari kwa tendo hilo. Lakini nasisitiza kwamba, inatakiwa lifanywe kwa staili tofauti ili kuleta ile maana ya msisimko, burudani na mazoezi kwa wakati mmoja.”

Sawant anasema, tendo la ndoa likifanywa kwa watu walioridhiana na kuwa na utayari, wanajiweka katika nafasi kubwa ya kuishi maisha marefu, yenye afya na furaha.

 

DAWA NGUVU ZA KIUME

Kwa mujibu wa maelezo ya Sawant kuhusu umuhimu wa tendo la ndoa, mwandishi wetu alitaka kujua iwapo matumizi ya dawa za nguvu za kiume kwa ajili ya kuongeza ufanisi ni sahihi ambapo alifafanua;

“Mwili unaozingatia ulaji ulio sahihi, hautahitaji dawa ya kusapoti. Kimsingi dawa siyo nzuri, lakini wapo wanaotumia kwa ushauri wa daktari.

“Mimi nasisitiza, dawa nzuri zaidi duniani ni chakula. Sishauri kabisa watu kutumia dawa za nguvu za kiume au za kike, hapana. Mpangilio mzuri wa lishe unatosha.”

 

FAIDA ZA MLO SAHIHI

Kuhusu mlo sahihi, Sawant anasema zipo faida nyingi, lakini kubwa zaidi ni kujiepusha na maradhi nyemelezi.

“Mtu anayekula vizuri kwa kufuata kanuni, hawezi kuugua hovyo. Chakula ni dawa. Chakula bora hutukinga na maradhi. Anza leo kufuata kanuni za ulaji bora, mazoezi na mtindo mzuri wa maisha, hutaugua na utashangaa sana,” anasema Sawant.

 

MUDA GANI UNATOSHA KULALA?

Wataalam wengi wanaeleza kuwa binadamu anapaswa kulala angalau si chini ya saa saba, lakini wengi wanasisitiza saa nane ndiyo hasa zinazofaa kwa afya bora ya binadamu, Sawant anasemaje?

“Kulala ni kupumzisha mwili na akili. Muda wako wa kupumzika unatokana na namna ulivyouchosha mwili wako na akili. Haiwezekani mtu ambaye hana kazi ngumu, akalala saa nane au tisa, akasema anapumzisha mwili, haipo hivyo.

 

“Kimsingi wastani mzuri wa kulala ni saa tano au sita. Kwa mfano mtu anayefanya mazoezi sana, atahitaji kulala muda mrefu zaidi. Kwa hiyo mtu wa mazoezi sana, ni sahihi kulala saa nane, lakini kwa mtu ambaye hana mikiki sana, saa tano mpaka sita zinatosha, uamke ukafanye kazi na afya yako itakuwa sawa.

“Utakumbuka hata kwenye mazoezi nilisema, inategemea na namna mtu anavyokula. Kama unajua kabisa umeingiza mafuta mengi mwilini, lazima ufanye mazoezi makali zaidi ili uweze kuyayeyusha, kadhalika na kulala ni hivyo hivyo.”

 

NIDHAMU YA MAISHA

Sawant anasema, mambo yote hayo yatawezekana kwa mtu ambaye atakuwa na nidhamu na maisha yake.

“Ukijua kuwa ulaji wako unaweza kukusababishia maradhi hatari na baadaye kifo, utakubali kufuata mfumo ulio sahihi.

 

“Ukitambua wazi kuwa, mtindo wako wa maisha siyo rafiki kwa afya yako, basi lazima utakubali kubadilika. Na bahati mbaya hakuna njia nyingine zaidi ya kubadilika, ila lazima ujipe malengo na ukubali kuwa na nidhamu,” anasema Sawant na kuongeza;

“Ugumu huwa wakati wa kuanza. Ukishaanza utajikuta unaendelea kila siku na baadaye unakuwa utaratibu wa maisha yako. Usile kila kitu, kula kinachohitajika na mwili wako.

“Usiende kila mahali, nenda sehemu iliyo salama kwako. Usile kila wakati bali ule wakati unaotakiwa tu. Fanya yaliyo sahihi kwa ajili ya afya ya mwili wako na uhai wako.”

 

UNYWAJI WA POMBE

Sawant anasema unywaji wa pombe unaofaa ni mzuri kwa afya na kwamba husaidia kufanya mmeng’enyo, lakini baadhi ya watu hujisahau na kugeuza pombe kama chakula hali inayosababisha uharibifu wa afya na kuwa chanzo cha maradhi.

“Pombe ikitumiwa kwa kiasi haina tatizo. Ni burudani nzuri. Huchangamsha damu na husaidia mmeng’enyo wa chakula, lakini iwe kwa kiasi.

 

“Tatizo utakuta mtu anakunywa kupita kiasi, halafu asubuhi anaamkia kula nyama au supu, anaongeza matatizo. Kwa kawaida pombe ina protini nyingi, ukichanganya na nyama ndiyo kabisa, mwisho wa siku mtu anajiweka kwenye hatari ya kupata shinikizo la damu.

“Kama unakunywa pombe, kichwani mwako lazima ujue kuwa unazalisha mafuta mengi mwilini. Kwa sababu hiyo sasa, lazima kila siku asubuhi ufanye mazoezi ili kuondoa hayo mafuta yaliyozidi mwilini ambayo hayana kazi,” anasisitiza Sawant.

 

MWILI NI MASHINE

Uko ugumu wa kufikia hayo aliyoshauri Sawant, kwa kulijua hilo mwenyewe anasema; “Jipe tabu ya wiki moja mpaka mbili. Najua ni ngumu, lakini ukishaanza, mwili utazoea na utapokea ratiba hiyo mpya.

“Itakuwa sehemu ya hitaji lako la siku. Mwili wa binadamu ni sawa na mashine; labda nifananishe na kompyuta. Ukianza kuamka saa 11 Alfajiri kwa wiki mbili za mwanzo kwa alamu, siku zinazofuata hutahitaji alamu, tayari mwili utakuwa unakupa taarifa.

“Utataarifiwa kila hatua; muda wa kula, muda wa kulala, muda wa kuamka, muda wa mazoezi nk. Miili yetu ni mashine.”

 

DONDOO MUHIMU ZA AFYA

Wakati tunamalizia upande huu wa mtaalam wa tiba lishe, zingatia dondoo hizi muhimu hapa chini kwa ajili ya kujenga afya yako bora na kujiweka kwenye nafasi ya kuwa na umri mrefu.

Jitahidi sana katika mlo wako kupunguza kabisa nyama na uzidishe mbogamboga kwa wingi. Kuna faida kubwa sana zinazopatikana kwenye mbogamboga.

 

Punguza kabisa matumizi ya sukari, ukiweza acha kutumia sukari. Penda zaidi kutumia matunda ya msimu kwa wingi, yatakupa sukari sahihi inayohitajika mwilini. Jitahidi kutumia asali badala ya sukari. Ikiwa mazingira uliyopo ni lazima sana kutumia sukari iwe kwa kiasi kidogo sana.

 

Punguza kutumia usafiri, jitahidi kutembea. Kwa mfano unafanya kazi maeneo ya Posta, Dar, mchana unaweza kwenda kula mgahawani kwa miguu tu, ukaacha gari lako ofisini. Usijizoeshe kutumia gari siku zote za wiki. Tafuta angalau siku moja, uliache gari lako utembee kwa safari fupi.

Jitahidi kuwa mtu wa furaha. Jichanganye na watu wanaokupa furaha zaidi kuliko watu wanaokutibua na kukuhuzunisha. Usijiweke mpweke na usikae sana peke yako.

 

Pumzika vya kutosha kama wataalam wanavyoshauri. Jipe muda mzuri na sahihi wa kupumzika kwa ajili ya afya yako.

Kwa hakika, ukiyafuata hayo utaishi maisha yenye furaha, utajiweka mbali na magojwa na utakuwa kwenye nafasi kubwa ya kuishi maisha marefu zaidi.

 

Usikose sehemu ya mwisho ya ripoti hii maalum wiki ijayo ambapo tutaangalia maelezo ya madaktari wa binadamu wa ndani na nje ya nchi kuhusiana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na uhusiano na mtindo wa maisha.

Makala: Joseph Shaluwa, Ijumaa Wikienda.

Comments are closed.