The House of Favourite Newspapers

DTB TANZANIA YAENDESHA WARSHA KWA WATEJA DODOMA

Mgeni ramsi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akitoa hotuba fupi katika hafla ndogo ya chakula na vinywaji kwa wateja na wadau wa DTB Tanzania iliyofanyika katika hoteli ya Nashera mjini Dodoma hivi karibuni.

 

Benki ya DTB-Tanzania, leo imeendesha warsha ya siku moja kwa wateja wake wenye biashara ndogondogo na kati waliopo katika mji wa Dodoma na vitongoji vyake. Warsha hii ya siku moja iliyofanyika katika hoteli ya Nashera, iliandaliwa kwa ushirikiano na kampuni ya PKF Associates; ambao ni wataalam wa utunzaji mahesabu, kodi na uendeshaji wa biashara.

Meneja Maendeleo na Biashara wa DTB Tanzania, Magusa Nhende akizungumza na wateja wenye biashara ndogondogo na wadau wa benki hiyo kutoka mji wa Dodoma na vitongoji vyake katika semina ya siku moja iliyojadili kwa kina kanuni za uendeshaji wa biashara na udhibiti wa mapato, sharia ya kazi na mwenendo wa Uchumi Tanzania. Warsha hiyo iliandaliwa na DTB Tanzania kwa kushirikiana na PKF Associates jijini Dodoma hivi karibuni.

 

Maswali yaliyojadiliwa kwa kinaga ubaga ni kanuni za uendeshaji wa biashara na udhibiti wa mapato, sharia ya kazi na mwenendo wa Uchumi Tanzani na dunia kwa ujumla.

 

Waendesha warsha kutoka PKF Associates walichanganua kwa undani marekebisho mbalimbali na miongozo katika ulipaji wa kodi na mambo mbali mbali yanayohusisha sheria za kazi nchini. Wageni waalikwa (wateja wa Benki ya Diamond Trsut) walipata kujua bidhaa na huduma mbalimbali zitolewazo na benki, zikiwemo dhamana za benki, mikopo mbalimbali, mikopo ya bima, huduma za kutuma na kupokea fedha ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akiwasili kwa ajili ya hafla ndogo ya chakula na vinywaji kwa wateja na wadau wa DTB Tanzania iliyofanyika katika hoteli ya Nashera mjini Dodoma hivi karibuni. Pamoja nae kutoka kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu ya TTCL Waziri Kindamba, Mwakilishi wa hoteli hiyo Phoebe Geoffrey na Meneja Maendeleo na Biashara wa DTB Tanzania Magusa Nhende.

Akiongea na waandishi wa habari katika warsha hiyo, Mkurugenzi mtendaji na Meneja mkuu wa DTB Tanzania, Ndugu Viju Cherian, alisema “Tumeweka lengo la kufanya warsha kama hii katika miji yote tuliyo na matawi  ili kuzungumza na wafanyabiashara wadogo na wa kati mikakati mizuri ya biashara bora: kuweka rekodi za biashara, kanuni za biashara na upangiliaji wa matumizi ya mikopo ya kibenki, ambazo ni vitu muhimu katika uendeshaji wa biashara”.

Mtendaji wa Kampuni ya PKF Associates, Muntansir Gulamhussein akizungumza na wateja wenye biashara ndogondogo na wadau wa DTB Tanzania kutoka mji wa Dodoma na vitongoji vyake katika semina ya siku moja iliyojadili kwa kina kanuni za uendeshaji wa biashara na udhibiti wa mapato, sharia ya kazi na mwenendo wa Uchumi Tanzania. Warsha hiyo iliandaliwa na DTB Tanzania kwa kushirikiana na PKF Associates jijini Dodoma hivi karibuni. Kulia ni Meneja wa Maendeleo na Biashara wa DTB Tanzania, Magusa Nhende.

 

Wageni waalikwa katika warsha hiyo walipata nafasi ya kuzungumza na viongozi kutoka DTB-Tanzania na kubadilishana ujuzi wa kazi pamoja na ubunifu wa biashara katika sekta mbalimbali kwa mfano Biashara, Viwanda, Usafirishaji, Ujenzi. “Warsha hii ni sehemu muhimu sana katika kukuza uchumi na sekta ya biashara ndogondogo na kati na inahitaji kupewa kipaumbele.Tumetoa mikopo zaidi ya Shs. bilioni 285 kwa biashara ndogondogo na kati. Hii ni asilimia 40% ya mikopo yote iliyotolewa na benki yetu”. Ndugu Viju aliongeza.

DTB Tanzania kwa sasa ina matawi 28 nchini, 14 kati ya hayo yakiwa jijini Dar es Salaam kama ifuatavyo (Mtaa wa Jamaat, Masaki, Morocco, Magomeni, Mbezi, Mbagala, Nyerere, Kariakoo, Tawi la Nelson Mandela, Upanga lililo barabara ya Umoja wa Mataifa na Tawi la CBD lililo kwenye makutano ya barabara za Samora na Mirambo) jingine ni Tawi Mbezi Chini lililo Kata ya Kawe na tawi jipya kabisa la Mlimani City.

Mkuu wa kitengo cha TEHAMA wa DTB Tanzania, Bi. Stella Masha (mwenye mtandio wa pinki) akimkaribisha Mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dk. Harrison Mwakyembe kuhudhuria hafla ndogo ya chakula na vinywaji kwa wateja na wadau wa DTB Tanzania iliyofanyika katika hoteli ya Nashera mjini Dodoma hivi karibuni. Kutoka kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu ya TTCL Waziri Kindamba na Katibu wa Waziri Andrew Magombana.

Matawi mengine yakiwemo matawi mawili kwa miji ya Mwanza na Arusha na tawi moja katika miji ya Dodoma, Kahama, Mbeya, Morogoro, Moshi, Mtwara, Mwanza, Tabora, Tanga na visiwa vya Zanzibar.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akisalimiana na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba wakati wa hafla ndogo ya chakula na vinywaji kwa wateja na wadau wa DTB Tanzania iliyofanyika katika hoteli ya Nashera mjini Dodoma hivi karibuni.

DTB Tanzania ni kampuni tanzu ya makampuni ya DTB (DTB Group) yanayoendesha shughuli za kibiashara katika ukanda wa Africa Mashariki nchini Kenya, Uganda na Burundi. DTB Tanzania pia ni kampuni tanzu ya Mfuko wa Aga Khan wa Maendeleo ya Kiuchumi (The Aga Khan Fund for Economic Development – AKFED) ambayo ni tawi la Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (Aga Khan Development Network -AKDN)

Comments are closed.