The House of Favourite Newspapers

Duni Haji Mwenyekiti Mpya ACT, Kumrithi Maalim Seif

0

 

Mkutano Mkuu Taifa katika kikao chake kilichofanyika jana tarehe 29 Januari 2022 katika ukumbi wa Mlimani City Dar es salaam, umejaza nafasi za Mwenyekiti wa Chama Taifa, Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa (Zanzibar) na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ambazo zilikuwa wazi kwa sababu mbalimbali.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mkutano Mkuu wa Chama umemchagua Ndugu Juma Duni Haji kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo Cha Maalim Seif Sharif Hamad.

Aidha, Mkutano Mkuu umemchagua Ndugu Othman Masoud Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa (Zanzibar).

Kwa upande wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama, Mkutano Mkuu Taifa umemchagua Ndugu Msafiri Mtemelwa.

Imetolewa na:

Janeth Joel Rithe,
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma,
ACT Wazalendo.
30 Januari, 2022.


Duni ni nani?

Duni alizaliwa mwaka 1950 huko Zanzibar, alisoma shule ya msingi Mkwajuni kati ya 1959 – 1965, baadaye akajiunga na sekondari ya juu ya Lumumba kati ya mwaka 1966 – 1969.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa masomo ya shahada ya kwanza ya elimu ya Sayansi kuanzia mwaka 1972 – 1975. Baadaye mwaka 1994 – 1995, alisoma shahada ya uzamili katika rasilimali watu katika Chuo Kikuu cha Manchester huko Uingereza.

 

Mwanasiasa huyo amefanya kazi katika Serikali ya Zanzibar katika nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na katibu mtendaji wa Tume ya Mipango (1981 -1982), katibu mkuu – viwanda (1980 -1981), ofisa mipango – elimu (1976 -1979) na mwalimu wa sekondari (1975 – 1979).

 

Katika medani za siasa, Duni pia ameshika nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo, naibu kiongozi wa chama, Waziri wa Afya katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, naibu katibu mkuu wa Cuf, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Cuf.

Leave A Reply