The House of Favourite Newspapers

Emmanuel Amunike: Tutaifunga Algeria

KOCHA wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, amesema bado ana matumaini ya kikosi chake kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo dhidi ya Algeria.

Stars leo itacheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa Afrika ‘Afcon’ dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Al- Salam nchini Misri.

Stars ambayo ipo mkiani mwa Kundi C, ilianza vibaya michuano hiyo kwa kufungwa na Senegal mabao 2-0, kisha Alhamisi iliyopita ikapoteza tena mbele ya Kenya kwa mabao 3-2 na leo watamaliza kwa kucheza na Algeria.

Akizungumza na Waandishi wa Habari nchini hapa, Amunike alisema kuwa, licha ya kuwa Algeria ina kikosi kizuri lakini bado ana matumaini makubwa na vijana wake kuwa watafanya vizuri katika mchezo huo wa mwisho wa Kundi C.

“Tumecheza na Algeria mara kadhaa, nakumbuka mchezo wa Dar es Salaam tuliocheza tukafungwa mabao 2-0 na baadaye tukaja kucheza nao tukatoka sare ya 2-2, nakumbuka pia walikuja wakatufunga mabao 7-0, lakini hiyo yote ni historia,” alisema Amunike na kuongeza:

“Kwa sasa hivi tunachokitazama ni namna gani tutaweza kusawazisha makosa yetu yaliyotokea katika michezo miwili iliyopita na kufanya maamuzi sahihi tunapokuwa na mpira.

“Jumatatu (leo) ni ukurasa mwingine na ni safari nyingine kwa Tanzania na Algeria. Hauwezi kutabiri nani atakuwa mshindi, kwa hiyo tutaingia uwanjani kupambana na kusaka pointi tatu.”
MWANDISHI WETU, Cairo

Comments are closed.