The House of Favourite Newspapers

Eric James Shigongo: Dimbwi la Damu-01

ERIC JAMES SHIGONGO: DIMBWI LA DAMU-01

Ilikuwa ni siku ya jumapili mjini Arusha, mawingu yalitanda kila mahali angani na manyunyu yalikuwepo kiasi cha kuwafanya watu wavae makoti, ilikuwa si kawaida ya mji wa Arusha katika kipindi hicho cha mwaka kuwa na baridi.

Jioni ya siku hiyo kulikuwa na kila aina ya furaha nyumbani kwa Martin na mkewe Hoyce! Shangwe na vigelegele vilitawala, watoto wengi kutoka nyumba za jirani walialikwa! Ilikuwa ni sikukuu ya kuzaliwa kwa watoto wao wawili mapacha, Victoria au Vicky na Nicholaus au Nicky kama walivyoitwa na wazazi wao!

Walikuwa watoto wawili mapacha waliofanana kupita kiasi kama ungekuta wote wamevalishwa magauni usingesita kusema walikuwa ni watoto wa kike! Walikuwa ni watoto wazuri na wenye afya njema! Walimvutia karibu kila mtu aliyewaona.
Martin, alikuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite aliyemiliki kampuni kubwa ya uchimbaji wa madini iliyoitwa Tanzamine Limited ambayo makao yake makuu yalikuwa mjini Arusha. Ilikuwa ni kampuni kubwa kuliko zote Afrika ya Mashariki, katika umri wake umri wa miaka 26 Martin alitisha kwa utajiri wake! Alihesabika kuwa kijana tajiri kuliko wote nchini Tanzania na hata Afrika ya Mashariki.

Ilikuwa si rahisi kukadiria kiasi cha fedha alichopata kutokana na biashara yake, aliuza madini yake katika nchi ya Bangladesh, Singapore, Ufaransa na Marekani, alikuwa ni mtu mwenye kazi nyingi kupita kiasi na alisafiri katika nchi 26 duniani kila mwezi akikaa na familia yake kwa muda wa siku nne tu katika mwezi.
Yeye na mke wake Hoyce walioana miaka mitatu kabla na walikutana kwa mara ya kwanza ndani ya ndege, Martin akisafiri kutoka Uingereza kibiashara na Hoyce akitoka masomoni Uingereza, walijikuta wamekaa kiti kimoja ndani ya ndege hiyo ya shirika la ndege la Uingereza, British Airways! Kabla ya kupanda ndege Martin alimwona Hoyce akikumbatiana na mvulana wa kizungu.

Baada ya kukutana moyo wa kila mmoja wao ulikwenda mbio na damu iliwatembea kwa kasi ya ajabu, pamoja na hali hiyo hakuna aliyetaka kumuonyesha mwenzake waziwazi hisia zilizokuwemo moyoni mwake, kila mmoja alijitahidi kuficha hisia zake lakini jambo hilo halikuwezekana kwa Martin kwani walipofika Muscat, Martin alilazimika kueleza ukweli wake.
“Yule mwanaume wa kizungu niliyekuona ukiongea nae uwanja wa ndege ni nani?”

“Ni boyfriend wangu!”
“Aisee! Anaitwa nani?”
“Anaitwa Richard Ford!”
“Ford? Ni mtoto wa yule tajiri au?”
“Hapana ni mjukuu wake!”
“Inaonekana unampenda au siyo?”
“Sana na tuna mpango wa kufunga ndoa!”
“Inamaana utarudi tena Uingereza?”

“Hapana ila yeye atakuja Tanzania mwezi Novemba na tutafunga ndoa nyumbani!” alisema msichana huyo bila kujua ni kwa kiasi gani aliuumiza moyo wa Martin! Katika maisha yake Martin alishaona wasichana wengi wazuri lakini hawakuwa kama msichana aliyekaa nae kiti kimoja ndani ya ndege hiyo, lilikuwa si jambo la ajabu kumfananisha na Malaika aliowaona katika michoro ya hadithi za Biblia.

“Unajidanganya! Utakuwa wangu tu utake usitake, huyo mzungu wako utaachana nae ili mradi nimekupenda!” alijisemea Martin moyoni mwake huku akimwangalia msichana huyo kupita kona ya kushoto ya jicho lake!
Kwa uwezo aliokuwa nao kifedha Martin alikuwa na uhakika wa kumteka tena msichana huyo na kumfanya wake! Hiyo kwake haikuwa kazi ngumu.

Martin alizaliwa Agosti 12,1969 hivyo nyota yake ilikuwa ni Simba, watu wa nyota hii inaaminika wana uwezo mkubwa wa kushawishi na ni wapendaji wazuri, wakimpenda mwanamke humpenda kikweli kweli na mwanamke huyo hujisikia Malkia, lakini kasoro yao ni wivu! Wana wivu kupindukia, wengi wanaume ambao hujinyonga au kuua sababu ya mapenzi ni waliozaliwa kati ya Julai 21 hadi Agosti 21.

Sifa zote za watu wenye nyota ya Simba alikuwa nazo Martin! Alikuwa si mtu wa kumwacha akiongea na mtu aliyegoma kufanya kitu fulani kwa hata dakika kumi asibadili msimamo wake! Sifa hiyo pamoja na pesa nyingi alizokuwa nazo tena katika umri mdogo zilimpa Martin kiburi cha kumchukua msichana yoyote yule aliyemtaka.
“Huyu nikimwingia kwa mkwara wa pesa sitampata, ni lazima nijifanye sina kitu lakini baadaye mambo yatakuwa sawa!”Aliwaza Martin.

“Ulikuja London kufanya nini?”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Nilikuja kwa matembezi na hivi sasa narudi nyumbani!”
“Unafanya kazi gani Tanzania?”
“Ah! Ah! Sina kazi ila dada yangu anaishi hapa London na aliniita ili anitafutie kibarua lakini imeshindikana na ameamua kunirudisha nyumbani!” Martin alificha ukweli.
Mara nyingi alipowaambia wasichana ukweli juu ya utajiri aliokuwa nao hata wasiompenda walijifanya kumpenda ili wawe naye na kutumia utajiri wake.
“Pole sana.”

“Ahsante wewe je ulikuwa ukifanya nini London?” Martin aliuliza.
“Mimi nilikuwa nachukua Shahada ya Pili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Oxford na sasa narudi nyumbani kwetu Tanzania!”
“Hongera! Kwa hiyo umemaliza masomo yako?”
‘Ndiyo!” aliitikia msichana huyo huku akitabasamu, ni tabasamu hilo ndilo lililozidi kuyapeleka kasi mapigo yake ya moyo wa Martin alishindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kinataka kumtokea katika maisha yake, lilikuwa ni penzi lililokuwa likija kwa kasi ya ajabu.

Hoyce alikuwa ni msichana mrefu, mwembamba na mwenye ngozi nyororo ya maji ya kunde, nywele zake zilikatwa na kuwa fupi, hali iliyomfanya aonekane kuwa na muonekano wa Kiafrika haswa.
“Unafanana sana na mwanamitindo Alek Wek.”
“Ndiyo na watu wengi sana husema hivyo lakini si kweli kwa sababu Alek ni mweusi zaidi halafu hana mwanya kama nilionao mimi!”

“Una mwanya?” Martin aliuliza kwa mshangao.
Hakuna kitu kilichomchanganya akili Martin ndani ya mwanamke kama nafasi iliyokuwepo kati ya meno mawili ya mbele! Wanaume wengi duniani walivutiwa na maumbile lakini kwa Martin ilikuwa tofauti kwani kila alipoona mwanya wa mwanamke alihisi umeme ukipita katikati ya mgongo wake.
Alipenda sana wanawake wenye mwanya kiasi cha kushindwa kutofautisha kati ya mwanamke mwenye mwanya na mwenye pengo, rafiki yake wa mwisho kimapenzi, Lightness waliyeachana nae baada ya kumfuma akifanya mapenzi na rafiki yake mpendwa hakuwa na mwanya hilo lilimfanya Martin alazimike kumpeleka kwa daktari bingwa wa meno na kuchonga mwanya wa bandia.

Taarifa kuwa msichana huyo alikuwa na mwanya zilizidi kumchanganya akili Martin, alitamani sana kumwambia akenue lakini aliona taabu kwa sababu hakumzoea, alijitahidi kumchekesha ili akenue na kuonyesha mwanya wake lakini msichana huyo alicheka kizungu bila kufungua mdomo! Roho ya Martin ilizidi kuumia.
“Ulisema unatiwa nini vile?”
“Naitwa Hoyce!”
“Aha! Na yule boyfriend wako anaitwa nani?”
”Richard!”
“Kwa hiyo siku hiyo itakuwa Richard to Hoyce au siyo?”
“Aaaa sanaa! Nitakupa kadi uhudhurie harusi yetu kama utaweza!” Aliongea Hoyce akionyesha furaha ya ajabu.
“Utamwacha tu!” aliwaza Martin kichwani mwake.

Je, nini kitaendelea?
Je, Martin aliweza kumpata Hoyce?
Huu ni mwanzo wa hadithi hii ambayo niliwahi kuitoa magazetini zamani.
Kama hukuisoma, hii ni nafasi yako kuifuatilia.
Unaweza kushare kwa ajili ya marafiki zako.

NILIPIGWA NA MGAMBO NIKAPOTEZA MTAJI WANGU, MAKONDA NISAIDIE MAISHA MAGUMU

Comments are closed.