The House of Favourite Newspapers

Eymael: Sarpong Anatua Yanga SC

0

RASMI mshambuliaji wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda, ambaye hivi sasa yupo huru anatua kuichezea Yanga katika kuelekea msimu ujao.Mshambuliaji huyo raia wa Ghana, hivi karibuni mkataba wake ulivunjwa na Rayon kwa kile kilichoelezwa kuongoza mgomo wa wachezaji wakidai malipo ya mshahara wa mwezi Machi, mwaka huu.

 

Staa huyo ni kati ya wachezaji waliopo kwenye mipango ya kusajiliwa na Yanga msimu ujao, katika kuimarisha safu yao ya ushambuliaji akiwemo na Heritier Makambo anayekipiga Horoya AC ya nchini Guinea.

 

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, mshambuliaji huyo ana sifa zote ambazo anazozitaka yeye, hivyo ana nafasi kubwa ya kutua kujiunga na Yanga katika msimu ujao.

 

Eymael aliitaja moja ya sifa hizo ni ujasiri aliokuwa nao wa kupambana bila ya kuwaogopa mabeki watukutu na watemi wa timu pinzani, jambo ambalo linamfanya aamini kuwa ni mtu sahihi kwenye timu hiyo.

 

Mbelgiji huyo aliitaja sifa ya pili kuwa ni mshambuliaji mwenye nguvu na kasi ya wakati akiwa anaukokota mpira kwenda kwenye goli la wapinzani kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji wake Ditram Nchimbi ‘Duma’.

 

Aliitaja sifa nyingine ya tatu, ni uwezo wake wa kufunga mabao kwa kutumia kichwa na miguu ndani na nje ya 18, akitumia miguu yote kupiga mashuti, hivyo anaamini ujio wake utaiimarisha safu hiyo ya ushambuliaji inayoongozwa na David Molinga, Yikpe Gnamien, Tariq Seif na Nchimbi.

 

“Sarpong yupo kwenye mipango yangu ya usajili katika msimu ujao, ninaamini viongozi hawatashindwana naye kwani ni mchezaji huru hivi sasa na uzuri tayari nimeanza mazungumzo na meneja wake.

 

“Na kama mazungumzo yakienda vizuri, basi atakuja Yanga kwani ni kati ya washambuliaji wenye sifa zote ambazo mimi ninazihitaji awe nazo mshambuliaji.

 

“Nimekuwa nikimfuatilia kwa karibu, hivyo ninamjua vizuri sina hofu ya uwezo wake, ninafanya mawasiliano na meneja wake kila kitu kinakwenda vizuri,” alisema Eymael.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply