FAHAMU TATIZO LA UVIMBE WA TEZI ZA SHINGO

UGONJWA huu ni uvimbe unaotokea shingoni hauchagui umri na hufahamika kwa kitalaamu kama cervical/neck lympadenopathy. 

 

Tatizo la kuvimba tezi mara nyingi huwapata watoto japokuwa hata watu wazima huweza kukumbwa hasa kama wamepata magonjwa ya kuambukiza kama tutakavyoona mbele. Uvimbe huu unapozidi sentimita moja,tezi hizi hugawanywa katika makundi matatu; tezi moja au fungu moja, yaani tezi zilizovimba sehemu moja, tezi zilizosambaa (generalized) sehemu mbalimbali na tezi zitokanazo na ngozi ya shingo (dermatopathic).

 

Pia tezi hizi hugawanywa kulingana na muda kama vile tezi za muda mfupi tangu kutokea (acute).Hizi hutokea ndani ya wiki mbili, tezi za muda wa kati (subacute) zilizo ndani ya wiki mbili hadi sita na tezi za muda mrefu (chronic) yaani zaidi ya wiki sita.

MAKUNDI YA TEZI YA UGONJWA

Makundi matatu makubwa ya magonjwa husababisha tatizo hili na ndiyo dalili mojawapo ya kuwepo kwa magonjwa hayo katika mwili. Kundi la kwanza ni magonjwa ya kuambukiza (infections), kwa mfano maambukizi mdomoni, puani, masikioni, kwenye njia ya chakula au koromeo.

 

KIFUA KIKUU (TB)

Kwa kawaida maambukizi husababisha matezi kuvimba kwa watoto zaidi kuliko kwa watu wazima. Ugonjwa mkubwa katika kundi hili ni wa kifua kikuu (TB) ya matezi, hili halichagui umri wala jinsia. Wapo ambao huvimba tezi za shingo na wakienda kupimwa hugundulika kuwa wana ugonjwa wa kifua kikuu, hivyo wanatibiwa tatizo hilo na lile la kuvimba tezi.

 

KINGA ZA MWILI

Kundi la pili ni kinga za mwili kushambulia sehemu ya mwili wake (auto-immune diseases. Kinga hizo zikishambulia mwili, tezi za shingo huvimba sana na  kumsababishia maumivu makali mgonjwa.

 

UGONJWA WA SARATANI

Kundi la tatu ni saratani. Mgonjwa anaweza kupata tatizo hili akiwa na saratani na anaweza kuhangaika sana kujua sababu za kuvimba kwa tesi zake. Tatizo hili litagundulika kama atakwenda kumuona daktari na akafanyiwa vipimo kama mtaalamu huyo wa afya attakavyoona inafaa. Saratani ya damu kwa mfano au ya tezi yenyewe au ya ngozi au ya viungo vilivyopo shingoni au kichwani huleta kuvimba kwa tezi.

 

Ifahamike pia kwamba saratani kutoka sehemu nyingine ya mwili kwa mfano tumboni au kifuani huweza kutembea na kuja kujitokeza katika tezi za shingo na kusababisha kuvimba. Hilo likitokea maana yake ni kiashiria kwamba tayari saratani imesambaa mwilini, hali ambayo ni mbaya sana kwa mgonjwa.

UKIMWI, MAFUA, TONSILIS

Magonjwa mengine yanayosababisha kuvimba kwa tezi ni Ukimwi, mafua (flu), kuvimba kwa koo kwa sababu mbalimbali ya maambukizi, vidonda kooni, tonsilis nk.

 

TIBA NA USHAURI

Ni muhimu kwa mgonjwa kwenda kwa daktari au hospitali kuweza kupata matibabu bila kupuuzia, hasa kwa matezi ya muda mrefu yasiyokwisha, matezi yanayoongezeka ukubwa kwa kasi na yale yasiyoambatana na maumivu kwa kupitia vipimo ni rahisi kujua chanzo cha tatizo na mgonjwa kuanza matibabu bila kuchelewa.

Hivyo tiba itatolewa baada ya matokeo ya uchunguzi wa kimaabara ambapo itagundulika sababu za tezi zako kuvimba.
Toa comment