The House of Favourite Newspapers

FAIZA HASIRA HASARA, JIFUNZE KUCHUNGA NA KUHIFADHI ULIMI WAKO!

0

 

TABIA ya mwanamitindo maarufu hapa Bongo, Faiza Ally, ambaye ni mama wa watoto wawili, Sasha na Lil Juniour, haijanifurahisha hata kidogo na kwa kuwa nina uwezo na nafasi ya kukemea, nimeona sina budi japo kukupa ushauri wa bure tu, kuufanyia kazi ni hiari yako.

Faiza, kwa nini unakubali kuufaidisha umma kwa kuyaanika mambo ya chumbani hadharani?, Umerogwa au ni kiki, ulimbukeni au ugumu wa maisha?. Unataka sifa mitandaoni, hujui unachokifanya, umeona hiyo ndiyo njia sahihi ya kudai haki yako, au ndiyo hizo unazoziita hasira?

Sitaki kujua matatizo yenu wewe na mzazi mwenziyo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, ambaye ni Mbunge wa Mbeya, hayo ni ya kwenu na mnatakiwa myamalize nyie wenyewe bila kudhalilishana. Kilichonishangaza ni njia ambayo unaitumia kudai haki yako, ambayo siyo sahihi kabisa na uache mara moja.

Kama Sugu hatoi huduma kwa mtoto wenu, zipo mamlaka husika kwa ajili ya kushughulikia mambo kama hayo. Kuanika migogoro yenu mitandaoni kunakusaidia nini, zaidi ya kujidhalilisha na kumdhalilisha baba mtoto wako, ambaye hata hii dunia ibadilike rangi haitabadilisha ukweli wa kwamba yeye ni baba mtoto wako.

Halafu mbona hueleweki? Juzi tu umesema Sugu akitaka mtoto mwingine utampatia, leo tena ujumbe wa matusi, mara unamuombea afe, ghafla awe maskini, hayo yote ya nini, yaani kweli unatamani Sasha abaki bila baba?

Inawezekana ni kweli una haki kwa madai yako, lakini kwa njia unayotumia hakuna atakayekuonea huruma wala kuamini kweli una haki, badala yake unaonekana mjinga kwa kushindwa tu kuhifadhi ulimi wako, na kutumia busara ambazo hazihitaji hata shahada kuwa nazo.

Sifa kuu ya mwanamke ni uvumilivu, stara ya mavazi, ulimi na kila kitu, pia wanawake ni walimu wakubwa tunaotegemea wawape elimu watoto wao ambayo haina cheti wala ada, lakini elimu hiyo huwezi kuipata popote isipokuwa kwa mama tu.

Inapotokea muda wa kuwa mama umefika na ukawa mama kweli halafu huna sifa nilizozitaja hapo juu basi umekula hasara kubwa sana, na tegemea kizazi chako

pia kama siyo nusra ya Mungu basi kitafuata nyayo zako.

Inawezekana hujui madhara ya ulichokiandika, ila kwa faida yako na watoto wako wanaokua wakiona mienendo yako, unatakiwa kubadilika, usitukane hovyo kwa kigezo cha hasira. Kuna kesho ambayo ni fumbo, pigania haki ya mtoto wako kwa njia sahihi lazima utaipata.

NA ISRI MOHAMED/GPL

Leave A Reply