The House of Favourite Newspapers

Fid Q adunda kifua mbele na heshima ya ZIFF

0

fid-q.jpgNa Boniphace Ngumije, Risasi Jumamosi

Agosti 13 mwaka jana, mwanamuziki wa Hip Hop Bongo, aliyetoka mbali na muziki huo, Fareed Kubanda ‘Fid Q’ aliwapa zawadi ya Wimbo uitwao Kemosabe (Interlude) mashabiki wake na wapenzi wa burudani duniani jambo ambalo ni kawaida kabisa kwa Fid Q kufanya kila mwaka anaposherehekea siku hiyo aliyozaliwa.

Mbali na ngoma mpya hufanya jambo fulani kwa ajili ya jamii na hata wapenzi wa kazi zake.

Akichonga na BMM ya Risasi Jumamosi, Fid amefunguka jinsi atakavyosherehekea siku hiyo leo pamoja na mambo mengine kuhusu kazi yake ya muziki.

BMM: Mashabiki wako watakuwa na kiu kusikia ni zawadi gani umewaandalia leo katika siku yako ya kuzaliwa!

Fid Q: Kiukweli ninasherehekea kama ambavyo huwa nafanya siku zote. Lazima nijitolee na hapa haijalishi fedha au chochote kile kwa kundi ambalo moyo wangu utanipeleka. Lakini pia dunia nzima hutegemea kazi mpya kutoka kwangu, hii itakuwa ni sapraizi ya masikio ya kila

 mmoja atakayebahatika kuisikia.

BMM: Agost 13 inamaanisha umri wako unazidi kusonga, lakini pia kwenye upande wa muziki una muda mrefu, kipi unaweza kukizungumza kuanzia unaanza gemu mpaka leo?

Fid Q: Gemu limebadilika sana lakini uzuri mabadiliko yake hayajahitilafiana kwa namna moja au nyingine na aina ya sanaa ambayo nimekuwa nikiifanya, lakini pia tunashuhudia aina mpya ya Muziki wa Kizazi Kipya wa Singeli ambao mtu akisikiliza vizuri ndani yake atagundua kuwa kuna muziki wa rap.

BMM: Wewe ni kati ya wasanii ambao walikuwa si wepesi kufanya video nje ya nchi, vipi baada ya kufanya video yako ya hivi karibuni ya Walk It Off unampango wa kutoka tena katika kazi zako mpya za hivi karibuni?

Fid Q: Mwaka 2008 nilishuti video ya I am A Proffesional nchini Ujerumani, kwa hiyo siyo kweli kwamba mimi nilikuwa naona uvivu kushuti nje, nilichelewa tu kwenda kushuti Sauzi.

Lakini kitu kizuri baada ya kwenda Sauzi nimetoka kwenye orodha ya wasanii wenye audio kali lakini video mbovu. Nimekuwa msanii mwenye video bora Afrika Mashariki nzima na hayo si maneno yangu bali ya kabineti nzima ya waandaaji wa tamasha linalohusika na masuala ya filamu lenye miaka 19, namaanisha ZANZIBAR INTERNATIONAL FILM FESTIVAL (ZIFF).

BMM: Hivi karibuni serikali imetangaza media ziwalipe wasanii, unalizungumziaje hilo?

Fid Q: Wasanii kulipwa na media ni muhimu na serikali inabidi ilipiganie kwa kila hali jambo hili maana kuna uwezekano ikaongeza mapato kwa kodi zitakazotoka kwenye kazi za wasanii, zaidi haitakisaidia tu kizazi hiki bali hata kijacho kitakula matunda ya wazee wao.

BMM: Matokeo gani chanya unayaona kwa sasa kwenye gemu la muziki Bongo?

Fid Q: Yapo mengi, naziona ‘records lebel’ zinavyokuwa ‘official’ na kuacha kulipana pesa chini ya meza. Lakini thamani ya sanaa inakua kwa kasi.

BMM: Wasanii ambao wamepata mafanikio kwenye siasa unafikiri wana mchango wowote kwenye tasnia ya muziki na wewe una ndoto za kuingia kwenye siasa?

Fid Q: Yaah wanamchango, kwanza wameipa thamani tasnia ya muziki kwa kitendo chao tu cha kufanikiwa kupitia

 majimbo yao. Hata hivyo, napenda kusisitiza kwamba ninaamini ninaweza kuibadilisha jamii yangu kwa kupitia sanaa ninayofanya, siasa si mwarobaini wa mabadiliko na sina mpango wa kujiingiza huko.

BMM: Vipi kuhusu maisha yako ya uhusiano, mashabiki wangependa kufahamu kama umeoa na una watoto wangapi?

Fid Q: Ni kwamba nina familia ambayo huwa natumia muda mwingi kuwa nayo karibu nikiwa free, hilo basi!

BMM:Kutokana na kukua kwa sanaa ya muziki ni changamoto gani unakutana nazo kama mkongwe?

Fid Q: Changamoto zipo nyingi na ninaweza kuzimudu,iwe kwa kukabiliana nazo au kuachana nazo.

BMM: Kupitia mitandao unaingiza kiasi gani kwa mauzo ya nyimbo?

Fid Q: Siwezi kuweka wazi, lakini kumbuka wasambazaji walikataa kukomaa na muziki wetu wa kizazi kipya, ninachoweza kushauri ni watu wenye uwezo kuwekeza kwenye soko la mtandaoni.

BMM: Mwisho kwa ajili ya mashabiki wako!

Fid Q:Ninawataarifu kuwa kuna uwezekano mwaka huu wakapata ile albamu yetu ya tatu iitwayo Kitaa Olojia.

Leave A Reply