FLORA LAUWO ASAIDIA WABONGO, APEWA TUZO UARABUNI

UKIINGIA katika Mtandao wa Google na kuandika jina la Flora Lauwo, utapata maelezo mengi, lakini zaidi utamuona kwenye kusaidia jamii yenye matatizo.

 

Utaona anaendesha harambee za kusaidia wagonjwa waliokata tamaa, wengine hadi kutibiwa nje ya nchi, hususan India. Lakini siyo kwa wagonjwa pekee, Flora kupitia Taasisi yake ya Nitetee anasaidia watu ambao wananyanyaswa kijinsia kwa kuwaibua na kuwapa misaada ya hali na mali.

 

Upo msururu mrefu wa watu ambao wamesaidiwa na Flora. Kutokana na moyo wake wa upendo, kusaidia jamii, Flora haoni shida kusafiri umbali mrefu hadi vijijini kabisa, kuwafuata wahitaji na kufanya sauti zao zisikike. Kutokana na juhudi hizo, Flora amepewa tuzo kadhaa hapa nchini na nyingine katika Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu na hasa Oman, ambao waliweza kumtunuku kazi yake kwa kumpa tuzo.

 

Hivi karibuni, Flora amefanya mazungumzo na mwandishi wa Risasi Jumamosi na kufunguka mengi kuhusiana na majukumu yake ya kila siku. Hapa chini ni sehemu ya mahojiano hayo;

Risasi Jumamosi: Kwanza hongera sana dada Flora kwa kazi yako nzuri unayoifanya kwa jamii.

Flora: Asante… nashukuru sana kwa kweli. Najitahidi kwa kadiri ninavyoweza, mkono wa Mungu nao upo ukinisimamia.

Risasi Jumamosi: Kazi unayofanya ni kubwa sana, ni chagamoto gani unakutana nayo?

Flora: Ni kazi kubwa kweli lakini ukiwa na moyo hakuna linaloshindikana. Changamoto kubwa ni pale unapokutana na watu wenye mitazamo tofauti; wengine wanaweza kukuambia unatafuta kiki nk, lakini hazinikatishi tamaa, naendelea kusonga mbele.

Risasi Jumamosi: Umepata tuzo nchini Oman… ilikuwaje ukapata? Je, ni tuzo ngapi?

Flora: Kwanza nilipata tuzo tatu, moja ilitoka Ubalozi wa Tanzania nchini Oman, nyingine nilipata kutoka kwa wamama watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 40 na ya tatu ni ya wanawake wenye umri chini ya miaka 40. Kule huwa kuna vikundi vingi vya kuhamasisha na kusaidia jamii na hasa vya wanawake. Sasa wao ndiyo walioona kazi zangu na kuamua kunituza.

Risasi Jumamosi: Ulifahamiana vipi na watu wa Oman au ni kupitia vipindi vyako?

Flora: Ndiyo ni hii kazi yangu ya jamii na kuna mtu mmoja wa huko ambaye ni mmoja wa familia yangu, tunaofanya kazi pamoja anaitwa Najat. Unajua watu wa kule wanajua sana kusaidia jamii na wanajitoa sana kwa ajili hiyo.

Risasi Jumamosi: Kwa hapa Tanzania ulishawahi kupata tuzo?

Flora: Ndiyo nilipata ya Malkia wa Nguvu na nyingine ya Woman Achievement niliyopewa na Irene Kiwia.

Risasi Jumamosi: Kwa nini uliamua kufanya kazi hii ya kusaidia jamii?

Flora: Niliamua kwa sababu najua uchungu wa maisha magumu maana hata mimi nilipitia kwenye maisha hayo. Niliamini kupitia sauti yangu nitaweza kuwasaidia wengine.

Risasi Jumamosi: Kwa kazi yako hii, huwa unapata muda wa kuhudumia familia yako?

Flora: Kwa kweli kazi ni ngumu sana na kuna wakati unakuwa kituoni mpaka usiku, basi inakuwa ni shida sana lakini kama mwanamke lazima utimize majukumu yote. Najua namna ya kupanga majukumu yangu ya siku.

Risasi Jumamosi: Najua umeolewa vipi mumeo anazungumziaje kazi unayofanya?

Flora: Namshukuru sana mume wangu na yeye ananipa sapoti kubwa sana katika hilo.

Risasi Jumamosi: Ni kitu gani ambacho huwezi kusahau ulichokutana nacho katika kazi yako?

Flora: Ni siku tulipopelekana polisi na familia ya kijana mmoja tuliyekuwa tunamsaidia, anaitwa Rajabu. Tuliweka namba mbili za kuchangisha, moja yangu na nyingine ya mama wa huyo kijana, akaibuka kaka yake akasema anataka fedha zote zipitie kwake. Hiyo ikawa mtafaruku hadi kupelekana polisi. Lengo la Nitetee ni kuhakikisha mgonjwa anasaidika na michango inayotolewa na wadau, siyo kama alivyokuwa akitaka kaka yake.

Changamoto nyingine, kuna mtoto alikuwa akifanyiwa unyanyasaji kwa kunyimwa haki yake ya kusoma na mambo mengine kama mtoto. Nikaamua kumchukua na kumpeleka kituoni, baba yake na huyo mtoto akaanza kunitishia maisha. Matukio hayo siwezi kuyasahau kamwe.

Risasi Jumamosi: Nini matarajio yako katika taasisi yako?

Flora: Ni kuipanua zaidi ili niweze kuwasaidia watu wengi.

Risasi Jumamosi: Nakushukuru sana kwa ushirikiano wako.

Flora: Asante sana, karibu tena wakati Mwingine

MAKALA: Imelda Mtema


Loading...

Toa comment