visa

Full Story Skendo Mondi, Zari Kulala Hoteli ya Trump

SKENDO mpya mjini inawagusa wazazi wenza, mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na mwanamama mjasiriamali Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Risasi Mchanganyiko lina ‘full story’.

 

WADAIWA KULALA

Mwaka mmoja na miezi kadhaa iliyopita baada ya kutengana kwa kashfa za hapa na pale, wikiendi iliyopita wawili hao walidaiwa kukutana na kulala pamoja katika Hoteli ya Kimataifa ya Trump iliyopo jijini New York, Marekani.

 

Skendo hiyo inaeleza kwamba, wawili hao ambao wamejaliwa watoto wawili, walikutana kimipango nchini humo kwani Diamond au Mondi alikuwa na shoo jijini New York, wakati Zari alikuwa ni Jaji Mkuu wa Shindano la Miss Uganda Northern America 2019 lililofanyika jijini Chicago nchini humo, wikiendi iliyopita.

 

Kwa mujibu wa kurasa za udaku za Instagram, Zari alibahatika kuingia nchini Marekani baada ya miaka kumi ambapo kuna madai kuwa alikuwa na kizuizi cha kuingia nchini humo, lakini haikuelezwa sababu hasa ilikuwa ni nini.

ZARI ATUPIA PICHA

Zari ndiye aliyeanza kutupia picha kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram akionekana nje ya jengo la hoteli hiyo maarufu nchini humo bila kusema kama ni jijini New York au Chicago.

 

MONDI AJIBU MAPIGO

Saa mbili baadaye, Mondi naye alijibu mapigo kwa kutupia picha akiwa ndani ya hoteli hiyo na kutaja mtaa alipo ambao ni Trump Towers 5TH Ave jijini New York.

Baada ya picha hizo ndipo wapenda ubuyu wakajiongeza na kuunganisha nukta kuwa wawili hao walikuwa pamoja ndani ya hoteli hiyo.

 

NDIVYO ALIVYO?

Baadhi ya watu walidai kuwa, ndivyo Mondi alivyo kwani akitaka kurudiana na mpenzi wake huwa anakutana naye nje ya nchi kisha kusawazisha mambo na wakirudi Bongo, watu wanapigwa tu na butwaa kuona mapenzi kedekede.

 

KISA CHA WEMA NA PENNY

Ulitolewa mfano wa kipindi kile aliporudiana na mwigizaji Wema Isaac Sepetu ambapo alikwenda kukutana naye nchini China na waliporejea, aliyekuwa mwandani ya Mondi wakati huo, mtangazaji Penniel Mungilwa ‘Penny’ akajikuta akipigwa na butwaa akiwa hana hili wala lile.

Katikati ya mkanganyiko huo ndipo gazeti hili likazama mzigoni kutafuta ukweli wa skendo hiyo kwani linajua kwamba, Zari alishakula kiapo kwamba hawezi kulamba matapishi yake kwa kurudiana na Mondi.

GAZETI LAJIRIDHISHA

Ijumaa lilijiridhisha kwamba ni kweli kuwa katika mahojiano ya hivi karibuni akiwa nchini Kenya, Zari alitangaza kumsamehe Mondi kwa yote aliyomtendea, lakini hicho hakitoshi kuwa kigezo cha kurudiana. Pia lilijiridhisha kuwa, wikiendi iliyopita Mondi na Zari walikuwa nchini Marekani kwa shughuli zao tofautitofauti.

Kingine lilichojiridhisha wawili hao kutupia picha kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii wakiwa kwenye hoteli hiyo maarufu. Lakini, jambo lingine lilojiridhisha ni kwamba wawili hao hawakuwa hoteli moja isipokuwa Hoteli za Kimataifa za Trump Towers zilizopo kwenye miji yote ya New York na Chicago.

Mtu wa karibu alilithibitishia gazeti hili kuwa, Mondi alikuwa hoteli hiyo ya Trump Tower jijini New York na kwamba hakuwa na mawasiliano yoyote na Zari isipokuwa ilitokea tu kila mmoja kutupia picha na watu kuunganisha nukta.

Uchunguzi wa Ijumaa ulibaini kuwa, Zari alitua jijini Chicago nchini Marekani, Jumatano iliyopita kwa ajili ya kuwa Jaji wa Shindano la Miss Uganda North America 2019 lililofanyika kwenye Ukumbi wa Hyatt Regency huko Chicago.

Kwa upande wake, Mondi alitua nchini humo Ijumaa iliyopita na alikuwa na shoo iliyokwenda kwa jina la Big Apple jijini New York.

HOTELI ZA TRUMP TOWER

Matukio hayo yote yalifanyika usiku wa Agosti 31, mwaka huu isipokuwa yalifanyika miji tofauti ya New York na Chicago wakati miji hiyo yote ikiwa na hoteli kubwa za Trump Tower zinazoelezwa kuwa zinamilikiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Mtu wa karibu na familia ya Mondi aliling’ata sikio gazeti hili kuwa, mambo hayo yote ya skendo zinazoibuliwa ni ili kumtibua mwandani wa sasa wa Mondi ambaye anajifungua muda wowote, Tanasha Donna Oketch.

Alisema wanaoeneza habari hizo ni watu wanaotaka tu kumrusha roho Tanasha na kwamba hawana lolote. Mondi na Zari walikuwa wapenzi ambao ni gumzo kutokana na nguvu zao kwenye mitandao ya kijamii na hata baada ya kutengana bado timu zao zimekuwa zikiendelea kurushiana maneno.

Kabla ya kutengana walijaliwa watoto wawili, mmoja wa kike, Tiffah na Nillan ambao Mondi amekuwa akilalamika kuwa Zari amemnyima kuwaona wanaye. Baada ya kuachana, Mondi yeye aliruka hewani na mtangazaji wa Kenya, Tanasha, wakati Zari yeye alikuwa akidai kuolewa na mwanaume anayemuita King Bae au Mr M ambaye amekuwa akimficha uso akihofia nyakunyaku kupita naye!
Toa comment